Mpango Mkakati ulivyodhamiria kuzing’arisha Mahakama nchini

MZALENDO - - HABARI - NA FURAHA OMARY

TAASISI, kampuni au shirika lolote linalohitaji maendeleo, lazima liwe mpango mkakati ambao utaliongoza na kutoa mwelekeo wa kule linapohitaji kwenda katika kufikia maendeleo ama mafanikio.

Hatua hiyo inatokana na umuhimu wa Mpango Mkakati, kwa kuwa unasaidia kujua nyenzo zinazohitajika, hivyo kuchukua jitihada ya kuzitafuta na kutathimini kama lengo la taasisi, kampuni, shirika au jumuia limefanikiwa ama la kwa muda uliopangwa.

Licha ya hayo, Mpango Mkakati umekuwa ni mwongozo kwa taasisi, shirika, kampuni ama jumuia katika kuhakikisha inafikia dira yake iliyojiwekea katika kupata mafanikio au maendeleo.

Hivi karibuni Mahakama ya Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa taasisi ama mihimili ya nchi iliyoweza kuwa na Mpango Mkakati baada ya kuzuindia Mpango wake Mkakati wa miaka mitano 2015-2020, unaolenga kuboresha huduma za kimahakama nchini huku ikiongozwa na Dira ya ‘Haki kwa Wote na kwa Wakati’.

Uzinduzi wa Mpango Mkakati huo ulienda sambamba na uzinduzi wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za mahakama ambao ni mradi shirikishi baina ya Serikali ya Tanzania, Mahakama ya Tanzania na Benki ya Dunia.

Wakati wa halfa ya uzinduzi wa Mpango Mkakati huo na Mradi wa Maboresho ulifanyika katika Mahakama ya Kibaha, mkoani Pwani ambayo imejengwa kisasa na kuhudhuriwa na Jaji Mkuu, Mohammed Chande Othman na viongozi wengine huku mgeni rasmi akiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Jaji Mkuu anasema Mpango Mkakati huo unaingia katika Mpango wa Taifa na Dira ya Taifa ya Maendeleo ambapo mambo mengi yanakwenda sambamba na kwamba Mpango Mkakati huo utagharimu sh. bilioni 238 na Mradi wa Maboresho utagharimu sh. bilioni 140.

Anasema mpango mkakati huo utakuwa dira yao na mwelekeo wao, ambao una nguzo tatu muhimu ambazo ni utawala bora na uwajibikaji na menejimenti ya rasilimali, fursa ya kutoa na kupata haki na uharakishaji wa mashahuri ambapo kwa pamoja umekusudia kutoa haki kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, (wa kwanza kushoto), Naibu Spika Dk. Tulia Ackson Mwansansu (wa tatu kulia), wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo na wa kwanza kulia ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Ferdinand Wambali.

wote na kwa wakati, pia una maeneo ya matokeo makubwa manane na malengo 17. Anasema pia ipo nguzo ya kuongeza imani kwa wananchi juu ya mahakama na kama mhimili wa kutenda haki. Anabainisha Mahakama ya Tanzania ilijipima na kuweka dira yake ambayo ni; ‘Haki kwa Wote na kwa Wakati’ kwa kuwa kila taasisi, shirika na kampuni ambayo inataka mafanikio lazima iweke dira hivyo kwa upande wao wanataka wafikie wakati mtu yoyote akileta shauri litapata haki sawa na kwa wakati.

Jaji Mkuu anayataja maeneo manane ya matokeo makubwa yaliyoko katika mpango huo kuwa ni mageuzi ndani ya mahakama katika kufanya kazi, ambapo imejipanga kutumia zaidi teknolojia kumaliza mashauri, kuboresha mfumo wa utendaji kazi kwa majaji, mahakimu, wasajili na watumishi wengine.

Katika matokeo hayo makubwa, Mahakama ya Tanzania imejipanga kuongeza ubora wa hukumu kwani inataka haki iliyo bora na sio bora haki na kuimarisha ukaguzi wa mahakama za Mwanzo, Wilaya na Hakimu Mkazi.

Kuhusu mradi wa Maboresho ya Huduma, Jaji Mkuu anasema lengo lake ni kuimarisha na kujenga miundombinu ya mahakama, kuongeza wafanyakazi, kuimarisha Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ili kiwe chenye hadhi na kitoe mafunzo kwa maofisa wa mahakama na wadau wengine.

Jaji Mkuu anasema

mahakama inataka kuimarisha na kujenga miundombinu kwa kuwa asilimia 47 ya Watanzania hawana fursa sawa ya kupata haki ya Mahakama Kuu kwa sababu wanaishi katika mikoa isiyo na mahakama hizo.

“Serikali imeliona hilo, hivyo imetuwekea nguvu na kwa kupitia Benki ya Dunia kwa kutuwezesha kupata fedha ili asilimia hiyo ya Watanzania ambayo inakosa haki hiyo kuweza kuipata tena kwa wakati,” anasema.

Anasema kuna wilaya na mikoa ambayo haina Mahakama za Mwanzo na za Mikoa, hali inayowafanya kusafiri kutoka wilaya moja kwenda nyingine, hivyo kupitia mradi huo, Watanzania watapata fursa ya kupata huduma hizo na kuboresha majengo ya mahakama.

“Hii fursa tunataka kila wilaya na mkoa uwe na Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu yake. Mpango huo tunaenda nao kwa kasi mikoa na mradi huu wa maboresho utatusaidia kufikia malengo yetu,” anasema.

Anasema Mahakama ya Tanzania imejipanga katika kuongeza imani kwa Watanzania kwasababu bila ya hivyo, wanaweza wasihudhurie wakati inapotolewa hati ya kuwaita kutoa ushahidi, kama hawana imani haki haitatendeka.

Jaji Mkuu anasema Mahakama itaongeza imani kwa wananchi kwa kuwashirikisha ambapo itawasikiliza na kuwapa fursa ya kutoa mapendekezo kwani nia yao ni kuwaondolea usumbufu kwa wale wanaofika kupata huduma na wasiofika.

Mafanikio na mipango ya Mahakama

Akielezea kuhusu mafanikio iliyoyapata Mahakama ya Tanzania, Jaji Mkuu anasema wamejenga zaidi ya Mahakama za Mwanzo 70 kwa mwaka huu na wanampango wa kujenga Mahakama ya Wilaya 20.

Jaji Mkuu anasema tayari mradi huo umewezesha kujengwa kwa Mahakama tano za kisasa zilizopo katika maeneo ya Kibaha, Kawe, Kisarawe, Kigamboni na Bagamoyo ambazo zitakuwa mfano wa uanzishwaji wa Mahakama za kisasa nchini.

Anasema Mahakama ya Tanzania imejipanga kuhakikisha inaongeza idadi ya mahakama zake ili kuondokana na tatizo la upungufu wa mahakama katika ngazi zote.

Jaji Mkuu anasema Mahakama inatarajia kujenga majengo ya Mahakama Kuu matano hadi saba ili kupunguza umbali wa upatikanaji wa huduma hiyo kwa mikoa isiyo na Mahakama Kuu kwa kuwa takwimu zinaonesha kwamba kati ya mikoa 25 ya Tanzania Bara ni mikoa 14 tu ndiyo yenye Mahakama Kuu.

Anaitaja mikoa isiyokuwa na Mahakama Kuu kuwa ni Lindi, Katavi, Geita, Simiyu, Njombe, Songwe, Singida, Manyara, Pwani na Morogoro.

Kwa upande wa Mahakama za wilaya, Mahakama itakuwa na uwezo wa kujenga mahakama kati ya 30 hadi 40, mahakama za Hakimu Mkazi kati ya tano hadi nane na aina mbalimbali za mahakama za Mwanzo kati ya 70 hadi 100 katika kipindi cha mwaka mmoja kwa kutumia teknolojia ya ujenzi ya kisasa.

Akizungumzia upatikanaji na utoaji wa haki kwa wakati, Jaji Mkuu anasema hadi kufikia Agosti 30, mwaka huu, Mahakama kwa ngazi zote, imefanikiwa ndani ya miaka mitatu kufikia lengo la kuwa na mashauri asilimia 80 yenye umri unaokubalika kimataifa wa kati ya miezi 6 hadi 24.

Anabainisha katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 Mahakama inalenga kuondoa mashauri yote ya zaidi ya miezi miezi mitatu hadi sita kwa Mahakama za Mwanzo, Wilaya na zile za Hakimu Mkazi (Mkoa) ili kuwa na asilimia 90 ya mashauri yote yaliyoko kwenye ngazi hizo za Mahakama yawe ndani ya miezi 3-6.

“Nguvu kubwa inaelekezwa huko kwa kuwa ndiko kwenye Watanzania zaidi ya asilimia 80,” anasema.

Waziri Mkuu: Mahakama ya Tanzania mfano wa kuigwa

Akizindua mpango na mradi huo, Waziri Mkuu, Majaliwa amezitaka taasisi za serikali kuiga mfano wa Mahakama ya Tanzania katika kuwapatia wananchi huduma bora na kwa wakati.

Majaliwa ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kufanikisha uandaaji wa Mpango Mkakati unaolenga katika kuimarisha Utawala bora, Upatikanaji na utoaji wa haki kwa wakati na kuimarisha imani kwa wananchi na Ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za mahakama.

Anasema Mpango Mkakati wa Mhimili huo sio tu kwamba ni muhimu kwa Mahakama bali pia ni muhimu kwa Serikali na Watanzania wote kwa ujumla kwa kuwa umelenga katika kuboresha huduma zinazotolewa na Mahakama katika ngazi zote na kuzisogeza karibu na wananchi.

Waziri Mkuu anasema azma ya Mahakama ya kuandaa Mpango Mkakati inakwenda sambamba na malengo ya Serikali ya kudhamiria kuimarisha mfumo wa utoaji haki kwa kufanya maboresho katika utendaji wa vyombo vya maamuzi ikiwemo Mahakama.

Majaliwa aliishukuru Benki ya Dunia kwa kukubali kuikopesha Tanzania sh. bilioni 141 zitakazosaidia kuboresha Huduma za Mahakama katika kipindi cha miaka mitano.

Aidha, ameihakikishia Benki ya Dunia kuwa serikali kupitia Mahakama itatumia fedha hizo kwa uangalifu na uaminifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.