Katu ushoga usipewe nafasi

MZALENDO - - MAKALA - Huo NI MTAZAMO. Na Solomon Mwansele suney27@yahoo.com 0713 349299

NAAM, ni miaka 17 sasa imetimia tangu muasisi wa taifa letu, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, atangulie mbele za haki. Hakika Watanzania tutazidi kukuenzi na kuzitumia busara zako katika kuvuka magumu yanayotupata kama Taifa.

Nimejikuta nashikwa na kigugumizi na kushindwa kuelewa hawa Wamarekani wanatutakia nini Watanzania wa Nyerere, kwa kutaka kutuingizia utamaduni ambao kamwe hatuujui na wala hatuutaki. Ni utamaduni huu wa ushoga.

Serikali tayari imetoa tamko kwamba haitawavumilia watu ama taasisi yoyote itakayobainika kuhusika na uhamasishaji wa vitendo vya ndoa za jinsia moja nchini, kwa kuwa vitendo hivyo ni kosa la jinai.

Imesema bila kificho kwamba hatua kali za kisheria itazichukua dhidi ya mtu, kikundi ama taasisi itakayobainika kufanya uhamasishaji, kuficha na kuendesha vitendo vya hovyo nchini.

Hatua hiyo ya serikali inafuatia kauli iliyotolewa na Serikali ya Marekani, kuwa Tanzania inakiuka haki za binadamu kwa kutowatambua na kuwabagua katika kuwapatia huduma za afya watu walioathirika na ugonjwa wa ukimwi, kifua kikuu na wale wanaojihusisha

na ndoa za jinsia moja.

Kwa mujibu wa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk.Harrison Mwakyembe, Tanzania haijawahi kuwa na sheria, sera, kanuni au muongozo ambao unalenga kuwabagua waathirika wa magonjwa hayo kwani waathirika wote wanapata huduma zote stahili.

Kuna muda mwingine mtu unaweza kuwaza na kufika mbali na kujiuliza hivi hawa

Wamarekani wanatutafuta nini sisi Watanzania?Yaani wanataka tuwe taifa la kusema ndiyo mzee hata kwa mambo ya kipuuzi kama ushoga?Kwa kweli wanatakiwa watambue kuwa hilo haliwezekani katu.

Hapana, hawa Wamarekani wanatakiwa kutambua kwamba Tanzania ni taifa huru, hivyo kamwe hatuwezi kukubaliana na mambo yasiyo ya msingi huku tukitambua wazi kuwa huo siyo utamaduni wetu.

Dk.Mwakyembe alisema Serikali ya Awamu ya Tano, haiko tayari kuendeshwa huku ikiangalia sheria za nchi zikivunjwa, kupitia vitendo visivyo vya kimaadili na hatimaye kuiletea nchi madhara makubwa kwa wakati huu na baadaye.

Kuna asasi 15 nchini zenye uhusiano na nchi zilizoendelea ambazo zinajihusisha na uhamasishaji wa vitendo vya ndoa za jinsia moja kwa mwamvuli wa kusaidia harakati za ugonjwa wa kifua kikuu na ukimwi.

Asasi hizo zinaelezwa zimejikita kuendesha uhamasishaji katika mikoa 11, ambayo ni Dar es Salaam, Arusha, Shinyanga, Mbeya, Iringa, Tabora, Dodoma, Kilimanjaro, Njombe, Lindi na Morogoro.

Naam, sasa ndiyo nimeanza kupata picha juu ya mchezo huu mchafu, kwani hivi karibuni wanaandishi wa habari mkoani Mbeya walipata taarifa kuhusu kufanyika kwa semina iliyowahusisha mashoga, ambayo ilikuwa inafanyika katika hoteli moja maarufu jijini humo.

Awali, sikuamini kama hilo kweli linaweza kufanyika Mbeya, kwani kwa utamaduni wa mkoa wa Mbeya, hauna sifa ya kuwa na mashoga, japo kimsingi kwa kuwa huu ni mchezo unaoenea huwezi kuwakosa kabisa.

Niipongeze Serikali Wilaya ya Mbeya, chini ya Mkuu wa wilaya hiyo, Paul Ntinika, kwa hatua thabiti aliyoichukua kwenda eneo la tukio na kuwatia mbaroni baadhi ya wahusika waliokuwa wanashiriki semina hiyo.

Kitu cha kushangaza na kuhuzunisha semina hiyo iliandaliwa na shirika moja ambalo limekuwa linajionyesha lipo mstari wa

mbele katika kupambana na ukimwi, kwa kugawa kondomu kumbe hiyo ni janja yao tu, kwani nyuma ya pazia wana madudu yao wanayafanya.

Watanzania kamwe tusikubali kuiga hata mambo ambayo ni chukizo kwa Mungu, tusimame pamoja na kukemea vitendo hivi, ili kulifanya taifa letu liendelee kwa na heshima mbele ya

mataifa mengine. Umefika wakati sasa Marekani inatakiwa kutambua, kwamba kamwe haiwezi kutupangia cha kufanya kwa vile tu yenyewe ni nchi tajiri na imepiga hatua kubwa katika sayansi na teknolojia.Hapana hapo tutaonana wabaya ni vyema tuwaeleze ukweli hawa ili wakome.

Nakubaliana na Dk.Mwakyembe kwamba kuna asasi, zimekuwa zikifanya mikutano ya siri na sherehe usiku, kuandaa na kuchapisha machapisho yanayohamasisha vitendo hivyo, kusambaza vilainishi na kondomu na kupeleka elimu ya ushoga katika shule za msingi na sekondari.

Hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuwa makini, kwa kuhakikisha anatoa taarifa za haraka, mara tu pale anapohisi kuna semina ama mkutano wa mashoga,kwenye vyombo vya sheria ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa.Kamwe tusikubali kuufumbia macho upuuzi huu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.