DC wa Karagwe aagiza SACCOS kupewa kiwanja

MZALENDO - - HABARI - NA ANGELA SEBASTIAN, BUKOBA

SERIKALI wilayani Karagwe mkoani Kagera imeagiza halmashauri ya wilaya hiyo kuwapatia kiwanja walichoomba wanawake wa Kikundi cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (KAWISA Ltd) kwa ajili ya kujenga hoteli ili kufanya uzalishaji na kuondokana na umaskini.

Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Godfrey Mheruka, wakati akiongea na wanawake zaidi ya 600 kutoka Wilaya za Kyerwa na Karagwe waliohudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya kuzaliwa kwa kikundi cha KAWOSA.

Mheruka alisema amepata taarifa kutoka kwa Kaimu Mrajisi wa vyama vya ushirika nchini Dk. Audax Rutabanzibwa kuwa wanawake hao waliomba kiwanja hicho mwaka 2008 kwa halmashauri ya wilaya hiyo ili wajenge hoteli ambayo itatoa ajira, lakini licha ya kufuatilia kwa kipindi kirefu hawajapewa majibu ya kuridhisha.

“Hivi mtu anaomba kiwanja awekeze katika mambo yatakayo pandisha uchumi na kuleta maendeleo ya wilaya yetu na taifa kwa ujumla unamnyima, maendeleo yanaonekana wewe unataka kuyadidimiza, katika serikali ya awamu ya tano mambo hayo ya ukiritimba hayana nafasi tena.”

“Naagiza uongozi wa Halmashauri ya Karagwe ndani ya wiki moja utaratibu wa kuwapatia kina mama hawa kiwanja hicho uwe umekamilika wapewe,î alisisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa KAWIOSA, Saphina Amran, alisema kikundi hicho kilianzishwa mwaka 2006 ili kuwezesha wananchi kusaidia kiuchumi.

Alisema kilianza kikiwa na wanachma 70 ambapo kwa sasa kina wanachama 2,852 na kutoa mkopo wa sh. milioni 164 ambapo mpaka sasa wametoa mikopo ya sh. bilioni 16.

Kwa upande wake, Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini Dk. Rutabanzibwa, alisema kitendo cha Mkuu wa Wilaya ya Karagwe kuagiza halmashauri kuwapatia wanawake hao kiwanja hicho kimeonyesha kuwa serikali inajali wananchi wake ikiwemo kuendeleza ushirika.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.