Familia ya Mwalimu Nyerere yawaasa vijana

MZALENDO - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

WATANZANIA wametakiwa kuepuka matumizi ya dawa za kulevya ili kulifanya taifa na vijana kwa ujumla kuishi kwa amani na utulivu.

Kauli hiyo imetolewa na mjukuu wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Moringe Magige kwa niaba wa familia ya Mwalimu wakati wa kuwashukuru vijana wa Taasisi ya Ushauri wa Kuzuia Dawa za Kulevya Tanzania (IOGT) waliofika kufanya usafi wa mazingira nyumbani kwa Baba wa Taifa, Msasani, Dar es salaam.

“Mwalimu Nyerere alianza uongozi akiwa kijana kwa hiyo vijana wanao wajibu wa kukemea matumizi ya dawa za kulevya kama njia ya kupambana na vitendo viovu nchini,îalisema Moringe.

Alisema kwa kupambana na dawa za kulevya taifa litapata mafanikio makubwa kwa sababu dawa hizo zimekuwa zikiathiri nguvu kazi ya Taifa.

Akielezea jina la Moringe, alisema alipewa na Hayati Mwalimu Nyerere kumuenzi Waziri Mkuu wa zamani Edward Moringe Sokoine aliyefariki kwa ajali ya gari mwaka 1984 akitoka bungeni mkoani Dodoma.

Mapema vijana wa IOGT walieleza athari zinazosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya kama bangi na cocaine kuwa chanzo cha kuzorotesha maendeleo ya taifa.

Mkurugenzi wa IOGT Mohamed Lichonyo, alisema vijana wa shule za msingi na sekondari wamekuwa wakiendeleza juhudi za kupambana na matumizi ya dawa za kulevya kwa kutoa elimu kwa jamii kwenye ngazi hiyo jambo alilosema ni mafanikio makubwa kwa vita hiyo.

Alisema wazazi wamekuwa mstari wa mbele kukemea matumizi ya dawa za kulevya kwa kushiriki kutoa wito kupitia mikutano ya hadhara shuleni na maeneo mbalimbali nchini.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.