Waziri awataka ma-RC, ma-DC kwenda shuleni

MZALENDO - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) George Simbachawene, amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kupita madarasani kukagua kinachofundishwa na walimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu iliyokusudiwa.

Akizungumza na wakazi wa vijiji vya Wotta na Wangi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Waziri Simbachawene alisema viongozi hao wana jukumu la kufuatilia maendeleo ya wanafunzi ili baadaye waweze kutoa ushauri na si kuachia jukumu hilo kwa wakaguzi wa elimu peke yao.

Aidha, Waziri Simbachawene aliziagiza mamlaka za serikali za mitaa nchini hususani halmashauri, kuhakikishazinashirikiana kukagua miradi hususan inayohusu maendeleo ya elimu ili kuona kama inakidhi ubora kulingana na gharama iliyotolewa.

ìTushirikiane na wataalamu tupite na kukagua hata madaftari ya watoto mara nyingi tumekua tukikagua miradi ya majengo ya shule, vituo vya afya, nyumba za walimu lakini ufike wakati tuwe tunakagua ubora unaotufanya tuwekeze fedha nyingi katika elimu,”alisema.

Alisema kila mwezi serikali hutoa sh.bilioni 23 kwa ajili ya uendeshaji wa shule huku akisema kuanzia Agosti mwaka huu, imekuwa ikiwapa walimu wakuu sh.200,000 kila mwezi kwa ajili ya kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana shuleni hivyo viongozi wa halmashauri hawana budi kupita kwenye shule hizo kuona upungufu unaoweza kujitokeza.

Waziri Simbachawene alisema elimu ya msingi ina changamoto nyingi hivyo aliwashukuru wadau kwa kuitikia wito wa Rais wa awamu ya tano Dk. John Magufuli kwa kutengeneza madawati kuwataka viongozi kufuatilia kwa karibu utengenezaji wa madawati hayo.

ìWakuu wa wilaya, wakurugenzi, watendaji wa kata, watendaji wa vijiji na madiwani hakikisheni madawati yanaingia madarasani, bado yapo madawati mengi kwa mafundi na makandarasi tumeyaona mengine pembezoni mwa barabara, yote yanatakiwa yawe shuleni na watoto wakalie,îalisema.

Aliwaomba viongozi wa halmashauri kutumia vizuri rasimali zilizopo hususan katika kufanya ukaguzi wa miradi mbalimbali kwa kushirikiana ikiwezekana hata kwa idara kuambatana kwenye ukaguzi ili kuthibitisha na kujiridhisha na kazi inayofanyika.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.