Hatutaki miungu watu serikalini-Jaffo

MZALENDO - - HABARI - NA FADHILI ABDALLAH, KIGOMA

NAIBU Waziri Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleiman Jaffo, amesema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kufanya maboresho makubwa katika utumishi wa umma na kuondoa tabia ya umungu mtu inayofanywa na baadhi ya watendaji.

Akizungumza na watumishi wa halmashauri za wilaya, mji na manispaa wakati wa ziara yake mkoani Kigoma, Naibu Waziri Jaffo, alisema serikali inataka kuondoa mtindo wa watumishi kufanya kazi kwa mazoea ili kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kuboresha maslahi yao.

Alisema wapo baadhi ya wakuu wa idara na wataalamu kutokana na utaratibu na mazoea waliyojiwekea muda mrefu wamekuwa wakikwamisha utekelezaji wa majukumu mbalimbali hususan yanayohusu kutolewa fedha.

Jaffo alisema serikali haitavumilia tabia hizo na kwamba kupitia wizara yake wanatarajia kuwafanya watumishi wa umma katika serikali za mitaa kuwa chachu ya kuleta maendeleo nchini.

Pamoja na hilo kiongozi huyo ametaka watumishi watalaamu kutumia taaluma zao na vipaji katika kutekeleza majukumu yao na kutaka watumishi walioonyesha ubunifu na kuleta mabadiliko kupongezwa na kupewa zawadi.

Akizungumzia madai mbalimbali ya watumishi, alisema serikali iko kwenye kipindi cha mpito kuwahakiki ili kuwaondoa watumishi hewa wakiwemo waliokufa na waliostaafu.

“Najua yapo malalamiko mengi ya watumishi kwamba madai yao mbalimbali hayalipwi wala fedha za uendeshaji na miradi haiji, ni kweli serikali imesimamisha fedha hizo kwa muda kupisha uhakiki huo lakini muda si mrefu hilo litamalizika na fedha zitaanza kuingia kwenye halmashauri kutekeleza majukumu yaliyopaswa,”alisema.

Awali akimkaribisha Naibu Waziri, Mkuu wa Wilaya Uvinza, Mwanamvua Mrindoko, alisema ofisi yake inasimamia kwa karibu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Halmashauri na imekuwa ikichukua hatua kila ambapo watumishi wameonekana kutekeleza majukumu yao kinyume cha sheria na utaratibu.

Mkuu wa wilaya alisema taarifa yake kwa Naibu Waziri huyo mkuu huyo wa wilaya alisema watumishi wanakabiliwa na tatizo la kutokuwa na majengo yenye sifa ya kufanyia kazi ikiwemo ofisi ya mkuu wa wilaya na kumuomba Naibu Waziri kusaidia upatikanaji wa fedha zilizopitishwa kwenye bajeti.

Akijibu hilo Naibu Waziri Jaffo alisema serikali imetenga sh. milioni 800 kwa ajili ya ofisi ya mkuu wa wilaya ya Uvinza na kwamba serikali itakapoanza kuruhusu fedha kwenda maeneo mbalimbali.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.