Tamasha la Fiesta kuiteka Mbeya leo

MZALENDO - - MICHEZO - NA MWANDISHI WETU

TAMASHA la burudani ya Tigo Fiesta linatarajiwa kufanyika leo kwenye Uwanja wa Sokoine, Mjini Mbeya.

Tamasha hilo linashirikisha wasanii mbalimbali ambapo limeshafanyika kwenye mikoa mbalimbali Tanzania Bara.

Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Kampuni ya Prime Time ambao ndio waandaaji wa tamasha la Tigo Fiesta, Joseph Kusaga, alisema kuwa tamasha hilo limekuwa na mwamko mkubwa kutokana na kuwa na lengo la kuibua vipaji vya wasanii mbalimbali.

Alisema kuwa kwa mwaka huu wamekuja kivingine kwani kila mkoa wanaopita wamekuwa wakifanya matamasha ya ngoma za asili ya Tamadunika ili kuibua vipaji vya wasanii mbalimbali.

Alisema kuwa pia tamasha hilo linatumika kuibua wasanii wa muziki wa bongo fleva la Super Nyota ambapo mshindi mmoja wa kila mkoa atapata fursa ya kupanda katika tamasha kubwa litakalofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi huu.

Alisema kuwa kumekuwa na muitikio mkubwa kwani pia wafanyabishara mbalimbali wamekuwa wakiongeza kipato kwa kuuza bidhaa zao kwa wingi.

Aliwataja baadhi ya wasanii watakaopanda jukwaani leo kwenye tamasha hilo kuwa ni pamoja na Jux, Ben Pol, Maua Sama, Chege, Shilole, Baraka da Prince, Man Fongo, Weusi, Msami, Lord Eyes, Quick Rocker, Nandi, Mr Blue na Hamadai.

“Tamasha la mwaka huu linatimiza miaka 15 na pia tumetoa fursa kwa vijana kujiajiri wenyewe ikiwa ni pamoja na kuibua vipaji vya wasanii chipukizi na kuendeleza ngoma za asili,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.