Viongozi washikiliwa kwa tuhuma za wizi

MZALENDO - - HABARI - NA LILIAN JOEL, ARUSHA

JESHI la Polisi mkoani Arusha linawashikilia watu watatu kwa kosa la kughushi nyaraka za ofisi na kusababisha wizi wa sh.milioni 50 za Chama cha Wakulima cha Tanganyika (TFA).

Kushikiliwa kwa watuhumiwa hao kumekuja siku chache baada ya polisi kumshikilia na kisha kumwachia kwa dhamana aliyekuwa mwenyekiti wa bodi ya muda ya TFA, Meynard Swai, kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali na fedha za chama hicho.

Mwenyekiti huyo alishikiliwa na polisi mkoani hapa Septemba, mwaka huu, ambako alihojiwa na kuachiwa kwa dhamana huku polisi wakiendelea na uchunguzi.

Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema watuhumiwa hao walikamatwa na kushikiliwa katika maeneo tofauti hapa nchini.

Aliwataja walioshikiliwa kuwa ni Salvatory Mwandu, Simon Mwandu na mkazi wa jijini Dar es salaam, Jesca Canisius ambao kwa sasa wameachiwa kwa dhamana.

Mkumbo alisema watuhumiwa hao wako nje kwa dhamana na kwamba uchunguzi wa madai yao unaendelea.

Alilisisitiza kwamba polisi haitasita kumchukulia hatua za kisheria yeyote atakayevunja sheria za nchi.

“Jeshi la polisi linaendelea na upelelezi wa tuhuma hizo na linatoa rai kwa wananchi wote wa mkoa wa Arusha kuacha vitendo vinavyovunja sheria za nchi kwa kuwa wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria,”alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.