Waziri Mwigulu Nchemba watizame askari hawa

MZALENDO - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

KUMEKUWEPO na sintofahamu kwa maofisa wapya wa Jeshi la Uhamiaji waliomaliza mafunzo yao ya uaskari, Juni 24, mwaka huu pale Chuo cha Polisi Moshi, kutopewa baadhi ya malipo yao.

Tayari vyombo vingi vya habari, vimetoa taarifa hiyo lakini ni wakati wa Wizara ya Mambo ya Ndani, kusimama kidete na kuondoa masikitiko hayo kwa vijana hao ambao hadi sasa hawajapata mishahara wala posho walizotakiwa kupata tangu Julai mwaka huu 2016.

Wameshapitisha miezi mitatu bila kupata chochote na hakuna majibu yoyote wanayopata kutoka kwa wakubwa wao zaidi ya ahadi zisizotimizwa watasaidiwa kupata fedha hizo watulie wakati Uhamiaji ikifanya taratibu.

Ni wakati wa Waziri Mwigulu Nchemba, kufanya kila liwezalo kuhakikisha anatoa mwongozo kwa maofisa hao, kwa kuwa uchapakazi wake na ueledi umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wengi wanaoamini kuwa wao ndio muhimu katika kuleta maendeleo kwa wananchi.

Kutopewa mishahara na posho kwa askari hao, ni fursa nyingine kumaliza tatizp hilo, ambalo linaonekana kuchipuka kwa kasi huku kila mmoja anaonekana kutokuwa tayari kuwahudumia askari hao kwa kupata stahiki zao.

Kulipwa stahili kwa askari hao, kutaongoza ari na uwajibikaji kwa kuwa askari wengi waliochukuliwa na uhamiaji ni vijana, ambapo naamini watafanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa huku kila mmoja akifurahia kazi yake aliyokuwa nayo.

Serikali sikivu ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli italifanyia kazi suala hilo, ambalo kumekuwepo na habari tofauti dhidi ya askari hao wapya wa uhamiaji ambao kwa namna moja au nyingine wameendelea kutojua hatma yao ya baadae.

Mfanyakazi kufanya kazi kwenye mazingira mazuri ni suala nzuri, ambalo kwa muda mrefu serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inamaliza matatizo ya wafanyakazi, hivyo suala hili tunaimani litakwisha na kila mfanyakazi kuwa na amani.

Hivyo, Waziri Mwigulu litazame suala hili kwa umakini mkubwa ili kuwasaidia vijana hawa, waliokuwa mstari wa mbele wa kuhakikisha wanalitumikia Jeshi hasa Uhamiaji kwa ufanisi mkubwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.