Serikali yazikana ajira 1,000

MZALENDO - - HABARI - NA ATHNATH MKIRAMWENI

SERIKALI imesema madai ya kutangazwa ajira 1,000 yaliyosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ni ya uongo na kuwaomba wananchi kuupuuza uzushi huo. Hatua hiyo inatokana na hivi karibuni kusambazwa kwa tangazo linalodaiwa kuwa ni la serikali lililokuwa likitangaza nafasi mbalimbali za ajira ikiwemo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii lililokuwa na kichwa cha kisomekacho ‘Sekretarieti ya Ajira kutangaza nafasi 1,000’ na kuwataka Watanzania wenye sifa na uwezo kuomba na kujaza nafasi zilizotangazwa.

Akikanusha tangazo hilo, jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Xavier Daudi, alisema aliyesambaza taarifa hizo za uongo aliingia kwenye tovuti ya sekretiati ya ajira na kuchukua matangazo yaliyotolewa Julai 9, mwaka 2015 kwa lugha ya kingereza na Kiswahili.

Aidha, alisema matangazo hayo yalitolewa na Sekretarieti ya Ajira kwa niaba ya waajiri wanne ambao ni Wakala wa Misitu Tanzania, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Katibu Mkuu huyo aliwataka Watanzania kufahamu kuwa matangazo yote ya kazi hutanganzwa kupitia tovuti ya sekretarieti ya ajira, hivyo aliwataka wajiridhishe na matangazo hayo kabla ya kuyafanyia kazi.

Daudi alisema iwapo kila mmoja atakuwa makini na kutafuta uhakika kupitia mamlaka mbalimbali zinazohusika kutasaidia kuondokana na usumbufu usio wa lazima.

Alisema sekretarieti yake kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola itafuatilia ulikoanzia upotoshaji huo ili kuwabaini waliohusika na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

“Tunawaomba radhi kwa niaba ya serikali, wananchi na wadau wetu wote waliopata usumbufu hivyo tunawaomba mvute subira katika kipindi hiki ambapo uhakiki wa watumishi hewa ukiendelea kufanyika,”alisema.

Aliwaasa wananchi kuendelea kuwa watulivu na kusubiri nafasi mbalimbali zitakapotangazwa na serikali pale itakapokuwa tayari,”alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.