Wafamasia waiomba serikali udahili wa wanafunzi ufundi

MZALENDO - - HABARI - NA LILIAN JOEL, ARUSHA

CHAMA cha Wafamasia Tanzania (PST), kimeiomba serikali kuongeza udahili wa wanafunzi wa ufundi dawa na fundi dawa wasaidizi ili wawasaidie w a f a m a s i a walioko kazini katika utoaji wa dawa sahihi kwa wagonjwa.

Akizungumza jana jijini hapa katika Kongamano la wafamasia, Rais wa Chama hicho, Michael Kishiwa, alisema idadi ya wafamasia nchini ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya wananchi wenye uhitaji wa uangalizi wa kifamasia.

“Jumla ya wafamasia hapa nchini ni 1,200, ambapo kwa mahesabu ya haraka kila mfamasia anatakiwa kuhudumia zaidi ya wananchi laki tano jambo ambalo siyo sahihi.

“Nitumie fursa hii kuimba serikali kudahali wanafunzi wengi zaidi ili kuboresha huduma zinazotolewa na wafamasia katika maeneo mbalimbali hapa nchini,” alisema.

Kishiwa alisema kazi kubwa ya chama chao kuhakikisha inasimamia ubora wa utoaji huduma ya dawa na kusimamia maadili, ili wananchi wapate dawa sahihi na kuzitumia ipasavyo.

Alisema licha ya changamoto, hiyo pia wanakabiliwa na kutokuwepo kwa kitengo katika wizara ya afya kwa ajili ya kushugulikia masuala ya wafamasia.

Michael alitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na mazingira duni ya kufanyia kazi hali, ambayo inawafanya wafamasia wengi kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo.

Kwa mujibu wa Kishiwa baadhi ya wafamasia wamekosa uandilifu ambapo wanaiba dawa kutoka maduka ya dawa ya serikali na kuwauzia wafanyabiashara wa dawa hizo, jambo ambalo ni kinyume na maadili.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka wafamasia wote nchini kuzingatia maadili ya kazi zao za kila siku ili kuboresha huduma hiyo muhimu kwa afya ya binadamu

Naye, Mkuu wa Mkoa Arusha, Mrisho Gambo, akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, alisema serikali katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora ya dawa imeanza kufanya marekebisho ya sera ya uanzishwaji viwanda vya madawa nchini.

“Endapo tutazalisha dawa zetu wenyewe nyingi iwezekanavyo, itatupunguzia gharamazisizozalazimakuagiza dawa nje ya nchi, sambamba na hili pia tunaboresha vyuo vya Wafamasia ili waweze kutoka wataalamu bora wa masuala haya ya madawa,” alisema.

Kwa upande wake, Msajili wa Baraza la Wafamasia, Elizabeth Shekalage, alisema kwa sasa wananchi wengi wamechukulia huduma ya dawa ni biashara huria wakati huo ni wito.

Alisema baraza limejipanga kupambana na watu wanaofanya huduma hiyo ni biashara na kuchakachua maadili.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.