UBORA MAGARI YA UTALII:

Mamlaka husika zinapaswa kuweka mambo hadharani

MZALENDO - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

WAKATI sekta ya utalii ikiwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato ya serikali, migogoro miongoni mwa wadau wa sekta hiyo huenda ikasababisha kuyumba kwake.

Utalii unachangia zaidi ya asilimia 10 ya pato la taifa kwa mwaka huku sehemu kubwa ya pato hilo ikitoka katika sekta ndogo ya utalii wa wanyama pori hasa katika hifadhi za taifa.

Hakuna ubishi kuwa miundombinu duni imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha kukua kwa utalii hapa nchini.

Ni ukweli uliowazi kuwa watalii uhitaji magari imara yenye uwezo ya kubeba familia nzima au kundi la watalii kati ya watano hadi saba kwa wakati mmoja.

Ni kutokana na hilo ndio maana wadau wa utalii huwaandalia wateja wao magari maalum yenye uwezo wa kuhimili mikiki mikiki ya safari za porini.

Kwa uwezo wa magari haya ambayo hubeba abiria saba na mizigo yao, huku ikiwawekea watalii mazingira rafiki ya kuweza kuwaona wanyama na hata kupiga picha, yameweza kupata umaarufu hadi yakapewa jina la ëWar Busí.

Magari haya ambayo asili yake (injini na mitambo mingine) ni Toyota, huwekewa bodi lililoundwa maalum kuweza kubeba idadi hiyo ya watu kwa mara moja, huku ikibakiza nafasi kubwa kati ya viti na kulifanya gari kuwa refu zaidi ya Toyota ëasiliaí.

Magari yenye bodi kama hizo ni maarufu sana kwa wakazi wa maeneo ya karibu na hifadhi za taifa kwa miaka mingi sasa.

YALITOKEA WAPI?

Ingawa wengi wanaweza kudhani kuwa magari hayo yapo nchini miaka mingi, ukweli ni kwamba mfumo huo wa ‘war bus’ ulianza kuundwa takriban miaka 12 iliyopita yaani mwaka 2004.

“Tulidhani kama Watanzania tunapaswa kuchangia kukua kwa sekta ya utalii kwa kuwapa watalii nyenzo bora za kuwasafirisha salama ndani na nje ya mbuga zetu,”anasema Manmohan Bhamra ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya RSA Limited ya Moshi inayoshughulika na utengenezaji wa mabodi hayo tangu mwaka 2004.

Bhamra alisema RSA ndio waliobuni aina hii ya mabodi kwa ajili ya watalii na kupata umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi.

Kwa kutambua umuhimu na faida ya ubunifu huo, RSA, waliowekeza fedha za kutosha katika kubuni mchoro thabiti (industrial design) ya mabodi hayo ya ‘war bus’ kuendana na mahitaji ya sekta ya utalii na , kusajili ubunifu huo kwenye taasisi ya kimatiafa ya ARIPO, Aprili 25, i 2005 ambapo ilipewa jina la ‘RSA Special Vehicle Optimum Body Booster System’.

ARIPO au (African Regional Intellectual Property Organization) ni taasisi ya Afrika inayoshugulika na usajili wa kazi za ubunifu na kulinda haki ya umiliki wa kazi hizo.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia kujiunga na kutambua kazi za ARIPO, hivyo kazi zote zilizosajiliwa na taasisi hiyo, pia zinatambulika Tanzania.

“Kwa kawaida watalii wote kipaumbele chao kikuu ni usalama. Hata nchi wanakotoka wanasisitiza usalama kwanza. Sasa suala la amani kwa Tanzania halina shida, lakini je, usalama wao wawapo safarini ukoje? Ndio maana katika kubuni mabodi haya tulizingatia vigezo vyote vinavyokidhi uimara na uthabiti wa mabodi yetu,î anasema Bhamra.

Usalama ni kigezo muhimu ambacho kikiimarishwa kitachangia na kuipaisha Tanzania kwenye utalii Afrika ikizingatiwa kwamba kwa mujibu wa taarifa ya ëThe 2015 Global Travel and Tourismí taifa letu lipo katika nafasi ya 93 duniani miongoni mwa mataifa yanapokea watalii wengi. Kenya ni ya 78 na Afrika Kusini ya 48.

Tanzania inakuwa ya tatu nyuma ya Afrika Kusini na Kenya ingawa hapa kuna vivutio vingi zaidi vya utalii na maeneo mengi ya urithi wa dunia yanayotambuliwa na UNESCO.

Lakini yapo maswali kadhaa ya kujiuliza kama; Iwapo usalama wa watalii ukitetereka nchini hali itakuwaje? Je, magari yanayobeba watalii yana ubora unaotakiwa? Nani ameyaidhinisha na kuyapasisha magari hayo kuweza kuchukua jukumu zito kama hili kwa uchumi wa Tanzania la kubeba watalii?

Ni nani atakayewajibika iwapo uduni katika ubora wa magari haya utasababisha Tanzania kutoaminika miongoni mwa mataifa yanayoleta nchini watalii?

Maswali haya yanatokana na taarifa za hivi karibuni kwenye vyombo vya habari zinazogonganisha kampuni mbili; RSA ya Moshi na Hanspaul Automechs Limited (HAL) ya Arusha.

RSA inadai kwa ushahidi kuwa ubunifu wa mabodi hayo iliyousajili ARIPO mwaka 2005 unatumiwa na HAL bila makubaliano yoyote ya msingi.

Taarifa zilizopo ni zinaonyesha mwaka 2007 HAL ilianza kutengeneza ‘war bus’ sawa sawa na zile za RSA kwa kila kitu bila kufuata sheria zozote za kitaifa au kimataifa.

Moja ya sheria hizo ni kuwasilisha mchoro wa ubunifu (industrial drawings/industrial designs) serikalini kabla ya kupewa leseni ya uzalishaji kitu ambacho kilishafanywa na RSA tangu mwaka 2004.

Huenda ni kwa kulitambua hilo ndio maana HAL ilianza kutengeneza magari hayo kinyemela tangu mwaka 2007 hadi Januari, mwaka huu ndipo walipoomba na kupewa leseni ya muda ya uzalishaji..

Ni wazi kuwa kwa muda wote huu (kabla na hata baada ya HAL kupewa leseni ya muda) haki ya RSA ilichezewa kama si kudhulumiwa na taasisi za serikali zenye wajibu

wa kuratibu na kusimamia biashara kwa uhuru na haki.

NANI ALAUMIWE?

Kwa namna yoyote taasisi kama Tume ya Ushindani wa Biashara (FCC) haiwezi kukwepa lawama kwa kuwa kwa mujibu wa sheria ya kuanzishwa kwake (FCA No. 8 of 2003), moja ya majukumu yake ni kulinda ushindani katika biashara huku ikiwalinda walaji (watumiaji).

Kwenye mgongano kati ya RSA na HAL, FCC hawakuonekana kulinda haki ya kampuni yoyote kati ya hizi wala kuwalinda watumiaji (watalii) wa mabodi hayo.

Hiyo inatokana na ukweli kuwa wakati RSA imekuwa ikifahamika kitaifa na kimataifa kama watengenezaji halisi wa mabodi hayo, HAL walikuwa wakiyatengeneza na kuyauza ndani na nje ya nchi bila kibali; kwa kuzingatia ubora wao wenyewe, hivyo kuhatarisha soko la RSA na watalii wenyewe.

Lengo jingine la kuanzishwa kwa FCC ni kuongeza ufanisi katika uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma, lakini hali hiyo ni tofauti kwenye mabodi ya magari hayo ya watalii.

Taasisi nyingine nyeti ambayo ilipaswa kuweka sawa mbambo katika mgongano huo ni Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambayo ina jukumu la kusimamia ubora wa bidhaa zinazotumika Tanzania.

Hata hivyo, katika suala la mabodi ya ‘war bus’ TBS imekuwa ikikwepa majukumu yake ma kushindwa kutoa msimamo licha ya kutambua kuwa magari yanayotumika ambayo yana viwango vya kimataifa (USO) hupachikwa mabodi mapya.

TBS imekuwa kimya kwenye suala la mabodi ya magari ya utalii ambayo utengenezaji wake hauna tofauti na suala la malori kutengenezwa mabodi ya mabasi na kisha kutoa huduma ya kubeba abiria.

Pia, TBS imekuwa kimya licha ya kutoa leseni kwa RSA na imekuwa ikilipwa fedha za leseni kwa miaka kadhaa sasa.

TBS wanapaswa wawaeleze Watanzania kama hawahusika na ubora wa mabodi yanayotengenezwa nchini kwa ajili ya matrela na mabasi ya abiria kisha kupachikwa kwenye Scania au magari mengine makubwa.

Katika mabodi ya magari ya utalii kuna tofauti gani na oparesheni iliyofanya TBS miaka kadhaa iliyopita kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kusaka mabodi ya mabasi yaliyopachikwa kwenye magari aina ya Fuso?

Iwapo suala la mabodi ya magari ya watalii halitachukuliwa kwa umakini na kufuata taratibu stahiki kuna uwezekano wa kuja kuyumbisha sekta ya utalii nchini.

MKURUGENZI Mkuu wa Kampuni ya RSA Limited ya Moshi, Manmohan Bhamra, akifafanua jambo kwa baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari.

MKURUGENZI Mkuu wa Kampuni ya RSA Limited ya Moshi, Manmohan Bhamra, akifafanua jambo kwa baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari.

MOJA ya mabodi yanayo tengenezwa na kampuni ya RSA.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.