JP yaingia mkataba na Star African kusafirisha mizigo

MZALENDO - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya JP Logistics imeingia mkataba na Kampuni ya Star African Freight Forwading LLC (Lake Oil Group, SAFF) wa kusafirisha mizigo katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mkataba wa makubaliano wa kampuni hizo, ulitiwa saini juzi Dubai kati ya Mkurugenzi wa JP, Jack Pemba na Mkurugenzi wa Star African Freight Forwading LLC (SAFF), Samir Al-Akrabi mbele ya baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa Dubai na washirika wao.

Tukio hilo, pia lilishuhudiwa na wafanyakazi wa SAFF Dubai na wafanyakazi wa JP Logistics Tawi la Dubai.

Akizungumza mara ya kutia saini, Pemba alisema mkataba huo utawezesha kampuni hizo kutoa huduma mbalimbali ikiwemo ya kusafirisha mizigo kutoka sehemu moja kwenda nyingine katika nchi husika zilizoanishwa.

Pemba alisema kwa pamoja kampuni hizo zitakuwa na jukumu la kutoa huduma na kusafirisha mizigo ya wateja wao kutoka nchi mbalimbali duniani kwenda Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na nchi nyingine za Afrika ya Kati.

Mkurugenzi huyo alisema kampuni yake itatoa huduma hiyo kwa gharama nafuu ili kuwawezesha wateja wao kumudu gharama na kupata mizigo yao kwa wakati.

Alisema kampuni ya SAFF na JP Logistics zitatoa huduma zake kwa kusafirisha mizigo kwa kutumia usafiri wa meli, ndege za kukodi, ndege za mizigo, vifurushi na maghala ya kuhifadhi bidhaa.

Pemba aliongeza kuwa kampuni hizo zitatoa nafasi ya kujenga mafanikio ya uboreshwaji wa ufanyaji wa biashara kwa haraka na mafanikio kwa nchi husika.

“Kampuni hizi ni mkombozi kwa wafanyabiashara na watu ambao watazitumia katika kuharakisha kutoa au kuagiza mizigo yao na kupatikana kwa haraka zaidi kwa kutumia teknolojia za hali ya juu,” alisema Pemba.

MKURUGENZI wa Kampuni ya JP Logistics, Jack Pemba (kushoto) akitia saini mkataba wa kusafirisha mizigo katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na Kampuni ya Star African Freight Forwading LLC (Lake Oil Group, SAFF). Kulia ni Mkurugenzi wa Star African Freight Forwading LLC, Samir Al-Akrabi. (Picha na Mpiga Picha Wetu)

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.