Dar imeonyesha mfano kila mmoja aige kutunza mazingira

MZALENDO - - HABARI - NA SOLOMON MWANSELE.

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan,jana, aliwaongoza wakazi wa Dar es Salaam, katika shughuli ya upandaji miti.

Mpango huo wa upandaji miti ni mkakati wa serikali ya mkoa wa Dar es Salaam katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira ambao unasababishwa na ukataji miti kiholela.

Aidha, mpango huo ulikwenda pamoja na uwekaji wa mfumo wa umwagiliaji maji katika bustani za jiji hilo unaotekelezwa kupitia Shirika la Maji Safi na Majitaka mkoa wa Dar es Salaam (DAWASCO.

Akiongoza shughuli hiyo, Makamu wa Rais alimtaka kila Mtanzania kuwa mlinzi wa mwenzie katika kulinda na kutunza mazingira ili kupunguza athari zinazosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Agizo hilo alilitoa huku akisisitiza kwa viongozi wote wa serikali za mitaa, kusimamia sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na kuendelea kuhamasisha wananchi na taasisi mbalimbali miti kwenye maeneo yao.

Makamu wa Rais alisema kutokana na kuongezeka kina cha maji baharini maji hayo yamekuwa yakihamia nchi kavu na kusababisha uharibifu wa makazi pamoja na mazao.

Utafiti mbalimbali uliofanyika umeonyesha kuwa, hewa ya ukaa ina asilimia kubwa katika ongezeko la gesi joto hivyo husababisha kumong’onyoka kwa tabaka la ozoni.

Kuharibika kwa tabaka hilo husababisha ongezeko la la joto duniani na hatimae kuchangia mdororo wa kiuchumi kutokana na kuathirika kwa shughuli za uzalishaji mali.

Takwimu zinaonyesha kuwa sekta ya misitu imechangia kwa asilimia 17 hadi 20 ya utoaji na mrundikano wa hewa ukaa dunia.

Jijini Dar es Salaam utafiti mbalimbali ulibainisha kuwa, hewa ya ukaa imeongezeka kutokana na ongezeko la viwanda na idadi kubwa ya wakazi.

Ukataji holela wa miti pia kumesababisha athari nyingi kwa upande wa makazi na mazao hususan katika mikoa ya Pwani ambayo miaka ya hivi karibuni ilikumbwa na mafuriko makubwa yaliyosababisha kuharibika kwa miundombinu, magonjwa ya mlipuko na uharibifu wa makazi.

Kutokana na takwimu hizo tunaunga mkono jitihada za serikali ya mkoa wa Dar es Salaam kwa kutoa kipaumbele suala la upandaji miti ili kunusuru mazingira.

Wakati Dar es Salaam ikijikionyesha kwa vitendo umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingiza ni muhimu kwa mikoa mingine kuiga kile kilichofanyika Dar es Salaam ili kuhakikisha juhudi za utunzaji wa mazingira linakuwa ni la nchi nzima.

Matukio ya kukithiri kwa ukataji miti bila kufuata utaratibu ikiwemo kupanda miti mingine kwa kiasi Fulani huchangiwa na usimamizi mdogo unaofanywa na mamlaka zilizopewa dhama ya usimamizi.

Ni muhimu sasa kila mmoja kutambua umuhimu wa kuhifadhi mazingira ikiwa ni pamoja na kupanda miti pia kujiepusha uharibifu kwa kukata miti kiholela kwa kuwa kufanya hivyo ni kuchochea nchi kuwa jangwa.

HATIMAYE ile sintofahamu ya muda mrefu, juu ya uhalali wa Pierre Nkulunzinza, kuwa Rais wa Burundi imepatiwa ufumbuzi na mahakama, ambacho ndicho chombo cha kisheria chenye jukumu hilo muhimu kwa ustawi wa nchi hiyo jirani na mwanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki..

Rais Nkulunzinza amethibitishwa na Mahakama, kuwa yuko madarakani kihalali. Mahakama iliyoa uamuzi huo ni ile ya Katiba ya Afrika Mashariki (EACJ), kutokana na kesi iliyofunguliwa dhidi yake na asasi tatu za kiraia za Burundi, ambazo zilidai amejiogezea muda wa uongozi kinyume cha Katiba.

Ikumbukwe mwezi Mei, mwaka jana, kulitokea jaribio la kumpindua Rais Nkulunzinza, lililoongozwa na Meja Jenerali Godefroid Niyombane.Hata hivyo, jaribio hilo lilizimwa na vikosi vitiifu vya serikali, na kupelekea kutokea kwa mauaji na wananchi wengine kulazimika kukimbilia nchi nyingine kama wakimbizi.

Hukumu hiyo ilisomwa Septemba 29, mwaka huu na Jaji Isack Lenaola, ambayo ilithibitisha uhalali wa Rais Nkulunzinza kuendelea kuongoza nchi hiyo kwa awamu ya tatu kwa mujibu wa Katiba.

Jaji Lenaola alisema walalakaji katika kesi hiyo, aliowataja kuwa ni Jukwaa la Asasi za Vyama Vya Kiraia katika nchi za Afrika Mashariki (EACSOF) na Chama Cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS),hawakukidhi kigezo cha kisheria kufungua kesi na kwamba ilifunguliwa nje ya wakati.

Naam, sasa ni muda wa wananchi wa Burundi kuganga yajayo kwa kuhakikisha kwamba, mnaendelea kuijenga nchi yenu badala ya kuendelea kulumbana na kupelekea mauaji kwa raia wasio na hatia huku mkizalisha wakimbizi.

Kamwe msikubali kuendelea kudanganywa na vikundi vya watu wachache wenye maslahi yao binafasi na siyo ya umma wa Warundi, walio wengi ili muendeleze choko choko na visasi ambavyo mwisho wa siku vinaifanya nchi yenu izidi kugawanyika vipande.

Mahakama tayari imeishatoa hukumu, hivyo ni vyema wote wakaheshimu uamuzi huo wa chombo hicho cha sheria, kwa maslahi mapana ya wananchi wa Burundi, ambao nina hakika kuwa hawapendi kuwa wakimbizi ama kuona ndugu na jamaa zao wakiuwa kikatili kwa visa vya kisiasa.

Msivipe nafasi visasi vya kisiasa, kwani nina hakika na huu ndiyo ukweli halisi ninaowaaambia, kwamba mtaigawanya nchi yenu vipande, jambo la msingi hapa ni kusahau yaliyopita na kuganga haya yaliyopo, ambayo ni kumpa ushirikiano Rais Nkulunzinza, ili aweze kutekeleza yale aliyowaahidi.

Siku zote kujenga amani na umoja wa kitaifa ni kazi ngumu, na inayoweza kuchukua hata miongo kadhaa kuifanikisha, lakini kuivunja ni jambo linalochukua sekunde chache tu, na kuifanya nchi kushindwa kutawalika, huku mamia ya wananchi wake wasio na hatia wakijikuta wanapoteza maisha kikatili.

Wananchi wa Burundi, itumieni humu hii iliyotolewa kuwa fundisho kwenu, kwani ndani ya miaka hii miwili, nyie wenyewe ni mashuhuda ya watu wangapiwakiwemo viongozi wenu, wamekufa kwa mauaji yaliyoonekana dhahiri shahiri kuwa ni visasi vya kisiasa.

Ni muda sasa wa kukaa mezani na kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu zile changamoto ambazo mnaziona zinaweza kuwa kikwazo, lakini kamwe msikubali kuipa nafasi roho ya visasi kwa upande mmoja kumwaga mboga na mwingine nao kuamua kumwaga ugali.

Nawasihi wananchi wa Burundi, msikubali kabisa kuiingiza nchi yenu kwenye vita vya wenyewe kwani nyie ni mashahidi wa vita vya aina hiyo na pia mnayajua kikamilifu madhara yake kwenu, kwani mmepitia huko, sasa msikubali kurudi.

Mpeni ushirikiano wa kutosha Rais Nkulunzinza na serikali yake iliyopo madarakaili aweze kutekeleza ahadi alizozitoa kwenu wakati wa uchaguzi, ili amalize kipindi chake cha uongozi nchi yenu ikiwa imetengamaa kisiasa na kiuchumi.Mnatakiwa kuilinda na kuienzi amani na utulivu ndani ya Burundi.

suney27@yahoo.com

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.