NEMC yaulima faini mgodi Sikonge

MZALENDO - - HABARI - NA ALLAN NTANA, TABORA

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limempiga faini ya sh.milioni 14.8, mwekezaji wa Mgodi wa Madini ya Dhahabu uliopo katika Kijiji cha Kapumpa Kata ya Kitunda wilayani Sikonge mkoani Tabora.

Akitangaza adhabu hiyo, Ofisa Mazingira Mwandamizi wa NEMC, Benjamin Doto, alisema mwekezaji katika mgodi huo kampuni ya Kitunda Gold Mine inayomilikiwa na Samweli Chitalilo, amepigwa faini hiyo kwa kutofuata sheria na utaratibu wa kupata kibali cha uchimbaji madini kutoka NEMC.

Alisema Mwekezaji huyo atatakiwa kulipa faini hiyo ndani ya siku 14 kwa kosa la kutokuwa na kibali cha NEMC pamoja na kutozingatia utaratibu wa kisheria wa utunzaji mazingira mgodini.

Alifafanua kuwa kitendo cha mwekezaji huyo kutopata kibali cha baraza kimemfanya kuendesha uchimbaji wa madini hayo pasipo kuzingatia suala la utunzaji mazingira ndio maana uharibifu wa mazingira umekuwa mkubwa katika eneo hilo.

Benjamini aliongeza kuwa mgodi huo una kasoro nyingi ikiwemo mmiliki kutokuwa na utaratibu mzuri wa utunzaji taka ngumu na wafanyakazi wake kutokuwa na mavazi rasmi ya kazi ya uchimbaji wawapo mgodini.

Akizungumza baada ya kutangazwa adhabi hiyo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina, alisema Mwekezaji yeyote katika mgodi wa madini anapaswa kuelewa na kuzingatia utaratibu wa sheria ya utunzaji mazingira ya mwaka 2004 kabla ya kuanza kazi ya uchimbaji.

Alibainisha kuwa serikali inathamani mchango wa wawekezaji katika sekta zote na ipo tayari kuwasaidia ili waendelee kuchimba madini kwa kufuata utaratibu wa sheria za nchi kama zilivyoainishwa na baraza lenye dhamana.

Alisema uchimbaji usiofuata sheria na utaratibu hauwezi kuliingizia pato taifa, ndio maana ofisi yake iko makini katika hilo na wawekezaji wote wenye tabia kama hiyo watalimwa faini sambamba na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wake mmiliki wa Mgodi huo, Samwel Chitalilo, alimpongeza Naibu Waziri kwa ujio wake katika mgodi huo na kuishukuru serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kwa kumpa leseni ya kufanya utafiti na uchimbaji mdogo huku akijitetea kuwa awali hawakupata maelekezo mazuri kuhusu utaratibu wa NEMC.

Aliomba serikali kuwabana maofisa madini kwani ndio wanaosimamia uchimbaji madini hivyo walipaswa kutoa maelekezo kwa wamiliki wa migodi mapema kabla hawajaanza shughuli za uchimbaji.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.