Majaliwa ashtukia kodi juu

MZALENDO - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameliagiza Baraza la Madiwani la Manispaa ya Dodoma, kufanya marekebisho ya kodi inayotozwa kwenye soko la Majengo, ambayo imepandishwa kutoka sh. 20,000 hadi sh. 150,000 kwa mwezi.

Amesema hakubaliani na ongezeko hilo ambalo ni sawa na asilimia 650 kwa kuwa linawaumiza wananchi.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa agizo hilo jana, alipotembelea soko hilo akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini Dodoma.

Alisema soko hilo linatakiwa lifanyiwe mapitio ili liwekwe kwenye hali nzuri na manispaa ihakikishe maboresho hayo yanafanyika bila ya kuwaumiza wafanyabiashara.

“Kwa kuwa uamuzi wa kupandisha kodi ulifanyika kisheria na kupitishwa na Baraza la Madiwani,

sitaki kuvunja sheria. Nawaagiza mkazungumze tena katika baraza na muangalie namna ya kupunguza gharama hizo.

“Hali hii haiwezekani kuachwa iendelee, huku ni kuwaumiza wananchi. Mkurugenzi wa Manispaa nenda kaitishe tena kikao, mfanye mazungumzo upya kwenye baraza lenu na mje mnieleze mmekubaliana nini,” alisisitiza.

Pia, aliitaka manispaa hiyo ihakikishe makusanyo yote ya fedha katika soko hilo yanafanyika kwa njia ya kielektroniki ili fedha hizo ziweze kuleta tija na kuwataka Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kuwachukulia hatua wote watakaobainika kuiba fedha hizo.

Alisema manispaa hiyo inatakiwa kupanua masoko kwa kujenga mengine mapya makubwa kwenye maeneo ya Nkuhungu, Kisasa, Mlimwa na Barabara ya Iringa ili huduma hizo zisambazwe.

Mapema akisoma risala yake, Mwenyekiti wa Soko hilo, Godson Rugazama, alimueleza Waziri Mkuu changamoto zinazolikabili soko hilo ni pamoja na ongezeko la kodi isiyozingatia uhalisia wa maisha na shughuli za wajasiriamali sokoni hapo.

Mwenyekiti huyo alitaja changamoto nyingine kuwa uchakavu wa mifereji ya maji machafu, kuvuja kwa paa la soko, bidhaa kuuzwa katika maeneo yasiyo rasmi na kusababisha wateja kutoingia sokoni.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kukagua maeneo mbalimbali zikiwemo wodi, jengo la wazazi na jengo jipya la wagonjwa wa Bima ya Afya (NHIF).

Akiwa hospitalini hapo, pia alizungumza na watumishi wa sekta ya afya na kuwataka wawahimize wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao unawezesha kulipia bima ya matibabu kwa mchangiaji mwenza wake na watoto au watemezi wanne ambapo serikali hujazia kiasi kama

alichochangia mhusika.

Akizungumzia miundombinu ya afya mkoani humo, Waziri Mkuu alisema mkoa wa Dodoma hauna shida ya matibabu au utoaji wa huduma hiyo kutokana na miundombinu iliyopo hivi sasa.

Aliwaasa watumishi kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu na kuongeza tija.

“Ninawasihi mjenge tabia ya huruma kwa wagonjwa huku mkitambua unyeti wa kazi mliyonayo. Naamini mtatunza vifaa mlivyonavyo na si kuvichukua na kuvipeleka kwenye zahanati zenu au maduka yenu binafsi ya dawa,”alionya.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.