Vijana watakiwa kuungana

MZALENDO - - HABARI - NA ANGELA SEBASTIAN, BUKOBA

VIJANA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kujiunga kwenye vikundi vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) ili waweze kutumia fursa za mokopo zinazojitokeza kuzalisha mali, kujiinua kiuchumi na kupunguza malalamiko ya ukosefu wa ajira.

Rai hiyo ilitolewa katika manispaa ya Bukoba na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Kagera, Amimu Muhamud, wakati akizungumza na vijana kwenye kilele cha maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Muhamud alisema endapo vijana watajiunga katika vikundi watakuwa na uwezekano mkubwa wa kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali zinazotoa huduma hiyo au serikalini na kwamba ni vigumu kumkopesha mtu mmoja mmoja.

“Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, msiwe wadhaifu unganeni muwe na nguvu ya pamoja, fursa zipo nyingi za kujiinua kiuchumi zinazohitaji watu walioungana. Mtapata mikopo inayotokana na asilimia tano ya mapato ya ndani ya halmashauri inayotengwa kwa ajili ya vijana,”alisema.

Aidha, aliwataka vijana hao kutumia vikao vyao kujadili namna ya kujenga nchi na Chama na kujihadhari na watu wenye uchu wa madaraka ambao huwadanganya wakati wa uchaguzi ili wawachague na baadaye kuwatelekeza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Bukoba Mjini, Ashraph Kazinja, alisema lipo tatizo la ajira kwa vijana na kuwataka kuungana ili kukabiliana na changamoto hiyo.

“Wanafunzi ambao bado mko shuleni someni kwa bidii ili elimu hiyo iweze kuwasaidia kukabiliana na tatizo la ajira baada ya kuwa na viwango vinavyokubalika ndani na nje ya nchi, lakini pia vijana mlioko kazini fanyeni kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko chanya katika vitengo mnavyofanyia kazi,”alisema.

Kazinja alisema kwa kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa anapenda ushirikiano na uchapakazi, vijana wanapaswa kumuenzi kwa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu, kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro aliungana na vijana hao kwa ajili ya kuadhimisha siku y vijana na kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kutumia fursa hiyo kuwataka kuipenda nchi yao na kuitumikia.

“Baba wa taifa alikuwa mzalendo wa kweli, lazima vijana tulitambue hilo na tulitumie, kwa kuwa uzalendo wa kweli nchi itakwenda pabaya huku nyinyi mkiwa ndio nguvu kazi ya taifa,”alisema Kinawiro.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.