Mnyika katika kashfa

MZALENDO - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

NAIBU Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika ,ameingia katika kashfa baada ya kumuingiza mkenge aliyekuwa Ofisa Habari na Uenezi wa chama hicho, Erasto Tumbo kuhusu nyumba yake iliyoko Bunju, Dar es Salaam.

Taarifa za kuaminika ambazo gazeti hili limezipata ikiwemo nyaraka za mkopo wa sh. milioni 300 kwenye Benki ya Stardard Chartered na dhamana ya mkopo huo kuwa nyumba mbili ikiwemo ya Tumbo.

Nyaraka hizo zilionyesha moja ya nyumba hizo ni ya Tumbo

ambayo ipo kwenye kiwanja namba 34, kitalu 2 katika eneo hilo na ambayo inaonyesha ilikuwa na thamani ya sh. milioni 140.

Hata hivyo, Mnyika alikana kuchukua mkopo huo au kutumia nyumba hizo kwa madai kuwa alishajiuzulu ukurugenzi wa Kampuni ya TESTA LIMITED, ambayo ilichukua mkopo kwenye benki hiyo.

“Waulize hao wanaosema nimewadhulumu nyumba zao na kwenda kuwakopea na waulize ni nani aliyewaambia watoe hati zao ni mimi kweli,’’alisema.

Taarifa zaidi zilisema wakati mkopo huo ukichukuliwa, Mnyika ndiye alikuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi na mtu mwenye mamlaka makubwa kwenye kampuni hiyo ikiwemo kutia saini uchukuaji wa fedha.

Vielelezo vinaonyesha Mnyika ambaye ni mbunge wa Kibamba kupitia CHADEMA, alianza kutumia mbinu kuhakikisha anakwepa lawama za kulipa fedha hizo na kuwaachia mzigo Tumbo na mwenzake Charles Tumaini.

Taarifa zilisema Mnyika na wenzake waliomba mkopo huo kwa ajili ya kufanyia biashara na kwamba akiwa Mwenyekiti wa Bodi alitoa dhamana ya hadhi yake ya sh. milioni 300, sambamba na Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Lazaro Mtani aliyetoa pia dhamana kama hiyo.

Ilielezwa kuwa hati hizo zilitiwa saini na Mnyika, Mtani mbele ya mwanasheria wa kampuni hiyo, Thomas Brash, Mei 11, mwaka 2012 na nyaraka hizo ziliwasilishwa benki kwa ajili ya kujipatia mkopo huo uliotoka Septemba 14, 2012 na kuanza marejesho ya kila mwezi.

Mkopo huo ulipaswa kuwa wa miezi 48 na kila mwezi kampuni hiyo ilitakiwa kurejesha sh. milioni tisa, ambapo hadi kufikia Julai, mwaka huu, walianza kushindwa kulipa malipo hayo ambapo ilikuwa wanadaiwa sh. milioni 222 na Mnyika alikuwa bado ndiye mwenyekiti wa bodi hiyo.

“Tunamshaanga leo anajitoa kwenye suala hili, yeye ndiye alitushawishi tumpe hati zetu ili akopee na tusiwe na shaka kwa vile ni mbunge. Sasa ameshindwa kulipa anasema si mhusika.”

“Anajidanganya, atalipa deni na kutupa hati zetu kwa kuwa ukikopa fedha benki na wewe ukiwa mwenyekiti wa bodi na ukatia saini, benki itakuhesabu kama wewe ndiye mkopaji na una wajibu wa kulipa deni hilo,’’ alisema mmoja wa wahusika wanaomdai hati Mnyika.

Aliongeza kuwa: ‘’Kitendo cha Mnyika kuweka dhamana binafsi anajikanganya zaidi, dhamana hiyo inamuhitaji kurejesha deni hilo katika hali yoyote ya kipato chake hata kama amefilisika.’’

Hata hivyo, gazeti hili lilielezwa kuwa kampuni hiyo ya Mnyika inadaiwa fedha nyingi zaidi ya sh. bilioni moja na benki mbalimbali nchini, ambapo baadhi ya mali zilizowekwa kama dhamana zinaanza kupigwa mnada.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.