Mgogoro CUF kutinga kwa viongozi wa dini

MZALENDO - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

MGOGORO wa Mwenyekiti wa Civic United Front (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu wake, Seif Shariff Hamad huenda ukapelekwa kwa viongozi wa dini iwapo Bodi ya Wadhamini wa chama hicho itashindwa kuutatua.

Kauli hiyo imekuja baada ya baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini kwenda mahakamani kwa ajili ya kumshtaki Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mtungi kutokana na madai ya kuingilia mambo ya vyama vya siasa kikiwemo CUF.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi wa CUF, Thomas Malima, alisema anatarajia kuitisha kikao cha Bodi ya Wadhamini kwa ajili ya kuwaita Profesa Lipumba na Maalim Seif ili waweze kuwasikiliza.

Alisema iwapo viongozi hao watakataa kwenda kusikilizwa na Bodi, watalipeleka suala hilo kwa viongozi wa dini.

“Ikiwa watakataa jambo hili tutalipeleka kwa viongozi wa dini... tunaamini kwa kuwa Maalim Seif ni Muislamu mzuri, na anaenda msikitini, hivyo hivyo kwa Profesa Lipumba wana viongozi wa dini ambao wanawaheshimu... basi tutawapa jukumu viongozi hao wa ili waweze kuwaita na kuwasikiliza,”alisema.

Alisema wanaamini wakiitwa na viongozi wa dini kila mmoja atatoa dukuduku lake na mwisho watasameheana.

“Hatuoni kama kuna jambo zito sana katika mgogoro huu, bali tunajua kuna vyanzo vinashiriki kwa nguvu zote kuhakikisha CUF inashuka,” alisema.

Alisema anaamini bodi ya wadhamini ndiyo iliyobaki ambayo inaweza kuwakutanisha viongozi hao na sio vinginevyo.

“Mimi kama katibu wa bodi nitafanya jitihada, ikishindikana nitalikabidhi kwa viongozi wa dini na ninaamini watalimaliza,” alisema.

Kuhusu baadhi ya wajumbe wa bodi kwenda mahakamani, alisema akiwa kama katibu wa bodi, haungi mkono suala la wenzake kwenda mahakamani.

“Nitakachokifanya ni kuchukua mahudhurio ya bodi ya Tanzania Bara na ya Zanzibar na ajenda zetu na kuzipeleka mahakamani, kuomba jalada la kesi iliyofunguliwa lifutwe kwa sababu bodi imegawanyika,” alisema,

“Lazima tufanye suluhu kwa sababu kwenda mahakamani hakutatusaidia,” alisema Malima.

Hata hivyo, Malima alieleza kusikitishwa na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini kuchukua jukumu la kuitisha kikao cha wajumbe wakati hawana uhalali wa kufanya hivyo.

“Kwa mujibu wa katiba ya chama chetu na kanuni ya fedha Mkurugenzi wa Fedha, ndiyo Katibu wa Bodi ya wadhamini na mimi (Malima) ndiyo mkurugenzi wa fedha. Hatutambui kama kuna kikao cha bodi kilichofanya maamuzi ya kumpeleka msajili mahakamani, “alifafanua Malima.

Alisema wanachotambua ni kwamba kuna kikao kilifanyika Zanzibar ambacho kiliitishwa na aliyekuwa Katibu wa Bodi hiyo, Joram Bashange ambaye kwa sasa hana nyadhifa hiyo na kilihudhuriwa na wajumbe watatu tu.

“Kwa mujibu wa katiba yetu ibara ya 98, Bodi ya Wadhamini ina wajumbe tisa, kati ya hao watano wanatoka Tanzania Bara na wanne wanatoka Zanzibar,”alisema.

Wakati huo huo, CUF inatarajia kuwafungulia mashtaka wanaolitumia jina la chama hicho vibaya.

“Sisi (CUF) tunafungua kesi polisi kwanza, halafu polisi watafanya utaratibu wa kupeleka kwa DPP ili ipelekwe mahakamani ikiwa itaonekana ni kesi ya msingi,” alisema.

Alisema wamefungua kesi kwa baadhi ya watu ambao ni Julius Mtatiro (Kaimu Mwenyekiti) Maharagande Mbarala (Mkurugenzi wa Habari na Uenezi) Joram Bashange (aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi).

Alisema hao wanalitumia jina la CUF vibaya huku wakizungumza na vyombo vya habari na kujitambulisha kuwa wao ndiyo viongozi wa CUF.

Profesa Ibrahim Lipumba

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.