Sh. bilioni 3 kudhibiti Pangani isimezwe na maji ya bahari

MZALENDO - - HABARI - LISA SAID, PANGANI

SHILINGI bilioni tatu zinatarajia kutumika kwenye mradi mkubwa wa kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi ambao utawezesha kuuhifadhi mji wa Pangani usimezwe na maji ya bahari.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, January Makamba, wakati wa ziara ya kukagua eneo litakalojengwa ukuta wa Mto Pangani ambalo limeathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi.

Alisema mji wa Pangani unakabiliwa na changamoto ya kipekee kwa sababu dalili zinaonyesha kuwa mji huo unakwenda chini ya kina cha bahari.

January alisema kadri muda unavyokwenda bahari inazidi kujaa mjini na hata makazi ya mkuu wa wilaya yapo hatarini kupotea na maji ya chumvi yanaingia katika Mto Pangani kwa kasi na kuathiri shughuli za uvuvi.

Alisema mradi huo unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na ulibuniwa mwaka 2009, lakini haukuweza kuanza kutokana na mabishano juu ya fedha zilizotoka kutotosha.

Hata hivyo, alisema mwaka huu serikali imetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na zabuni zilikwishatangazwa na makandarasi wamepeleka zabuni zao.

January alisema wazabuni watano wamepatikana na katika siku mbili zijazo zitafunguliwa na hatimaye mradi uanze kujengwa ili kunusuru mji wa Pangani.

Alisema kabla ya mwisho wa mwaka, jiwe la msingi la mradi huo litawekwa.

Waziri huyo alisema mradi huo utasaidia kuhifadhi na kuulinda mji wa Pangani usimezwe kabisa na kusababisha athari katika shughuli za wakazi wa mji huo.

Alisema uharibifu huo umesabisha athari nyingi ikiwemo shughuli za uvuvi, makazi ya watu na shughuli za kilimo katika mji huo.

January ambaye pia ni mbunge wa Bumbuli, alisema uvuvi haramu wa ulipuaji mabomu ni moja ya changamoto ambayo inaukabili mji huo kwa kuwa matumbatu yanayokinga ukali wa mawimbi yanaharibika na maji yanakuja kwa kasi kubwa.

Alisema kuna kisiwa kinachoitwa Maziwe kimedidimia na wakati hakionekani kabisa kwa sababu ya kina cha bahari kupanda kutokana barafu kuyeyuka huko katika mabara ya Arctic na Antarctica.

Hata hivyo, alisema mradi huo hautafika maeneo yote kwa sababu wakati mradi unabuniwa maeneo mengine yalikuwa na nafuu, lakini kwa sasa nayo yameharibika hivyo watafanya upembuzi yakinifu ili kujua gharama za mradi huo ili waweze kutafuta fedha za ziada .

Mkurugenzi wa Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Richard Muyungi, alisema mradi huo ambao wanaupa kipaumbele, utakuwa wa mwaka mmoja.

Muyungi alisema kuwa mradi huo unafadhiliwa na UNOPS kwa kushirikiana na UNEP kutoka Narobi nchini Kenya.

Mbunge wa Pangani Mkoani Tanga, Jumaa Aweso, alisema kuanza kwa mradi huo kutawasaidia kuondokana na athari hiyo ambayo ilikuwa inahatarisha uhai wa wakazi wa Pangani.

Pia, alisema pamoja na utekelezaji wa mradi huo amemwomba Waziri ifanyike tathmini ya eneo la Pangadeco kunusuru eneo hilo na shughuli za wakazi wa Pangani.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.