Samia: Wafichueni wanaofuja fedha

MZALENDO - - MBELE -

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi kuwafichua watumishi wa halmashauri na taasisi za serikali katika wilaya na mikoa wanaodhaniwa kufuja fedha na kupoteza mapato.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuzikusanya fedha na kuzirudisha katika mikono ya wananchi waone faida yake.

Pia, Makamu wa Rais, Samia alisema Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea na nguvu yake ya kukusanya mapato na kuziba mianya ya rushwa na kupotea kwa mapato.

Alitoa rai kwa wananchi mkoani Pwani kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kulinda amani na usalama wa mkoa huo kufuatia kujitokeza kwa mambo ambayo yameonekana kuhatarisha usalama hivi karibuni.

Katika hatua nyingine, Samia aliwahakikishia wakazi wa mji wa Chalinze kutatua tatizo la maji ambalo bado ni kero kubwa na kuwa mwishoni mwa mwaka huu matunda yataanza kuonekana.

Akizungumza na baadhi ya wananchi wa Mlandizi na Chalinze, mkoani Pwani wakati aliposimama kuwasalimia akienda Dodoma kikazi, alisema wananchi waiamini serikali yao kwani imeanza kuirejesha nchi katika nidhamu ya mapato na matumizi na kazi ya maendeleo inaendelea.

ìWatanzania watajenga Tanzania yao wenyewe na serikali yake na Tanzania inaweza kujiendesha yenyewe na kama itategemea misaada iwe si kwa kiasi kikubwa. îalisema.

Aliwasisitiza wananchi kulipa kodi pale inapohitajika ili kusaidia na serikali kuinua mapato yake.

Hata hivyo, Samia aliwataka wakulima na wafugaji kuishi kwa upendo na mshikamano baina yao pasipo kutofautiana kwani kwa kufanya hivyo kunasababisha migogoro isiyo na tija na wakati mwingine kuvunja amani.

Kufuatia ombi la mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, aliyemueleza makamu wa rais kuhusu kero ya maji inayowakabili wakazi wa jimbo hilo, Samia alisema serikali inatambua hilo na kwa sasa ipo katika mpango mzuri wa kumaliza tatizo la maji lililopo.

Alielezea kuwa Wami yapo maji ya kutosha, lakini tatizo ni usambazaji, hivyo wanatarajia kuvuta maji kwa mabomba hadi eneo la Pera na kujenga matanki makubwa ili maji yakifungwa yaweze kufika kwa wananchi kirahisi.

Makamu huyo wa rais alisema watajenga hifadhi nyingine ya maji Mazizi yenye lita za ujazo milioni 1.2 ambayo itawezesha kutumia maji ndani ya wiki mbili bila kukatika.

Makamu wa Rais Samia wakati anafanya kampeni ili kuomba kuchaguliwa kuingia madarakani aliahidi kuwatua kina mama ndoo kichwani kwa kutatua tatizo la maji na kusema anashughulikia suala hilo hadi hapo atakapowaondolea wananachi adha ya kutembea umbali mrefu kusaka huduma hiyo muhimu.

Akizungumzia suala la afya kuhusu vifaa tiba, alisema atazungumza na wizara husika kutatua kero ya vifaa tiba, dawa na watumishi katika Kituo cha Afya Msoga ili kupunguza mzigo kwa hospitali za rufani ikiwemo Tumbi.

Alisema tatizo la watumishi karibu litamalizika na kuwa kulikuwa na idadi kubwa ya watumishi hewa, hivyo hivi karibuni watafungua ajira mpya baada ya zoezi hilo kukamilika.

Samia aliipongeza Chalinze kumaliza tatizo la madawati ila alisema kwenye mafanikio kunajitokeza tatizo jingine hasa kutokana na idadi ya wanafunzi imekuwa kubwa na kuzalisha tatizo la madarasa .

Aliwataka viongozi wa wilaya na mkoa kuelekeza

nguvu zao kujenga, kuongeza na kukarabati majengo ya madarasa ili watoto waweze kusoma .

Akiwa Mlandizi, Makamu wa Rais aliahidi kuweka uzio kama alivyoahidi wakati wa kampeni kwenye uchaguzi uliopita katika Kituo cha Afya Mlandizi kwani ni moja ya sifa ya kupandishwa kwa kituo cha afya kupanda hadhi ya wilaya na bado wanania ya kupandisha hadhi ya vituo mbalimbali.

Alisema soko la mlandizi bado ni dogo ila ana taarifa kuwa kwenye eneo la Kisabi A na B kuna maeneo yamepimwa kwa ajili ya masoko na TAMISEMI wameweka mkono kidogo na kuwahakikishia kuwa atakaa nao kuangalia uwezekeno wa kuachia maeneo hayo ili kuwepo na soko na stendi kubwa .

Kuhusu kupimwa mji wa Mlandizi, Samia alisema ataongea na Wizara ya Ardhi ambao wamekuwa wepesi kufanya upimaji, hivyo ataweka msukumo ili waweze kupimiwa na barabara ya Mlandizi-Mzenga ahadi ipo palepale itajengwa kwa kiwango cha lami .

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, akimfariji mjane wa aliyewahi kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, marehemu Dk. Didas Masaburi, Zurfa Masaburi, nyumbani kwa marehemu, Chanika, Dar es Salaam, juzi. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, akipokea mfano wa hundi ya sh.620,000 kutoka kwa Mtandao wa Wasanii Tanzania (SHIWATA), Dar es Salaam, juzi. kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.