Shule za walemavu zijengwe nchini

MZALENDO - - MAKALA - NA MWANDISHI WETU

WATOTO wana haki ya kupata malezi bora kutoka kwa wazazi wao elimu na afya bora ili aweze kuishi katika msingi bora maisha.

Agripina ni msichana (27), anayeishi mkoani Morogoro, aliyekosa msingi mzuri wa maisha kwa sababu ya kukosa elimu kutokana na kuungua moto na baadhi ya viungo vyake vya mwili kuungua na kumsababishia ulemavu wa kudumu na kukosa elimu.

Msichana Agripina mpaka hivi sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa kifafa ambao umemsababishia kuungua moto kutokana na kuanguka kila wakati.

Mwaka 1996, Agripina alipokuwa na umri wa miaka mitano aliungua moto ambao mama yake alikuwa ameutayarisha kwa ajili ya kupika chakula cha jioni.

Agripina anasema wakati huo alipokuwa anateketea na moto alikuwa hana fahamu na mama yake alikwenda kisimani kuchota maji.

Agripina anasema aliungua na moto huo kwa dakika 15 mpaka mama yake aliporudi kisimani alikuta tayari ameshaungua vidole vyote vya mkono wa kulia na vidole vya mguu wa kushoto.

Agripina anasema baada ya hapo alilazwa hospitali takriban miezi mitano kwa ajili ya kuuguza majeraha aliyoyapata.

Hata alivyotoka hospitali alikuwa hawezi kufanya chochote kutokana na majeraha aliyokuwa nayo ambayo yalimsababishia ulemavu mpaka leo hii.

Anasema alipofika umri wa miaka saba alimuomba mama yake ampeleke shule, baada ya kuona wenzake wanakwenda shule, alipelekwa lakini walimu hawakumpokea kutokana na majeraha aliyokuwa nayo ambayo yalimsababishia kutotembea vizuri na alikuwa hana uwezo hata wa kushika kalamu kwa ajili ya kuandika.

Agripina anasema aliumia hasa akiwaona wenzake wanarudi kutoka shule na yeye akiwa yupo nyumbani amekaa bila ya kufanya shughuli yoyote.

Miaka ilienda Agripina akawa msichana mkubwa, lakini alikuwa hajui kusoma wala kuandika kutokana na kukosa elimu.

Anasema mpaka hivi sasa amekuwa ni mtu wa kuishi wa kutegemea misaada kutoka kwa ndugu zake.

Anasema anaishi maisha magumu kutokana na ulemavu aliokuwa nao .

Pia, anasema baadhi ya watu wanamnyanyapaa kutokana na hivyo alivyo.

Agripina anasema hata yeye hakupenda kuwa hivyo alipenda asome na kuwa familia yake na maisha mazuri kama wanavyoishi watu wengine.

Hata hivyo, Agripina anaiomba serikali kuanzisha shule za wanafunzi walemavu mikoani ili watoto walemavu wanaohitaji kusoma nao wapate elimu.

Anasema hivi sasa kuna watoto wengi wenye matatizo kama yeye, lakini wanakosa elimu kwa sababu ya uchache wa shule hizo hapa nchini.

Elimu ni ufunguo wa maisha hivyo hata mtoto mlemavu ana haki ya msingi ya kupata elimu ili hapo baadae aweze kumudu maisha yake.

Wapo baadhi ya wazazi na walezi wenye tabia ya kuficha watoto walemavu wakidai kuwa ni mkosi katika familia .

Wengine hudiriki hata kuwaua na watoto hao, hivyo hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao kwa wale wote wenye tabia ya kuwanyanyapaa watoto hao kwa kuwa nao wana haki yao ya msingi na kupata elimu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.