UVCCM: Tunataka vitendo zaidi kuliko maneno

MZALENDO - - HABARI - NA MWANDISHI WETU, SIMIYU

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema zama za viongozi wa kutoa ahadi zisizotekelezeka zinapaswa kufika tamati badala yake kuwepo maneno machache na vitendo vingi vyenye tija na manufaa kwa taifa.

Umesema kaulimbiu ya hapa kazi tu isitumike kupiga porojo, mzaha au kuchangamsha mikutano badala yake itumike kutekeleza mambo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya kweli.

Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alitoa kauli hiyo alipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka ofisini kwake Bariadi, mkoani hapa.

Shaka alimueleza mkuu huyo wa mkoa kuwa ipo haja kwa wakuu wa mikoa mingine kuiga mfano wa utekelezaji kwa vitendo unaofanywa na Simiyu kwa kuhimiza maendeleo na kuonyesha njia ya utekelezaji.

“Inafurahisha kuona mkoa wa mmeamua kusema na kutenda kwa vitendo, Wilaya ya Maswa imeanza kuwa na viwanda vidogo vya maziwa na utengenezaji chaki, wananchi wanahitaji kuona vitendo badala ya maneno mengi,”alisema Shaka.

Alisema ni wajibu na haki ya kila mkuu wa wilaya au mkoa kwa kushirikiana na watendaji, wataalam na wananchi kutimiza majukumu yao na kuvutia wawekezaji makini kuwekeza katika viwanda na sekta zingine za kimaendeleo sanjari na utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Aidha, alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mtaka kwa kutekeleza kwa vitendo mikakati na mipango ya utekelezaji wa sera za serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kutoa fursa ya ajira kwa vijana.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mtaka, alimueleza Kaimu Katibu Mkuu Shaka kwamba serikaili mkoani mwake imejipanga kuleta mabadilko kwa kuwa na viwanda vidogo na vya kati ambapo wameanza na kiwanda cha maziwa wilayani Meatu na kiwanda cha chaki kilichopo Bariadi.

Alisema kwa kutumia mazingira bora ya ardhi ya Tanzania nchi inaweza kupiga hatua kupitia sekta za kilimo kwa kuweka mkazo katika ufugaji wa kisasa wa samaki na usindikaji mazao ili kuyaongezea thamani mazao ya kilimo.

“Tumeandaa mpango mkakati ambao naamini utawavutia na kuwashawishi wawekezaji wengi kuja na kuwekeza Simiyu. Tunaendelea kuwahamasisha waje kwa wingi na kuchangamkia fursa zilizopo za kiuchumi ili kutongezea ajira kwa vijana na maendeleo ya jamii,”alisema.

MKUU wa Kituo cha Polisi cha Mlandizi Silvester Njau, akipkea msaada wa mifuko ya saruji kutoka kwa mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Mlandizi-Dar es Salaam ,Richard Milinga uliotolewa na madareva hao kusaidia ujenzi wa nyumba za askari Polisi, Mlandizi mkoani Pwani. (Picha na Mwamvua Mwinyi).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.