D R A M A -3

Sakata hili la onyesho la “Kidrama” lafananisha kuwa kiongozi mpya yupo “IKULU” na kiongozi wa zamani yupo “MSITUNI” kama “gorila” mpiganaji.

MZALENDO - - MAKALA - Na Dk. Muhammed Seif Khatib muhammedkhatib@yahoo.co.uk

KATIKA hali ya kawaida na ni utamaduni unaokubalika kwa mataifa na tawala zote duniani yakitokea mapigano au vita ama uasi ambao hatima yake husababisha kiongozi mkuu wa taifa au serikali kuondolewa madarakani hali hiyo huitwa Mapinduzi.

Mapinduzi hayo yanaweza kufanywa na askari, jeshi, kundi la watu maalumu au miongoni mwao viongozi ama kiongozi mkuu au familia yake.

Mapinduzi yanaweza yakapangwa na kutekelezwa kutoka ndani ya nchi au nje ya mipaka.

Lakini kuondoshwa kwa nguvu kwa kiongozi katika “Ikulu” au katika “Kasir” yake na wakati mwingine katika makao makuu yake au nchi yake, huhitimisha kusitishwa kwa mamlaka yake.

Yule anayeshika makao makuu ndiye anayekuwa mtawala. Jambo linalobaki na kuwa mjadala ni kiongozi halali au la, wengine watamtambua na wengine hawamtambui.

Na yule kiongozi wa zamani aliyepinduliwa na kubaki nje ya makao Makuu ya Utawala huitwa “Mpinzani” au “Mwaasi”.

Katika muktadha huu, yule kiongozi wa chama aliyevamia makao makuu ndiye kiongozi halali.Isitoshe akatambuliwa msajili akiwa kiongozi wa mamlaka ya vyama vya siasa.

Kiongozi huyo mpya akatangaza uongozi mpya akiwa ndani ya makao makuu rasmi. Yule aliyepinduliwa na kufanya kazi zake nje ya makao makuu, ambaye anapaswa kuitwa “Mwaasi”, yeye hamtambui kiongozi huyo aliyejinyakulia madaraka kwa nguvu.

Sakata hili la onyesho la “Kidrama” lafananisha kuwa kiongozi mpya yupo “IKULU” na kiongozi wa zamani yupo “MSITUNI” kama “gorila” mpiganaji.

Lakini kawaida viongozi wanaoingia madarakani kwa nguvu huwa na sababu zao zilizowasukuma kufanya hayo Mapinduzi.

Bila shaka sababu alizotoa, ilikuwa kuzikubali au kuzikana, hilo ni jambo lingine.

Kiongozi aliyeingia madarakani kwa” nguvu ”aghlabu kwa siku za awali sio aghlabu kuondoka au kusafiri na kuacha makao makuu. Huyu kiongozi anajiamini.

Amefanya ziara katika mikoa ya Lindi na Mtwara na huko alipokelewa kwa shangwe. Bila ya shaka yapo maeneo mengine ataenda ikiwemo Tanga na Tabora.

Onyesho la drama hii ni kule kwa msajili kumhalalisha kiongozi kuandika barua katika benki na kumuhalalisha awe na uhalali wa matumizi.

Hili ni eneo nyeti ambalo kiongozi aliyepinduliwa “Muasi” pamoja na kundi la bodi lililomeguka, kila upande kwa namna yake, wakaandika barua kumweka zuio kiongozi mpya.

Kwa wahusika wa benki hawajitokezi jukwaani, sisi watazamaji au hadhira hatujui nani kuruhusiwa kutumia fedha za walipa kodi zinazogombaniwa.

Onyesho lingine la “KIDRAMA” limetuchukua nje ya lango kuu la Mahakama Kuu.Kupitia kinywa cha wakili dhidi ya Kiongozi aliyeko madarakani, akiwa amezungukwa na washabiki wake, mbele ya waandishi wa habari, alieleza kuwa mahakama imekubali kumburuza mahakamani kiongozi “aliyejinyakulia madaraka”.

Huko atakwenda kujibu mashitaka ya kuingia makao makuu, kutangaza viongozi wake, kutaka kudhibiti fedha za chama na kujitangaza kama yeye ndiye mwenyekiti halali.

Huku akiwa amevaa shati jeupe lenye mashada shingoni na koti jeusi na kwa mbwembe za kiwakili, aliwahakikishia kuwa mashitaka na vielelezo vyake, watafanikiwa.

Lazima kiongozi huyo aliyejitangazia uenyekiti atasulubiwa mahakamani. Onyesho la Mtwara na Lindi limetikisa kambi ya waasisi walipo “Misituni” licha ya kiongozi mpya kupokewa kwa shangwe na hoihoi, madiwani wengi wameonekana kumuunga mkono.

Aidha, wamepiga sauti zao kwa kuwataka viongozi wa UKAWA waache kuingilia chama chao. Waache unafiki wa kujidai kuipenda kambi moja na ili hali wanafurahia mgogoro huo kwa faida yao.

Wakati huohuo katika jukwaa la msajili sauti nyuma ya pazia imesikika ikipazwa na kunena ofisi yake inamtambua pia kiongozi aliyeko msituni kuwa naye ni kiongozi halali kama alivyo yule aliyevamia makao makuu.

Hata hivyo anamkataa huyu mwenyekiti wa muda aliyepewa kienyeji na kujigamba katika majukwaa na kuongea na waandishi habari mara kwa mara.

“DRAMA” hii yenye maonyesho katika majukwaa tofauti na wahusika tofauti huenda yakahamishiwa maonyesho yake katika eneo moja na jukwaa moja badala ya sasa maonyesho kuwa huku na huko.

Itabidi waigizaji wote wakusanyike pamoja. Jengo la maonyesho litakuwa mahakamani.Jukwaa la maonyesho litakuwa ni kizimbani.

Katika onyesho na maonyesho yatakayofuata pazia litafunguliwa na onyesho la igizo la kimahakama. Hapa wapo wataoingiza uhakimu au ujaji na mbwembwe zote. Igizo la mahakamani kutakuwa na upande wa wanaoshitaki na kushitakiwa.

Kutawekwa mezani shitaka lenyewe. Bila ya shaka mshitakiwa atakuwa pandikizi la jana dume la Kinyamwezi kutoka Tabora. Yule anayeshitaki atakuwa baba la Kisuranama la miraba minne na madevu husemi Hemed Bin Marej “Tip Tip” wa Mtambwe Pemba.

Jukwaani itakuwa mara ya kwanza mafahali hawa waliokuwa chanda na pete kukutana uso kwa mboni. Tusubiri jaji aingiye onyesho lianze tujuwe mbichi na mbivu. Tusiandikiye mate! Utamu wajaa!

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.