Uganda, Kenya zakumbwa na ukata

MZALENDO - - MICHEZO - NA MWANDISHI WETU

NCHI za Uganda, Kenya na Rwanda zimeshindwa kujitokeza kushiriki michuano ya wavu ya ‘Nyeyere Cup’ inayoendelea kwenye Uwanja wa Hindu Mandal mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro baada ya kukumbwa na ukata.

Michuano hiyo ya wazi ilianza rasmi juzi na kutarajiwa kushirikisha zaidi ya timu 17 lakini kutokana na hali hiyo timu sita tu ndizo zimejitokeza kushiriki.

Akizungumza jana kwa njia ya simu kutoka Moshi, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA) Muhalamu Mchume, alisema kuwa mabingwa watetezi timu ya Magereza kutoka Kenya nao wameshindwa kujitokeza.

“Tunasikitika kwani timu nyingi hazijaja kushiriki, na asilimia kubwa zimekuwa zinalalamikia hali mbaya kiuchumi, kwahiyo hadi sasa (jana) tuna timu sita tu,” alisema.

Mchume aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo timu zitacheza kwa mtindo wa ligi ambapo kila siku zitachezwa mechi sita na baadae kutafuta mshindi wa kwanza hadi wa tatu.

Alizitaja timu zilizojitokeza kuwa ni Jeshi Stars ya Dar es Salaam, Pentagon Arusha, Dodoma ambayo ina timu mbili na Hai na kufanya idadi ya timu sita.

“Licha ya timu chache kujitokeza, mashindano yamechangamka sana kwani mashabiki wamejitokeza kwa wingi hivyo kuzitia moyo timu hizi chache,” alisema.

Michuano hiyo inalenga kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.