Yanga kuivaa Mtibwa Sugar Uhuru

MZALENDO - - MICHEZO - NA VICTOR MKUMBO

KLABU ya Yanga imesema kuwa itatumia uwanja wa Uhuru kama uwanja wao wa nyumbani kucheza na Mtibwa Sugar.

Yanga na Mtibwa Sugar zinatarajiwa kuvaana katikati ya wiki ijayo kwenye uwanja huo baada ya kuzuiliwa kuutumia Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kutokana na vurugu.

Timu za Yanga na Simba zilizuiliwa na Serikali kuendelea kuutumia Uwanja wa Taifa kutokana na mashabiki wake kufanya fujo kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Oktoba Mosi mwaka huu.

Kwenye mchezo huo mashabiki wa Simba walifanya vufugu na kung’oa viti wakidai kutoridhishwa na uchezeshaji wa mwamuzi Martin Saanya kwenye mchezo huo wakati wa Yanga walifanya uharibifu wa mageti.

Hata hivyo Serikali iliamua kuzifungia timu hizo kutumia uwanja wa Taifa kama uwanja wao wa nyumbani na kuziamuru kutafuta viwanja vingine.

Yanga awali waliandika barua kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Shirikisho la Soka Visiwani Zanzibar kuomba uwanja wa Amaan, lakini juhudi zao ziligonga mwamba kutokana na kuwa kanuni na sheria za soka kusema kuwa timu hizo zinatakiwa kutafuta viwanja vingine vilivyopo Bara.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, alisema kuwa wanatarajia kuutumia uwanja wa Uhuru kwenye mechi zao kwani huo hawakufungiwa.

Alisema kuwa uwanja waliofungiwa na Serikali ni ule wa Taifa hivyo walikuwa wana nafasi ya kuchagua uwanja mwingine ili kuutumia kama uwanja wao wa nyumbani.

Alisema kuwa maandalizi kwa ajili ya mchezo wao na Mtibwa yanaendelea vizuri na hivyo wana imani ya kuutumia uwanja huo baada ya kuiandikia barua Wizara na Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

“Tumeshaandika barua Wizara ya Michezo na pia Bodi ya Ligi kuwapa taarifa kuwa tutautumia uwanja wa Uhuru baada ya kufungiwa uwanja wa Taifa, hivyo tutacheza mchezo wetu na Mtibwa Dar es Salaam kwani tumefungiwa kucheza Taifa na sio kwingine,” alisema.

Alisema kuwa wanatarajia kuendelea kuutumia uwanja wa Uhuru hadi hapo Serikali itakapoamuru warejee kwenye uwanja wa Taifa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.