Wapinzani watakiwa kuonyesha vitendo kama inavyofanya CCM

MZALENDO - - HABARI - WILIUM PAUL, MWANGA

VYAMA vya upinzani nchini vimeshauriwa kuachana na maandamano na vurugu zisizo na tija kwa taifa badala yake vipeleke nguvu hizo katika elimu.

Vimetakiwa kujenga shule ili zishindane na zile zinazomilikiwa na Jumuia ya Wazazi ya CCM katika kutoa elimu bora na kulinufaisha taifa kwa vitendo.

Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, Aaron Mbogho aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Mwanga inayomilikiwa na jumuia hiyo.

Mbogho alisema jumuia ya Wazazi imejikita katika kuhakikisha inawakomboa Watanzania kwa kupambana na maadui ujinga, maradhi na umaskini kuanzisha shule za sekondari na vyuo ambavyo hutoa elimu obora na zenye ushindani kwa taifa.

Alisema vyama vingine vya siasa vinapaswa kuiga mfano wa CCM kwa kuanzisha shule ili viweze kuleta changamoto katika utoaji huduma bora kupitia shule za vyama vya siasa.

“Kama vyama vya siasa vitaiga mfumo wa CCM kwa kuanzisha shule za wazazi itasaidia taifa kujiletea maendeleo kwa kuwa na wasomi wengi na kuahidi kutoa ushirikiano kwa vyama vya upinzani vitakavyotaka kuja kuwekeza wilayani Mwanga kwa kujenga shule,” alisema.

Akizungumzia changamoto ya uhaba wa ardhi inayoikabili shule hiyo, Mkuu wa Wilaya alisema atahakikisha anashirikiana na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mwanga ili kuona uwezekano wa kutatua changamoto hiyo.

Aidha, Mbogho alitoa wito kwa Wazazi nchini kutoua vipaji vya watoto wao walivyonavyo kwa kuwa ndio ajira zao za badae huku pia akitoa wito kwa Wanafunzi kuhakikisha wanatulia pindi wanapoingia katika mitihani Novemba Mosi mwaka huu na kujibu maswali kulingana na maelekezo yaliyowekwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Mkoa wa Kilimanjaro, Festo Kilawe aliiomba serikali kuzisaidia shule za jumuia hiyo kwa kuzifutia kodi mbalimbali zinazotozwa sasa na kudai shule hizo hazifanyi biashara bali zinatoa huduma ya elimu kwa jamii.

Awali akisoma kwa mgeni rasmi, Mkuu wa Shule hiyo, Mena Kengera, alisema shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa eneo kwa kuwa hivi sasa wanalo eneo la ukubwa wa ekari tatu tu ambalo halitoshi kuwa na huduma muhimu kama viwanja vya michezo hali inayochangia kushindikana kwa upanuzi wa shule kwa maendeleo ya badae.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.