Bei ya korosho yapaa

Hii ni kufuru haijawahi kutokea kwa mkulima kupata fedha hizi...

MZALENDO - - MBELE - NA RASHID MUSSA, MTWARA

WAKULIMA mkoani Mtwara wameanza kuuza korosho katika minada iliyofanyika wiki hii kwa bei kubwa ya takribani mara tatu ya ile elekezi ya sh. 1,300 kwa kilo moja.

Kupaa huko kwa bei ya korosho ambako hakujawahi kutokea katika

historia ya zao hili kunaelezwa kuwa kunatokana na bei ya soko la nje kuwa ya juu kufikia dola 2.34 kwa kilo moja

Sababu nyingine inayotajwa ni mfumo mzuri wa uuzaji wa zao hilo wa stakabadhi ghalani ambao huwashindanisha wanunuzi na mwaka huu wakulima wenyewe wakihudhuria minada hiyo.

Kaimu Mkurugezi wa Masoko wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Juma Yusufu, aliithibitishia MZALENDO kuhusu bei hiyo njema kwa mkulima wa korosho na taifa kijumla.

Yusufu alisema katika minada iliyofanyika Wilaya za Masasi, Newala na Mtwara, takribani tani 3,000 ziliuzwa kwa bei ya kati sh. 3,670 na 3,650 kwa kilo moja.

Alisema katika mnada uliyofanyika katika ghala la Mtandi Masasi na

Mtwara, tani 2,400 za korosho ziliuzwa kwa bei ya sh. 3,650 na Newela tani 591 ziliuzwa kwa sh. 3,670.

Kaimu Mkurugezi huyo wa Masoko wa CBT alisema bei hiyo ni kubwa zaidi ukilinganisha na ya mwaka jana ambayo ilikuwa kati ya sh. 2,000 hadi 2,800 kwa kilo moja.

Alisema kwa mujibu wa mjengeko wa bei wa mwaka huu, baada ya serikali kuziondoa toza tano zilizokuwa zinakatwa mwaka jana na kubakia na makato ya sh. 191 tu, wakulima wanatarajia kujipatia

mapato makubwa kwa bei hiyo iliyouzwa katika minada hiyo ya mwanzo ya takribani sh. 3,450 kwa kilo moja.

Wakulima wameipokea bei hiyo ya minada ya mwanzo kwa kuishukuru serikali kwa kuweka mfumo mzuri wa uuzaji wa zao hili na kuusimamia kwa nguvu zote kuhakikisha unafuatwa na wafanyabiashara wote wanaonunua zao hili hapa nchini.

“Hii ni kufuru haijawahi kutokea kwa mkulima kupata fedha hizi,” alisema Hasani Lingwenje wa Mkangala Mtwara.

Mwishoni mwa wiki, Bodi ya Korosho ilitangaza kuanza kwa minada katika mikoa ya Mtwara na Lindi ambapo ilisizitiza na kuonya wafanyabiashara kutokununua korosho nje ya utaratibu uliyowekwa wa stakabadhi ghalani.

Kaimu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Mudhihir M. Midhihir, alisema atakayekamatwa akinunua korosho nje ya mfumo huo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kutaifisha korosho zote

zilizokamatwa na vyombo vilivyotumika kusafirishia iwe gari, pikipiki hata baiskeli.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.