Tutunze mazingira kwa uhai wetu-Samia

MZALENDO - - MBELE - NA JESSICA KILEO

MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan, amezindua kampeni ya upandaji wa mti yenye kauli mbiu ‘Mti Wangu’ na kuwataka wakazi wa jiji la Dar es Salaam kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzie katika kulinda na kutunza mazingira ili kupunguza athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Pia, amewataka viongozi wote wa serikali za mitaa kusimamia sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na kuendelea kuhamasisha watu kupanda miti katika maeneo yao.

Aidha, alisema kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari maji yamekuwa yakihamia nchi kavu na kusababisha uharibifu wa makazi pamoja na mazao ambayo yanatokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Samia aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizindua kampeni hiyo maeneo ya Barabara ya Kilwa.

Alisema akiwa kama msimamizi wa masuala yote ya mazingira nchini, anafarijika kuona kampeni hiyo kwa kuwa miti ina mchango mkubwa katika uhifadhi wa mazingira hususan katika suala zima la kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

“Wote tunafahamu kuwa mabadiliko ya Tabia nchi hutokana na shughuli za kibinadamu ambazo husababisha kuongezeka kwa kiwango cha gesi joto.

Ongezeko hili la gesi joto husababisha mabadiliko ya tabia nchi na hivyo kuleta changamoto kubwa ya ukuaji wa uchumi, ustawi wa jamii na maendeleo endelevu hususan katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania,” alisema.

Hata hivyo, alisema madhara hayo yameonekana duniani kote katika mazingira, afya, uchumi, maliasili na miundombinu.

Alisema tafiti zimeonyesha hewa ya ukaa ina asilimia kubwa katika gesi joto, hivyo husababisha kumong’onyoka kwa ozone na kupelekea kuongezeka kwa kiasi cha joto dunia na kuathiri uchumi wa nchi.

Samia alisema sekta ya misitu imechangia kwa asilimia 17 mpaka 20 ya utoaji na mrundikano wa hewa ukaa dunia na kwamba anatambua athari za ongezeko la gesi joto hususan gesi hewa ukaa na kuunga mkono juhudi za dunia zilizofikiwa katika makubaliano ya Paris ya kunusuru joto la dunia lisiongezeke zaidi ya nyuzi joto mbili.

Pia alisema serikali kupitia mkoa wa Dar es Salaam imekuja na kampeni hiyo ya kupanda mti ili kukabiliana na changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi.

Samia alisema tafiti mbalimbali katika jiji hilo zinaonyesha hewa ya ukaa imeongezeka kutokana na kuongezeka kwa viwanda na idadi kubwa ya wakazi.

“Utafiti wa mkoa wa mwaka 2015 ulionyesha mkoa una viwanda 1,854 kati ya hivyo 480 ni vikubwa na vidogo ni 1,374. Pia idadi ya wakazi inatarajiwa kufika milioni 5.89 kwa mwaka 2017 ambayo itaongeza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa hewa ya ukaa kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya nishati, chakula, usafiri, uzalishaji viwandani na kuanzishwa kwa maeneo mapya ya makazi hivyo kukata miti,” alisema.

Makamu wa Rais alisema kutokuwa na miti pia kumesababisha athari nyingi kwa upande wa makazi na mazao hususan katika mikoa ya Pwani ambayo miaka ya hivi karibuni ilikumbwa na mafuriko makubwa na hivyo kuharibika kwa miundombinu, magonjwa ya mlipuko na uharibifu wa makazi.

Mbali na hilo, alisema kwa wakulima mabadiliko ya misimu ya mvua na ukame kwa mikoa ya Pwani, wameendelea kupoteza nyenzo za kiuchumi kama utalii na uvuvi kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari na kumezwa kwa fukwe.

Samia alisema huku akinukuu kauli ya Papa Francis katika mkutano wa pili wa Lishe Duniani uliofanyika mwaka 2014 mjini Roma, kwamba ‘Mungu anasamehe lakini mazingira hayasamehe’.

Alibainisha kuwa neno hilo lina maana ya tunza mazingira yakutunze na wewe, kupanga ni kuchagua basi kila mmoja achague mti wake.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliwataka vingozi waliopewa kazi ya kusimamia miti hiyo kuhakikisha inastawi na kwamba ikifa watakuwa wamejivua vyeo walivyo navyo.

Pia alisema mtu yeyote atakayebainika kugonga vyuma vilivyowekwa pembeni mwa barabara, akigonga chuma kimoja atalipa kumi na atakayebainika kuiba vyuma au minyororo iliyopo atawajibishwa kwa kosa la wizi wa wilaya nzima husika.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.