Profesa Mbarawa atema cheche kwa mkandarasi

MZALENDO - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Sinohydro Corporation anayejenga barabara ya Dodoma-Mayamaya yenye urefu wa kilomita 43.65 kukamilisha ujenzi huo ifikapo Novemba, mwaka huu.

Akizungumza baada ya kukagua barabara hiyo mkoani Dodoma na kuridhishwa na ujenzi wake, Profesa Mbarawa alisema barabara hiyo ni muhimu kwani ni kiungo kikuu kwa watu wanaosafiri kati ya mkoa wa Dodoma, Manyara, Arusha na nchi za Kusini mwa Afrika.

“Kamilisheni kipande hiki kilichobaki haraka kwani barabara hii ni kiunganishi cha nchi za Kaskazini na Kusini mwa Afrika, hivyo kukamilika kwake kutasaidia kufungua fursa za kibiashara na kukuza uchumi wa nchi,”alisema.

Alimtaka mkandarasi huyo kuzingatia viwango bora vya ujenzi wa barabara kama ilivyo kwenye mkataba na kuhakikisha thamani ya fedha katika ujenzi huo inaonekana.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, alimhakishia Waziri Mbarawa kusimamia barabara hiyo kwa mujibu wa sheria za barabara ikiwemo kuzuia wananchi wasivamie miundombinu ya barabara na kuzuia mifugo kuchungwa barabarani.

“Nitasimamia sheria za barabara, kwani mradi huu ni mkubwa na serikali imetumia gharama kubwa katika ujenzi wake, hivyo ni lazima niutunze ili udumu,”alisema.

Barabara ya Dodoma - Mayamaya ni sehemu ya mradi wa barabara ya Dodoma - Babati yenye urefu wa kilomita 188.15 uliogharimu sh.bilioni 40.

MWANDISHI wa Habari wa Kampuni ya Uhuru Publications Limited (UPL), wachapishaji wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, Mariam Mziwanda, akipokea cheti baada ya kuhitimu mafunzo ya kuandika habari za usalama barabarani kutoka kwa Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamaii, Wazee na Watoto, Dk. Mohamed Mohamed, Dar es Salaam. Mafunzo hayo yalioandaliwa Taasisi ya Habari Tanzania (TMF). Kulia ni Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura. (Picha na Jumanne Gude).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.