SIMBA MWENDO MDUNDO

nYailaza Kagera Sugar, Kichuya noma

MZALENDO - - MBELE - NA VICTOR MKUMBO

SIMBA ya jijini Dar es Salaam, jana imeonyesha dhamira ya kutwaa ubingwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania bara baada ya kuifunga Kagera Sugar mabao 2-0.

Mchezo huo ulioanza kwa kasi, ulichezwa uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Tangu dakika ya kwanza, pambano hilo lilionekana kuwa na kasi ya aina yake ambapo Kagera Sugar nusura wajifunge baada ya beki wake, Mwaita Gereza kurudisha mpira wa nguvu kwa kipa Hussein Shariff.

Kipa huyo aliupangua ikawa kona, lakini haikuzaa bao. Dakika 14, Ibrahim Ajib naye alijaribu kupiga shuti lililotoka nje ya lango la Kagera Sugar.

Dakika nne baadae, Fredrick Blagnon alitaka kujaribu bahati yake kufunga kwa kichwa kufuatia kona iliyochongwa na Mohammed Hussein.

Pamoja na mashambulizi hayo ya kila upande, washambuliaji wa timu zote walionyesha nidhamu ya hali ya juu uwanjani.

Christopher Edward, mchezaji wa zamani wa Simba ambaye sasa anaichezea Kagera Sugar, alijaribu dakika ya 31, lakini shuti lake halikuwa na macho.

Hata hivyo, iliwalazimu Simba kusubiri mpaka dakika ya 43 kuandika bao la kuongoza lililowekwa kimiani na Mzamiru Yassin ambaye alifunga kwa kichwa.

Mfungaji huyo, aliuwahi mpira kabla haujadakwa na kipa wa Kagera Sugar baada ya Shiza Kichuya kuchonga kona maridhawa.

Baada ya mapumziko ambayo Simba walikuwa mbele kwa bao hilo, kasi ya ushindani kwa pande zote iliongezeka.

Simba wakitaka kuongeza bao huku, Kagera Sugar chini ya kocha wake, Mecky Mexime wakihaha kutafuta namna ya kusawazisha.

Ili kuongeza nguvu, Kagera Sugar waliwapumzisha Edward na Danny Mrwanda nafasi zao zikajazwa na Paul Ngwai na Themi Felix huku Simba nao wakiwatoa Blagnon na Ibrahim Ajib nafasi zao zikizibwa na Mohammed Ibrahim na Laudit Mavugo.

Mabadiliko hayo, yaliongeza kasi ya mchezo na dakika ya 64, Mavugo alipata nafasi nzuri ya kufunga, guu lake halikulenga lango.

Alikuwa ni Kichuya aliyekwamisha wavuni bao la ushindi kwa mkwaju wa penati dakika ya 75. Penati hiyo ilitokana na beki wa Kagera Sugar, Juma Ramadhan kumfanyia madhambi Ibrahim.

Katika kuimarisha zaidi eneo la kiungo, kocha wa Simba Joseph Omog, alilazimika kumtoa Mwinyi Kazimoto na kumuingiza Said Ndemla.

Lakini mpaka filimbi ya mwisho, Simba ilitoka kifua mbele kwa ushindi huo wa mabao 2-0.

Ligi hiyo inaendelea tena leo kwenye uwanja wa Uhuru ambapo Yanga itavaana na Azam FC, zote za jijini Dar es Salaam.

MZAMIRU Yassin wa Simba (kushoto), akimtoka George Kavila wa Mtibwa Sugar katika mchuano wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, jana. Mtibwa ilinyukwa 2- 0. (Na Mpigapicha Wetu).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.