JPM: Mianya fedha za safari nje idhibitiwe

Ataka watumishi wasio na kazi ubalozini kurejeshwa

MZALENDO - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

RAIS Dk. John Magufuli, ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kudhibiti mianya yote ya matumizi mabaya ya fedha za umma ambazo zimekuwa zikitumika katika safari za nje ya nchi na matumizi mengine yasiyo ya lazima.

Aidha, ameitaka kuhakikisha watumishi wote ambao wapo katika ofisi za ubalozi bila sababu za msingi wanarejeshwa nchini ili kupunguza mzigo wa gharama kwa serikali.

Rais Dk. Magufuli aliyasema hayo alipokutana na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani ambapo aliwataka utekelezaji wa diplomasia ya uchumi utiliwe mkazo katika uwekezaji kwenye sekta ya viwanda.

Katika mkutano huo uliofanyika juzi Ikulu, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Dk. Magufuli alisema serikali imeweka dhamira ya kukuza sekta ya viwanda kutoka ukuaji wa asilimia 7.3 hadi kufikia asilimia 15 ifikapo 2021 na kuzalisha ajira kwa asilimia 40.

“Sasa nimeona niwaite mabalozi ili tuelewane, mjue mwelekeo tunaoutaka na mjue ni namna gani mtakavyoshiriki kuhamasisha uwekezaji wa viwanda,” alisema Rais Magufuli.

Aliongeza kuwa: “Nataka badala ya kubaki mmejifungia ofisini, mtoke mwende mkawatafute wawekezaji wawekeze katika viwanda ili nchi yetu inufaike kwa watu kupata ajira, serikali kukusanya kodi na tuinue maendeleo yetu.”

Maeneo mengine ambayo Rais Dk. Magufuli aliwataka mabalozi wayafanyie kazi ni kutangaza na kuwavutia watalii kuja nchini, kufanyia kazi fursa zote zenye manufaa kwa Tanzania katika nchi wanakowakilisha, kulinda mali za nchi zilizopo katika nchi hizo na kufuatilia utekelezaji wa mikataba ya biashara na uwekezaji inayofanywa kati ya Tanzania na nchi wanazowakilisha.

Pia, Rais Dk. Magufuli aliwataka mabalozi kufanya kazi kwa juhudi, kuondoa kasoro za utendaji ambazo zimekuwa zikilalamikiwa katika ofisi zao na kubana matumizi ya fedha yasiyokuwa ya lazima.

“Kuna wafanyakazi wapo kwenye balozi zetu wakati hata sifa za kuwa katika nafasi wanazoshikilia hawana, ilifika mahali mtu akiharibu hapa nyumbani anapangiwa ubalozini,” alisema.

“Wakati mwingine unakuta ubalozi wa Tanzania kwenye nchi fulani una idadi kubwa ya wafanyakazi kuliko mahitaji ya ubalozi huo, haiwezekani” alisisitiza Rais Magufuli.

Hata hivyo, aliwapongeza mabalozi hao kwa kazi wanazozifanya kwenye nchi wanazowakilisha na aliwahakikishia kuwa serikali ina matumaini nao na inawategemea kuwa wataendelea kuiwakilisha na kuitangaza vizuri nchi.

Mkutano huo pia ulihuduriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa taasisi mbalimbali na wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

RAIS Dk.John Magufuli, akisalimiana na Kiongozi wa Jumuia ya Mabohora Duniani, Dk. Seydna Mufaddal Saifuddin, alipowasili Msikiti wa Bohora, Upanga, Dar es Salaam, jana ambako alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za kuadhimisha Mwaka Mpya wa Kiislamu wa 1438. Habari Uk. 3, Picha zaidi Uk. 4. (Picha na Ikulu).

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, akikata utepe, kuzindua katiba ya Jumuia ya Wanawake Wafanyabiashara Kariakoo (JUWABIKA), Dar es Salaam, jana. Kutoka kushoto ni Katibu wa jumuia hiyo, Zaituni Juma, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk.Hamisi Kigwangala, mke wa Rais Mstaafu, Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete na Mwenyekiti wa jumuia hiyo, Mwanamvua Kinanda. (Picha na Christopher Lissa).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.