JPM amteua Profesa Tibaijuka kuhudhuria mkutano wa UN

MZALENDO - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

RAIS Dk. John Magufuli, amemteua Profesa Anna Tibaijuka (Muleba Kusini - CCM) kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa unaohusu makazi na maendeleo endelevu.

Profesa Tibaijuka aliwahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, katika serikali ya awamu ya nne.

Mkutano huo unatarajiwa kuanza Oktoba 17 hadi Oktoba 20, mwaka huu, nchini Ecuador.

Taarifa za uhakika ambazo MZALENDO inazo zilisema Profesa Tibaijuka ataongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Yamungu Kayandabila.

Profesa Tibaijuka aliwahi kufanya kazi Umoja wa Mataifa akiwa Katibu Mkuu Msaidizi Mwandamizi wa umoja huo kwa kipindi cha miaka 12.

Septemba 24, mwaka huu, Profesa Tibaijuka alishinda tuzo ya kimataifa nchini Marekani inayojulikana kama ëHis Royal Highness Prince Khalifa bin Salman Al Khalifa Award for Sustainable Developmentí.

Tuzo hiyo ililenga kutambua mchango wa Profesa Tibaijuka katika kuhamasisha maendeleo duniani na na hutolewa kila baada ya miaka miwili.

Profesa Tibaijuka alikabidhiwa tuzo hiyo nchini Marekani katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya UN, New York.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali duniani ambapo Tanzania iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Lupembe.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.