Uaminifu na uadilifu wa Mwalimu Nyerere bado wa kukumbukwa

MZALENDO - - MAKALA - NA EMMANUEL MOHAMED

MIONGONI mwa mambo yanayotajwa katika maisha ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambayo yanakumbukwa kwenye maadhimisho ya kifo cha miaka 17 ni uaminifu na uadilifu kwenye uongozi wake.

Oktoba 14, mwaka huu ilikuwa siku ya maadhimisho ya miaka 17 ya kifo cha Mwalimu Nyerere ambapo kulikuwa na makongamano kadhaa ya kumbukizi juu ya maono yake ya maendeleo katika taifa hili.

Makongamano hayo yalijikita zaidi kwenye lengo la kutoa mafundisho kwa viongozi wa sasa na kizazi kijacho ambapo Rais wa awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, alihudhuria na kueleza namna Mwalimu Nyerere alivyokua akiwataka viongozi kuwa na maisha ya uadilifu.

Mwinyi anasema maadhimisho ya miaka 17 ya kifo cha Mwalimu Nyerere yanatakiwa kuenziwa kwa kuzingatia maono yake hususan kwa vitendo ikiwemo suala muhimu la uadilifu na uzalendo ambapo ndio msingi wa maendeleo halisi.

Anasema Baba wa taifa alikuwa akitekeleza dhana ya maendeleo kwa uhalisia wake na si juu juu ambapo siku hizi jamii na viongozi wanatafsiri maendeleo kuwa na vitu kama barabara na majumba.

ìViongozi wakiwa waaminifu na waadilifu kwa wananchi wao ndipo suala la dhana ya maendeleo linatimia mfano utakuwa na utu kwa watu wako na kutojiona mungu mtu katika uongozi wala kutoshiriki kwenye vitendo vya rushwa,îanasema.

Rais mstaafu Mwinyi anaendelea kusema katika hali ya kuenzi mafundisho ya Mwalimu Nyerere, viongozi wanatakiwa kujifunza kuwa na utajiri wa mioyo na utu na si kuwa na matajiri wa vitu na mali.

Anasema wakati umefika kwa jamii kutafakari kiundani kwanini Tanzania imefika hapa na kwamba viongozi wanatakiwa kuacha dhuluma ya kutumia rasilimali za taifa.

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Phillip Mangula, anasema jamii ya Watanzania bado haijashika vizuri mawazo ya Mwalimu Nyerere, hivyo kuna haja ya kuzitafakari fikra zake namna moja ama nyingine.

Mangula anasema katika kipindi cha uongozi wa Baba wa Taifa alifahamu na kuamini kuwa kiongozi mzuri anaandaliwa ili kuwa na misingi ya uadilifu na uzalendo kwa taifa.

ìImani yake hiyo ilimfanya atafute ubunifu wa kutumia Chuo cha Mafunzo Kivukoni ambapo alitumia chuo hicho kuwatengeneza viongozi kujitambua kuwa wao ni watu na si miungu watu, wafanye kazi za kimaendeleo kwa ajili ya watu,îanasema.

Anaendelea kusema, katika kuadhimisha miaka 17 ya Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere lazima viongozi wajifunze kutotumia nafasi zao za uongozi vibaya kwa kujilimbikizia mali ama kushiriki kwenye vitendo vya rushwa.

Makamu Mwenyekiti huyo anasema bado kuna wakati na nafasi ya kufikiria kwa makini fikra na maono aliyoacha Baba wa Taifa ili kufikia maendeleo yanayokusudiwa kwa Tanzania.

“Pia kuzingatia kupatikana kwa viongozi waadilifu ambao wataleta maendeleo kwa ajili ya watu,” anasema.

Kwa upande wake Balozi wa China nchini, Dk.Lu Youqing anasema China inamkumbuka Mwalimu Nyerere kwa mchango wake aliotoa kwa kuhakikisha nchi hiyo inarejesha kiti halali katika Umoja wa Mataifa (UN).

Dk.Youqing anasema jina la Baba wa Taifa linasifiwa sana China kutokana na sifa alizokuwanazo ikiwemo kuaminika na kukubalika na wananchi kutokana na uadilifu wake.

Anasema Mwalimu Nyerere aliongoza Tanganyika katika kupata uhuru na ambapo hakuishia hapo tu na baadae alijenga Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hakuchoka alitafuta njia za maendeleo ya taifa.

“Cha kushangaza licha ya hali halisi ya Tanzania kiuchumi kuwa duni, aliendelea kujitoa kwa moyo wake wote kujenga maisha ya Watanzania kuwa bora na kwamba aliishi maisha ya kawaida yenye uaminifu na uadilifu bila ya kuwa na nyumba ya kifahari, kampuni binafsi wala kuhifadhi fedha kwenye benki za nje,” anafafanua sifa za Mwalimu

Balozi huyo anasema Baba wa Taifa anasifika kuwa ni ìMtakatifu wa Afrikaî anapendwa na kuungwa mkono na wananchi. Ndiye shujaa wa PanAfricanism aliongoza kutoa msaada kwenye vita dhidi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.

Dk.Youqing anafafanua kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa shujaa wa pekee kutokana na mchango wake kwa mataifa mengine ya kujikomboa na utawala wa kikoloni licha ya kuwa taifa lake lina matatizo ya kiuchumi.

Anasema Baba wa Taifa hakuogopa kuwekewa vikwazo kutoka nchi za ukoloni kutokana na msaada wake wa kuziunganisha nchi za Afrika kuwa na umoja wa kujikomboa kisiasa na kimaendeleo ya kiuchumi barani Afrika.

“Mwalimu Nyerere alijitolea maisha yake yote kwa ajili ya Tanzania na Afrika kwa ujumla. Mawazo yake kuhusu uhuru, usawa, ukombozi na umoja wa Afrika ambapo alikuwa na ushawishi” anasema.

Balozi huyo anamalizia kwa kusema kuwa China inamkumbuka sana Mwalimu Nyerere kutokana na uwasisi wake na urafiki wa kudumu na imara kati ya China na Tanzania ambao ulisaidia kuzalisha miradi mingi ya maendeleo ikiwemo kilimo, viwanda na miundombinu.

Naye, Mkurugenzi wa Kavazi cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji, anasema bado fikra za Baba wa Taifa zinaishi hai licha ya yeye kufariki na kwamba ndio misingi ya maendeleo ambayo jamii ya Tanzania inayataka.

Profesa Shivji anaendelea kusema miongoni ya falsafa zake ambazo zinaishi milele na viongozi wanatakiwa kuzingatia dhana ya usawa na haki kuwa binadamu wote ni sawa.

Mwalimu Nyerere alijitolea maisha yake yote kwa ajili ya Tanzania na Afrika kwa ujumla. Mawazo yake kuhusu uhuru, usawa, ukombozi na umoja wa Afrika ambapo alikuwa na ushawishi” anasema.

“Kipimo cha dhana ya usawa ni utu ambapo alihakikisha viongozi wa Chama na serikali kwa ujumla wasiwe wanyonyaj na walipewa masharti magumu ya kuwa na uadilifu,”anaelezea.

Mkurugenzi huyo ambaye ni Mwanazuoni, anasema lazima ifike mahala jamii na viongozi wa vyama na serikali kukubali kutafakari fikra na maono ya Baba wa Taifa ambayo ndio itakuwa muktadha wa maendeleo ya taifa

Anasema masuala yote ambayo Mwalimu Nyerere alikuwa ameyapa kipaumbele kama vile masuala ya uzalendo, maadili na tunu ya taifa kwenye maendeleo ya taifa basi vyama vya siasa vinatakiwa kukaa na kujadiliana kuona namna gani yanatekelezwa.

“Hapa kinachotakiwa ni kuona vyama vya siasa vitashirikiana vipi katika kutengeneza itikadi ambazo zitasaidia kuziba mmomonyoko na ubaguzi wa ukabila na udini ili kwenda sawa na fikra za baba wa taifa na si ukombozi wa siasa chafu,”anasema.

Kwa upande wake, mwasiasa na kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zi o Kabwe, anasema Mwalimu Nyerere aliamini uongozi ni kuwa na miiko ya uongozi hata kama kuna mabadiliko ya mifumo na mazingira.

Zi o anasema Baba wa Taifa alishawahi kusema kuwa hata kama kunatokea mabadiliko ya aina yoyote ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni bado haitaondoa haja ya taifa kuwa na mifumo dhabiti ya kimaadili ya uongozi.

“Viongozi wanapofanya maamuzi yoyote yanapimwa katika mifumo ya maadili ya nchi na kama taifa suala la maadili ni muhimu kuendelea hata kama mabadiliko yanajitokeza lazima twende na misingi ya maadili kama alivyoamini Baba wa Taifa” anafafanua.

Anasema kuwa katika kuenzi fikra za Mwalimu Nyerere viongozi wa vyama na serikali wanapaswa kujifunza katika kukubali na kukiri makosa kwani hiyo ni moja ya misingi ya uadilifu ambayo Baba wa Taifa aliwafunza viongozi katika utawala wake.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.