NANI DIKITETA

MZALENDO - - MAKALA - NA ELIAS SABUNI: Email: eliassabuni@yahoo. com Mobile No. +255756 341989.

KABLA sijaenda mbali katika harakati ya kutaka kujua, maisha na uhai wa mwanadamu, inakuwaje mtu uitwe dikiteta.

Waumini wa imani mbalimbali za kumcha Mwenyezi Mungu nawaombeni msamaha endapo mtakutana na maneno yatakayogusa imani zenu.

Tafakari inayotolewa na wataalamu kwa lugha za kibinadamu ni kuwa, Dikteta ni mtu katili asiyesikia la mtu, analoamua yeye ni lazima lifanyike hivyo.

Je, Mwenyezi Mungu ni dikteta? Kuna mambo mengi ambayo mwanadamu amekatazwa asiyafanye na pale anapokosea akayafanya, Mwenyezi Mungu anatoa adhabu, je huo ni udikteta?

Ili kiongozi wa familia uweze kuiendesha familia yako vema, ni lazima uwe na mambo ambayo mwanafamilia usipoyafanya inavyotakiwa lazima apate adhabu.

Kama Mwanadamu anaweza kuacha kutekeleza maagizo ya muumba wake, Je wewe mwanadamu mwezie ataweza bila kuwepo na tofauti?

Mwanadamu anapoadhibiwa na Mungu hukimbilia kusema ” Hayo ni mapenzi ya Muumba.”

Hivi unapopewa adhabu na aliyejuu yako kwani nini usione hiyo ni mapenzi ya aliye juu yako? Hakuna baba au mlezi wa familia anayetaka familia yake ipotee. Hivyo hivyo hakuna kiongozi wa nchi ambaye anapenda kuliona taifa lake linaharibikiwa.

Mwenyezi Mungu alipomuumba mwanadamu kwa mapenzi yote alimkabidhi kuitawala dunia na vyote vilivyomo, lakini kwa uharamia wa shetani aliamua kuzunguka huku na kule, na alipoona Muumba yupo mbali kidogo akamshawishi yule mama na kufanya maasi.

Hivyo hivyo, wanadamu wenye mapenzi shaka, huzungukiwa na shetani na kuwashawishi kutoa lugha chafu hadi kumuita Kiongozi Mkuu wa Taifa lao ‘dikteta’.

Katika kutafuta kutawala au kuongoza taifa ni kawaida wagombea hupita wakitangaza nini watafanya katika kipindi cha utawala wao.

Ahadi hizo ndizo zinajulikana kama “sera” ya chama huzika. Si rahisi kubadilisha sera hizo bila kibali cha chama husika, lakini kutokana na mabadiliko ya maisha, mhusika ama aweza kupendekeza mambo zaidi na kupata kibali cha chama.

Katika kipindi cha utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kuna mambo matatu ambayo hayakuwemo kwenye Ilani ya Chama ambayo aliyafanya kwa kupata kibali cha Chama. Kikwete aliazisha shule za kata, mchakato wa katiba na Bunge la Katiba.

Wapinzani hilo la katiba kwa kuona kuwa sasa wamepata nafasi ya kuleta mabadiliko walilivalia njuga hata wakapata walichokiita Umoja wa Katiba ‘UKAWA’. Raha ya ngoma ingia ucheze.

Hapa wapinzani na hata wasio wapinzani walifurahia sana mchakato huo. Lakini ukitumia kiona mbali; wengi walifurahia hili maana liliwapa mwanya wa kujipatia pesa. Jinsi walivyounda njia za kuchelewesha, ndivyo walivyojipatia fedha za kula.

Tume ya Katiba ambayo baadaye ilipewa jina la “Tume ya Warioba”ilitumia kiasi cha sh. Bilioni 69 na Bunge la Katiba sh. bilioni 49, na bado hatukupata katiba.

Wapinzani sio hela hiyo tu waliyotumia bali walienda hadi nje ya nchi na kupewa ufadhili wa mamilioni wakidai kufanya kampeni ya kupambana na mchakato mbaya wa Katiba ya CCM.

Wakati mabilioni ya fedha yakitumika bila kupata mafanikio, shule zilizoanzishwa na zile za msingi, watoto walibaki wakisoma bila madawati. Sasa uchanguzi umekamilika na Rais wa Awamu ya Tano ameanza kazi na kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”.

Mchakato wa Katiba umepumzishwa kidogo, na watoto sasa wamepata madawati, na walimu kupata haki zao kwa wakati. Hao walioshiba kutokana na mchakato wa Katiba, sasa wanadai Dk John Magufuli ni “Dikteta.” Je ni kweli au kuna walichokosa ndio maana wanamwita “Dikteta”.

Mungu alipomkabidhi Adamu na Eva Bustani ya Edeni aliwaambia chochote katika bvustani hii tumieni lakini Matunda ya ule mti wa katikati ya Bustani Msile.

Je huo ulikuwa ni Udikteta? Dk. John Magufuli, amewaambia wanasiasa wote kuwa sasa ni kazi tu, siasa na maandamano ni dalili ya mizozo. Lakini ni vipi hawa watu wamuone ni Dikteta? Je, wao hawataki kufanya kazi ili kuwaletea wananchi maendeleo?

Adamu na Eva; Ibilisi aliwarubuni na wakala Matunda ya Mti ule. Matokeo yake tunayajua. Vivyo hivyo, wanasiasa wetu, kuna ibilisi wa ndani na nje, ambao wanawashawishi kula tunda la kuendesha mikutano na maandamano.

Ubishi wa namna hii watanzania wenye macho tumeona matokeo kutoka nchi zenye ushindani wa namna hii. Swali kubwa la kujiuliza, Ni nani huumia kwenye ushindani huo? Ibilisi ile adhabu ya Mungu kwa Adamu haikumgusa mara moja na hivyo hivyo, mateso ya ushindani wa siasa viongzi wa vyama hayawaumizi mara moja lakini Raia wengi huathirika.

Kama siasa ingekuwa ni dini, basi watu wengi sana wangeenda motoni, maana lugha na maneno mengi ya wanasiasa huwa na utamu kama yale matunda ambayo Adamu na Eva yaliwafanya wamkosee Muunba wao.

Hebu jiulize maisha waliyopoteza watu na mali zao Syria, Nigeria -Boko Haram, Sudan, Somalia, Congo na hata huko Pakistani.

Wosia wa “Siasa” kwa Watanzania tusidanganyike, tulindeni kauli ya Baba wa Taifa ya kuwa na siasa njema na uongozi bora.”

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.