MKE WANGU

MZALENDO - - MATANGAZO - NA EMMANUEL MOHAMED

KARIBU tena msomaji wa safu hii kwa mara nyingine,jina la kitabu kinachohakikiwa ni hadithi ya “MKE WANGU” kimetungwa na Muhammed Said Abdalla.

Mchapishaji wa kitabu hiki,Dar es salaam University Press (DUP) na kimepewa namba katika sekwensia ya vitabu duniani(ISB): 9987371624 kitabu kina kurasa 57 na kimechapwa mwaka 1999.

Hadithi hii imeweka msisitizo katika tabia za mke wa msimulizi, hali inayotiliwa mkazo na ukweli kwamba msimulizi mwenyewe hatajwi kwa jina.

Kutokana na umuhimu wake mkubwa, mke wa msimulizi anatajwa kuwa ni Aziza.

Wanawake wengine ambao msimulizi alichaguliwa kuwaoa ni Salma Fadhil, Fedhele Salim na Seluwa na kitu anachokithamini Aziza ni kipimo cha utu.

Uhusiano baina ya msimulizi na mkewe unapewa kipaumbele katika hadithi hii.

Hadithi inaeleza jinsi msimulizi alivyopata mke miongoni mwa wanawake aliopendekezewa kuwaoa, walivyoanza safari ya maisha ya ndoa.

Mgogoro uliotamalaki uhusiano wao na hatimaye jinsi mke alivyoomba talaka baada ya kuona kwamba haelewani na mumewe katika kila jambo.

Mwandishi anatumia kalamu yake katika hadithi hii kukashifu mfumo wa utabaka kati ya wasionacho na walionacho ambao hutegemea kuvuna nafuu kutokana na jasho la wasionacho.

Katika kitabu hicho, mwandishi anaendelea kuonyesha mtazamo wake kuwa wanajamii wanapaswa kutambua mke ndiye anayestahili kuelekezwa na kufunzwa ustaarabu na mwanamume ambaye ametawaliwa na ubabe dume (taasubi za kiume).

Msimamo wa mwandishi wa hadithi hii ni kwamba, ushirikiano baina ya wanandoa ndio msingi unaojenga familia imara.

Hadithi hii inaonyesha kuwa dhana ya utabaka bado ipo ndani ya jamii yetu ambapo hali inayojitokeza kuwa walionacho wanaishi kwa jasho la makabwela ambao daima hufanya kazi za sulubu na shokoa.

Kuna kazi za watu wa daraja la chini na zile za makabaila walio katika daraja la juu. Kazi zinazochukuliwa kuwa duni ni pamoja na kilimo, kuchoma mihogo, kuchunga punda na kuuza nazi.

Mtunzi anahoji kwamba ni aibu kwake kufanya kazi za watu duni. Anasema, ìLo! Ati mimi nichome mihogo niuze! Si nitaonekana nina wazimu mie?... kila mtu na kazi yakeî (ukurasa tano).

Anaendelea kusema kuwa kazi za hadhi kubwa ambazo zinastahiwa na matajiri ni zile za kuajiriwa ofisini. Maskini huishi mashambani au hulazimika kwenda mijini kufanya utwana na ujakazi katika nyumba za matajiri.

Hadithi hii inaonyesha jinsi watu wanaoishi katika maeneo ya mijini wanachukuliwa kuwa wajuaji na waliostaarabika kinyume na wale wanaoishi mashambani au vijijini.

Dhana ya kustaarabika kwa mujibu wa mtunzi wa hadithi hii ni kufuata mambo ya kisasa kama vile kupiga mswaki na kuvaa viatu, mambo ambayo watu wa mashambani hawana mazoea nayo.

Mtunzi anamtumia mhusika Aziza kwa kuonyesha kuwa anakataa kutumia brashi kwa kudai kwamba ni manyoya ya nguruwe.

Anasema kwamba hataki kuvaa viatu kwa kuwa vimetengenezwa kwa ngozi ya mnyama asiyemjua.

Hadithi hii inajikita katika mgogoro dhidi ya Aziza na mumewe ambapo Aziza anapingana na mumewe kwenye suala la ubaguzi wa kitabaka.

Moja ya mzozo huo ni pale anapoona inapojitokeza hali ya kabwela kutoruhusiwa kuingia nyumbani kwa kabaila.

Jambo hili lilimfanya mtunzi asitake muuza madafu ambaye ni mchochole, kuingia nyumbani kwao - nyumbani mwa tajiri.

Lakini Aziza alimruhusu kuingia, auze madafu na kujipatia riziki yake halali. Aziza aliamini kwamba binadamu wote ni sawa na thamani ya utu ni kazi hata kama umetoka katika familia yenye utajiri mkubwa.

Anasema, ìNimemwita bwana huyu aje huku juu kusudi mmuoneÖhuyu ni binadamu kamili, kwani ni mkulima, tena ni mfanyakaziî (ukurasa wa tisa).

Baadaye Aziza anautambua ‘ugumegumeí wa msimulizi na kuamua kuomba talaka. Mwandishi anaonyesha umuhimu wa kazi katika maisha ya binadamu.

Anahoji kwamba hata kama mtu ametoka katika familia ya kitajiri iliyo na kila kitu, kuna hasara atakazozipata ikiwa atakosa kufanya kazi.

Anamchora msimulizi kama mmoja wa watu walioathirika pakubwa kwa kutofanya kazi.

Ingawa msimulizi ana uwezo wa kupata chochote anachokitaka kutoka kwa wazazi wake, anamkosa mkewe Aziza ambaye hataki kuishi na mume asiyefanya kazi na badala yake kuishi kwa jasho la wengine.

Aziza alimuasa mumewe kuhusu umuhimu wa kazi, kila mara akimkosoa kwamba si lazima afanye kazi ya kuajiriwa ofisini.

Aziza alishazoea kufanya kazi na si kufanyiwa. Alimpinga mumewe aghalabu, akimweleza kuwa ni jukumu la mke pia kufanya shughuli zote za nyumbani na sio kufanyiwa na watumishi wa wazazi wao.

vilevile mtunzi anatuchorea jinsi jamii zinaendeleza ubaguzi dhidi ya wanawake.

Mwanamke anaonekana kuwa ndiye anayehitaji maongozi ya mwanamume na si kinyume chake. Hata hivyo, Aziza hakuwa kama alivyodhani msimulizi.

Wakati ambapo alidhani kwamba angemfundisha mkewe ustaarabu, Aziza ndiye ‘anamfundishaí mumewe.

Msimulizi anasema, ìMimi niliyetaka kumfunza msichana huyu maisha ya kistaarabu, leo hii yeye kanianzia hivi?î (ukurasa wa tano).

Pia mwandishi amefanikiwa kupambana na utamaduni na mila dhaifu ikiwemo jamii kulazimisha vijana kuoa na kuolewa pindi wanapofikisha umri wa ndoa.

Utamaduni unaunga mkono kitendo cha mume kuchaguliwa mke.Kijana wa kiume alioa mke aliyechaguliwa na wazazi wake.

Msimulizi anapendekezewa na mamaye kumuoa Fedhele, Salma na Seluwa ila anawakataa kwa hofu kwamba ni wa mjini na kwa hivyo ni wajuaji.

Alichelea kw amba wameharibika kimaadili na badala yake anamkubali Aziza ambaye amelelewa na kulia mashambani.

Mtunzi anamtumia mhusika Aziza akisema ìlazima awe mbichi na mfuto katika mambo mengi ya mjini yaliyokuwa sababu za kuharibu ndoa nyingi za wenzangu kwa muda mchache wa makazi yao,î (ukurasa wa pili).

Kwa upande wa fani mwandishi ametumia lugha rahisi yenye msisimuko na molali wa kuendelea kusoma kitabu hiki cha MKE WANGU ambapo ametumia vyema wahusika pamoja na taswira mbalimbali alizotaka kukusudia dhamira yake kwa jamii.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.