Mwinyi awataka viongozi wa dini kuhubiri amani

MZALENDO - - HABARI - NA SYLVI SEBASTIAN

RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ally Hassan Mwinyi, amewataka viongozi wa dini kudumisha upendo, mshikamano na mahusiano mazuri ili kulinda amani iliyopo.

Wito huo aliutoa juzi Dar es Salaam katika mkutano mkuu wa 47 wa Jumuia ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania

Mwinyi alisema amevutiwa na jumuia hiyo kuandaa mkutano huo kwa kuwa hatua hiyo inaashiria kuzingatia misingi sahihi ya Uislamu ambayo ni pamoja na kukuza udugu na urafiki miongoni mwa wanajumuia na wanajamii.

“Kazi yangu leo ni kuwashukuru kwa kunialika kwenye nafasi yangu kama mzee wa Tanzania. Nakuombeeni dua shughuli zenuzote zifanikiwe kama ilivyokusudiwa,”alisema.

Aidha, alisema ni jambo jema kuwakutanisha waumini kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Msumbiji, Uganda, Burundi, Malawi na Uingereza jambo ambalo litaongeza chachu ya usambazaji elimu ya kuhubiri amani.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, aliipongeza jumuia hiyo kwa kuandaa mkutano huo kwa kuwa umewaunganisha na kudumisha amani.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu aliyealikwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mkutano huo, Masauni alisema ni vyema taasisi za dini kuhubiri amani na kujiweka kando na itikadi za kisiasa.

“Viongozi wa dini wanatakiwa kuhubiri amani na kutojiingiza katika masuala ya kisiasa badala yake muendelee kuitii serikali inayokuwa madarakani,”alisema.

Aliipongeza Ahmadiyya kwa kuwa kuhubiri amani na kutoa mafundisho mazuri ambayo ni msingi wa dini ya Kiislamu na upendo kwa wote.

Kwa upande wake Kiongozi Mkuu wa Ahmadiyya Tanzania, Sheikh Tahir Chaudhry, aliwashukuru viongozi wa serikali kuhudhuria mkutano na kuahidi kuendelea kuhubiri amani na kutojihusisha na siasa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.