Mangula uko sahihi, huu ni wakati wa kukisafisha Chama

MZALENDO - - HABARI -

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula ametoa tamko kuwa Chama kamwe hakitasita kukata majina ya wagombea wote ambao wanazunguka na kuwashawishi wanachama kwa ajili ya uchaguzi wa CCM mwakani.

Aidha, amesema Chama hakitakubali kuona watu wakitoa fedha kwa ajili ya kununua uongozi na kwamba umefika wakati mpigakura asinunulike kama bidhaa sokoni kwa sababu kitendo hicho ni kujidhalilisha.

Kauli hiyo ya Mangula, imeanza kutoa taswira pana kuwa Chama kimejizatiti katika kuijenga CCM ili kiendelee kuwa Chama bora na chenye uwezo mkubwa wa kumtetea mwananchi mnyonge, ambaye kwa zaidi ya miongo minne wamekuwa wakikithamini na kukiamini Chama Cha Mapinduzi.

Ni wakati wa Kamati za Maadili za Chama kuanzia wilaya hadi mkoa, kuunga mkono tamko hilo la Mangula ili kusaidia kupatikana kwa viongozi bora na wenye uwezo wa kufanya mambo bora kwa maslahi ya CCM na taifa kwa ujumla.

Tunaamini kuwa kulikuwepo na malalamiko kutoka kwa watu wengi, waliokuwa wakilalamika kuhusiana na mchezo mchafu uliokuwa ukifanyika hususan uchaguzi wa ndani wa Chama unapokaribia kwa watu kupanga viongozi wao kwa maslahi yao binafsi na si vinginevyo.

Huu ni wakati wa kuhakikisha kila kiongozi ndani ya Chama anapatikana kwa kuzingatia kanuni na maadili ili kuondokana na mifumo mibaya ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka, ambapo huaminika kwamba ukiwa Mwenyekiti wa CCM wa wilaya au Mkoa ni fursa nzuri ya kujitengenezea mazingira serikalini.

Haya ni makosa makubwa katika jamii kununua uongozi kama bidhaa sokoni, hivyo ni wakati wa kutoa nafasi kwa wapiga kura waamue na wasikubali kununuliwa kama bidhaa kwa kuwa kuruhusu hilo ni kujidhalilisha jambo ambalo halipaswi kupewa nafasi.

Uchaguzi ujao wa CCM, uwe wa mfano kwa kila mwana-CCM mwenye sifa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali kuanzia Ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM na nafasi nyingine kwa kushinda kwa hoja na si uwezo wa kifedha.

Chama kwa muda mrefu kimekosa kupata viongozi waadilifu kutokana na uwepo wa ghiliba nyingi za wagombea wanaotumia fedha kwa maslahi yao binafsi ili mradi watimize majukumu wanayoyalenga.

Watu wa aina hiyo ni wabaya na safari hii, hawapaswi kupewa nafasi za kuwania uongozi na ndio maana tunaamini kauli ya Mangula itachukuliwa kuwa mwingozo kwa Kamati za Maadili za CCM za wilaya na mkoa kukata majina ya watu wanaokwenda kinyume na utaratibu.

Umefika wakati kufuta dhana inayoendelea kuaminishwa katika jamii kuwa kiongozi mzuri ni yule anayetoa fedha jambo ambalo si kweli. Ni wakati wa kuungana na Mangula hasa kwa wana-CCM kuwakataa wanaotumia fedha kupata uongozi ndani ya Chama.

Shime kwa kila mwana-CCM kutembea kifua mbele kwa kuwa Chama kimeshatoa mwongozo kwamba watoa rushwa na wanunua uongozi safari hii, hawana nafasi ya kupewa madaraka ndani ya Chama.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.