CCM Korogwe yaunga mkono udhibiti wa waharibifu misitu

MZALENDO - - HABARI - NA SOPHIA WAKATI, KOROGWE

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Korogwe Vijijini, kimeunga mkono jitihada za serikali wilayani humo kuvunja mtandao wa hujuma ‘wizi’ dhidi ya mazao ya misitu.

Pia, kimesema hakitamkingia kifua kiongozi yeyote wa Chama ambaye atajihusisha na vitendo vya wizi ikiwemo hujuma katika mali na nyara za serikali.

Tamko hilo lilitolewa wakati Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mhandisi Robert Gabriel, akitangaza kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wa wizi wa mazao ya misitu.

Watumishi kadhaa wa Wakala wa Misitu (TFS) tayari wametiwa nguvuni wakidaiwa kuhusika na hujuma za bidhaa za misitu, ambapo DC huyo ameahidi kuanza nao katika kuhakikisha wanashughulikiwa kinidhamu.

Katibu wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini, Jumanne Kitundu, alisema kutokana na kushamiri wizi wa mazao ya misitu na mkuu wa wilaya kuanza kuwasaka wahalifu kwa lengo la kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, CCM inamuunga mkono kiongozi huyo wa serikali.

Alisema kuwa kinawalaani vikali wote waliojiunga kwenye mtandao wa hujuma dhidi ya mazao ya misitu kutokana na ukweli kwamba wamekuwa ni watu wenye kujali kunufaisha matumbo yao bila kuzingatia maslahi ya umma na pasipo kudhibiti jangwa hilo.

Pia, alisema Chama chake ndicho chenye ilani inayotekelezwa na tangu Gabriel afike wilayani humo, ameonyesha njia kwa kuwashughulikia wezi na watumishi wasiozingatia maadili mazingira ambayo yatasaidia kuleta neema kwa jamii.

Alisema inatakiwa kila mwananchi kuwa mzalendo kwa nchi yake kulinda rasilimali zilizopo huku akisistiza umuhimu wa viongozi wote kujenga uaminifu sanjari na watumishi wa idara zote kuzingatia uadilifu kwenye kazi zao.

Wakati CCM ikitoa kauli hiyo, naye DC Gabriel, alisema mbao zilizokamatwa ikiwa ni sehemu ya mazao ya misitu huko Kijiji cha Zege, Kata ya Dindira, Tarafa ya Bungu zimerejeshwa mikononi mwa serikali ili kutumika kwa maslahi ya umma.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.