UVCCM: Dk. Magufuli anatimiza malengo ya TANU na ASP

MZALENDO - - MAKALA - NA MWANDISHI WETU, SIMIYU

WAKATI ikiwa ni miaka 17 sasa tangu Baba wa Taifa Hayati, Mwaalimu Julius Nyerere afariki dunia, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umesema utendaji wa Rais Dk. John Magufuli katika kipindi cha mwaka mmoja madarakani ametekeleza kwa vitendo madhumuni na malengo ya uanzishwaji wa vyama vya TANU na ASP. Pia, umeeleza kuwa licha ya fikra, mikakati, malengo, sera, maazimio yatokanayo na misingi ya kitaifa, sasa inatekelezwa kwa vitendo na ujasiri mkubwa. Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, amehojiwa na gazeti hili, wakati akifungua kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Kata ya Sipiwi Wilaya ya Bariadi mkoani hapa. Shaka anasema dhamira, misingi na madhumuni ya kuanzishwa vyama vya TANU na ASP kulilenga kuwakomboa waafrika katika madhila ya unyonge, umasikini ili kuwapatia haki, huduma bora, elimu, uhuru na kuchochea maendeleo.

Anasema licha ya hayati Mwalimu Nyerere kuondoka duniani, malengo hayo na madhumuni yote yanatekelezwa kwa vitendo na serikali ya Rais Dk. Magufuli ambayo imeamua kupigania maslahi ya wanyonge na hatimaye kujenga uchumi imara.

“Watanzania wanaona fahari wanapomuona Rais Dk. Magufuli akipita juu ya nyayo za Mwalimu Nyerere huku akitekeleza kwa vitendo madhumuni na malengo ya vyama vya TANU na ASP “anasema shaka.

Aidha, anawaeleza wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM kata ya sipiwi kwamba kitendo cha kukutana kwao na kufuata kalenda ya vikao vya kikatiba vya chama, kunaonesha uhai na maendeleo ya CCM.

Kaimu Katibu Mkuu Shaka anasema waasisi wa Taifa walitumia akili, maarifa na kuona mbali hatimaye wakafanikiwa kukiwekea misingi madhubuti Chama Cha Mapinduzi kwa kutazama maslahi mapana ya umma.

“Kwa bahati mbaya sasa ni miaka 17 tangu Mwalimu Nyerere atutoke, taifa letu limeendelea kubaki moja, lenye mshikamano, umoja wa kitaifa , amani na maendeleo, kwa gharama yoyote tutamuenzi Mwalimu Nyerere na UVCCM itafuata nyayo zake,”anasisitiza.

Shaka anawahimiza wanachama wa CCM Kata ya Sipiwi kuendelea kushirikana na mbunge wao, Mtemi Andrews Chenge ambaye yuko ziarani katika jimbo lake huku akishiriki vikao vya tathmini ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Kwa upande wake, Katibu wa Siasa na Uenezi wa Kata hiyo, Omar Brandy, anamshukuru Shaka kwa uamuzi wake wa kuja na kushiriki kikao hicho cha juu cha Kata huku akidai kitendo hicho kimewapa faraja wanachama wa CCM.

Brandy akizumgumza kwa niaba ya wanachama wenzake alisema wameridhishwa na utendaji wa Rais Dk. Magufuli huku akisema ni jambo la kujivunia kwa CCM mwaka 2015 kumsimamisha mgombea bora wa urais na baada ya kushinda kwake sasa anaonyesdha uzalendo kwa vitendo.

Naye, Mwenyekiti wa Tawi la CCM Sipiwi Marry Masunga, anamuomba Kaimu Katibu Mkuu kuwafikshia salaam zao kwa Rais Magufuli na kusisitiza kuwa sasa kila mtanzania anajipanga kafanya kazi na si kupiga porojo.

“Mfikishie salaam zetu Rais na umueleze kuwa yanayotekelezwa na serikali yake yanawatia ari wananchi, yanaridhisha na kumtaka asikubali kukatishwa tamaa na vyama vya upinzani na vibaraka wao,”anasema.

Hivyo, Shaka anasema ni wakati wa kila mmoja kwa vijana ndani ya CCM, kuhakikisha wanafanya kila linalowezekana kukimboa Chama kwa kuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo kwenye jamii.

MKUU wa mkoa Simiyu Anthony Mtaka (kushoto) akimsikiliza kwa makini Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM UVCCM) Shaka Hamdu Shaka (katikati) aliyefika ofisini kwake kumtembelea siku moja kabla ya kuhitimishwa kwa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu mapema wiki hii. Mwingine ni Mbunge wa Itirima, Njalu Silanga. (Picha na Fahd Siraji)

KAIMU Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.