Wasomi wakunwa kasi ya ukuaji uchumi

Wasema ni matokeo ya kubana mianya ya upotevu wa mapato Wataka vijana wajikite kwenye uzalishaji na kuacha uchuuzi

MZALENDO - - MBELE - NA JACQUELINE MASSANO

BAADHI ya wasomi nchini wameipongeza serikali kwa kuimarisha pato la taifa ikiwa ni pamoja na kuziba mianya yote ya ukwepaji wa kulipa kodi.

Pongezi hizo zimekuja baada ya mwishoni mwa wiki iliyopita kuripotiwa kuwa uchumi wa taifa umeimarika na kuiwezesha serikali kujiendesha na fedha zake ikiwa ni pamoja na kulipa madeni ya ndani kiasi cha sh. bilioni 96.

Akizungumza na Uhuru jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk.Benson Banna, alisema ukuaji wa uchumi umeashiria taifa kupiga hatua kubwa za kimaendeleo zitakazosaidia kuondokana na utegemezi.

Aidha, alisema ukuaji huo umeakisi vigezo vya kimataifa vinavyopaswa kutumika hivyo maneno ya upotoshaji yanayotolewa na baadhi ya watu hayana ukweli.

“Watu wamekuwa wakipiga maneno yasiyokuwa na tija. Ukuaji wa uchumi

haupimwi kwa kuzingatia uchumi wa mtu au wa kaya moja. Zipo kanuni za kimataifa zinazozingatiwa nchini kuakisi ukuaji huo kama ambavyo mataifa mengine yanavyofanya,” alisema.

Alifafanua kuwa vijana wanapaswa kujikita kwenye uzalishaji ili kwenda sambamba na ukuaji wa uchumi na kuacha kufanyabishara za kichuuzi ambazo hazina tija kubwa kwenye ukuaji wa uchumi.

Kwa mujibu wa Dk. Bana ni muhimu kwa wananchi kuunga mkono juhudi za serikali ikiwemo za ukusanyaji kodi ili kufanikisha jitihada za ukuaji wa uchumi.

Naye,Mhadhiri na mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk.Timothy Lyanga, alisema aliipongeza serikali kwa kudhibiti vyanzo vya rushwa ambavyo vimepelekea kukua kwa uchumi.

Alisema katika awamu iliyopo, makusanyo ya mapato yamekuwa mazuri kutokana na kudhibiti vyanzo vya rushwa.

“Kwa kiasi kikubwa mapato yalikuwa yanapotea lakini sasa yamedhibitiwa…kwa maana hiyo makusanyo yamekuwa halali. Kwa sababu yalikuwa yanapotea kwa njia ambazo si halali,” alisema.

Dk. Lyanga alisema moja ya maeneo ambayo yameweza kuchangia ukusanyaji wa pato la taifa kama kodi yameimarika zaidi kwa sababu hakuna udanganyifu tena.

Alisema awali fedha nyingi zilikuwa zinaingia kwenye mifuko ya watu binafsi lakini sasa hivi hali hiyo imedhibitiwa.

“Serikali ilipoziba mianya yote ya rushwa na ujanja ujanja nayo imechangia kuongezeka kwa pato la taifa,” alisema.

Kuhusu usafiri wa basi za mwendokasi katika jiji la Dar es Salaam, alisema umechangia kutatua tatizo kubwa la usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam pamoja na kuliigizia taifa mapato.

“Hivi sasa serikali inapata asilimia yake kupitia Udart, na hivyo kujaziliza pato la taifa…hapo mwanzo watu walikuwa wanadanganya kupitia njia ya usafiri na fedha ikawa haionekani,” alisema.

Alisema hivi sasa mapato yanayolipwa kama kodi ni halali kutokana na kila mmoja kuwajibika katika ulipaji.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk.Francis Michael, alisema katika kipindi hiki kifupi ambacho serikali ya Awamu Tano imeingia madarakani imefanikiwa kuziba mianya mingi ya ukwepaji kodi na rushwa.

“Zile fedha zote ambazo zilikuwa zinapaswa ziingie kwenye mfuko wa taifa zimeweza kuongezeka kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Alisema kama pato la taifa limeongezeka, serikali inaweza kupata nafasi ya kuboresha huduma ya jamii kwa kujenga barabara, kununuliwa kwa ndege, kuboresha madawati na hata huduma za hospitali.

“Kukua kwa pato la taifa kunachochea uchumi pia,” alisema.

Alisema vigezo vya upimaji vya uchumi vimepanda kutokana na vyanzo hivyo vya mapato kuongezeka.

Hata hivyo, Dk. Michael aliishauri serikali kuendeleza juhudi za ukusanyaji kodi ikiwa ni pamoja na kupunguza uagizaji wa vifaa kutoka nje ya nchi. Alisema iwapo serikali itapunguza uagizaji wa vifaa kutoka nje itapunguza kutoa fedha za kigeni kwenda nchi za nje.

Aidha, alisema serikali ijitahidi kujenga viwanda vya kusindika matunda, na vya kuhifadhia mazao ambayo yanaharibika kama nyanya ili visaidie kukuza pato la taifa.

“Kwa mfano kipindi hiki nyanya zimelimwa nyingi na zinaharibika kama tungekuwa na viwanda vingesaidia kuifadhi na tukaziuza nje na kuchangia pato la taifa,” alifafanua.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ilitoa tathimini ya za kiuchumi na kuonysha kwamba pato la taifa limeongezeka kwa asilimia 7.9 kutoka asilimia 5.8 na jumla ya thamani ni sh. trilioni 11.7 ikilinganishwa na sh. trilioni 10.9 mwaka jana.

Pia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kupitia Gavana Benno Ndullu nayo ilitoa tathimini yake na kuweka bayana kuwa uchumi wa taifa umekua kwa kipindi cha robo mwaka huku serikali ikijiendesha kwa fedha zake kwa kipindi hicho na kulipa madeni ya ndani kiasi cha sh. bilioni 96.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.