YASMIN ALOO

Kada wa CCM Zanzibar anayemtaja Mwalimu Nyerere kama muasisi aliyepigana na Mzee Karume kuulinda Muungano

MZALENDO - - MAKALA - NA MWANDISHI WETU

WATANZANIA wametimiza miaka 17 bila ya uwepo wa baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyyerere aliyefariki dunia Oktoba 14, mwaka 1999 baada ya kuliongoza taifa kwa muda mrefu na hatimaye kustaafu.

Kazi kubwa iliyofanywa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, imeendelea kuwa mfano bora na mzuri kwa miaka mingi wakati wa harakati za kupigania uhuru na baadae kuwa na Tanganyika huru na baadae Tanzania.

Mengi na makubwa yaliyofanywa na Hayati Mwalimu Nyerere kwa kushirikiana na viongozi wenzake akiwemo muasisi mwenza wa Tanzania, Rais wa kwanza wa Zanzibar na kiongozi wa Mapinduzi, Hayati Mzee Abeid Amani Karume, yanaendelea kukumbukwa na kuwafanya Watanzania na Waafrika wote kuendelea kutambua mchango wao na kuona uwepo wao ulihitajika zaidi hivi sasa kuliko wakati mwingine.

Moja ya mambo makubwa aliyohusika kuyaasisi na kuyasimamia ni pamoja na muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania ya sasa, ambayo wananchi wa maeneo yote wanaishi kwa amani na upendo.

Kwa kushirikiana na Sheikh Karume, Mwalimu Nyerere aliunda muungano huo ambao hadi sasa umeendelea kuwa nguzo imara na kimbilio la maendeleo kwa Watanzania wote.

Mbali na muungano, Mwalimu Nyerere aliwaongoza wenzake kuunda umoja wa kitaifa, mshikamano, upendo na uzalendo wa kweli ambao hivi sasa umekuwa wa kupigiwa mfano na kuwavuta watu kutoka pande mbalimbali za dunia kuja kujifunza kwa Tanzania.

Wakati Tanzania ikiadhimisha miaka 17 ya kifo cha Mwalimu, wengi wamejitokeza kueeleza namna Mwalimu Nyerere alivyokuwa imara na alivyoweza kusimamia maadili na uongozi uliotukuka.

Miongoni mwa waliojitokeza kumueleza Hayati Mwalimu Nyerere ni pamoja na Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), visiwani Zanzibar, Yasmin Aloo, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha muungano wa Zanzibar unalindwa kwa nguvu zote.

Yasmin aliyewahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya Chama ikiwemo na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuia ya Wazazi ya CCM (Zanzibar), anasema Mwalimu ataendelea kukumbukwa wakati wote kwa kuwa amefanya mengi ya maendeleo yatakayokuwa ni ya kujivunia kizazi hadi kizazi cha Watanzania.

Moja ya mambo anayoyaeleza Yasmin kwamba yataendelea kukumbukwa ni pamoja na ujasiri, uthubutu, uzalendo na ueledi aliokuwa nao Mwalimu uliowavutia viongozi kutoka pande mbalimbali za dunia na kuifanya Tanzania kuwa kituo muhimu cha harakati za ukombozi wa bara la Afrika.

Anasema chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere, ndipo harakati za ukombozi kwa bara la Afrika ziliposhika kasi na kwa kiasi kikubwa zilifanikiwa kwa kuwa nchi zote zilipata uhuru na bara hilo kuwa huru.

Mbali na harakati hizo, Yasmin anasema Mwalimu atakumbukwa zaidi na Wazanzibari kwa namna alivyoweza kuimarisha umoja wa kindugu uliokuwepo kwa muda mrefu na kuwafanya Watanganyika na Wazanzibari kuwa kitu kimoja kinachoonekana sasa na kusema hilo si jambo dogo.

Kwa mujibu wa Yasmin, Mwalimu kwa kushirikiana na Mzee Karume, waliasisi maendeleo ya kweli yaliyowahusu waafrika wanyonge ikiwemo kuanzishwa kwa viwanda vilivyotoa ajira kwa watu wa hali ya chini, kuondoa matabaka kwenye jamii, kujenga makazi bora yaliyotolewa kwa wananchi jambo ambalo halikuwa raisi chini ya utawala wa kikoloni.

Aidha, Yasmin anasema Mwalimu Nyerere ndiye aliyetengeneza misingi ya taifa iliyofanikisha kuwa na mfumo mzuri wa kupata viongozi bora ambapo leo hii Tanzania inashuhudiwa ikiwa kwenye Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli anayetajwa kufuata nyayo zake kwa asilimia kubwa.

“Mwalimu ndiye aliyeongoza utaratibu wa kuwapata viongozi. Wakati Tanzania ikipata sifa kubwa kwa kudumisha amani, umoja na mshikamano, Mwalimu Nyerere anapaswa kupwewa sifa zaidi kwa kuwa yeye ndiye aliyeongoza yote hayo.

“Mwalimu aliweza kuka mikakati na kujenga dhana ya demokrasia na kuachiana nafasi za uongozi. Tumekuwa tukishuhudia sehemu mbalimbali viongozi waking’ang’ania madaraka na kuendelea kutawala miaka na miaka jambo ambalo halipo hapa kwetu. Sifa nyingi zimuendee Mwalimu Nyerere,”alisema.

AMTAJA JPM KUWA MRITHI WA NYERERE

Yasmin anasema tangu Mwalimu ang’atuke na kujiweka kando na uongozi wa nchi Tanzania imeendelea kuendeshwa katika mstari imara hadi sasa zikiwa zimepita awamu nne.

Hata hivyo, anasema katika awamu zote hizo, awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ingawa bado ni muda mfupi tangu ilipoingia madarakani lakini ina viashiria vya kulandana na uongozi wa mwalimu Nyerere.

Anasema mambo yaliyofanywa na Dk. Magufuli katika muda huo mfyupi yamelenga kuwapa haki wanyonge, wanaodhulumiwa na masikini ambao kwa muda mrefu walikuwa wakikosa haki kutokana na tamaa za watu wachache.

Anasema anaamini Tanzania chini ya Rais Dk. Magufuli itafanya mambo makubwa na ya kupigiwa mfano itafanikiwa kuivusha nchi kuwa ya uchumi wa kati ifikapo 025 kwa yanayofanyika sasa haitakuwa ngumu kufikia huko.

ATAKA MUUNGANO UDUMU

Kwa upande wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Yasmin anasema ndio muhimu wa kila maendeleo yanayoweza kufikiwa na Watanzanuia.

“Bila ya muungano huu huenda hivi sasa tusingekuwa tunazungumzia hapa tulipofika. Umoja wetu, uimara na mafanikio tuliyonayo sasa yanatokana na umoja huo. Tusikamane, tuelekezane na tuzipatie ufumbuzi wa haraka kasoro zinzoibuka ili kuwa muungano imara zaidi kwa ajili ya maendeleo ya Watanmzania,”anasema.

Akimueklezea Rais Dk. Ali Mohamed Shein anasema anaifananisha awamu hii ya tano na ile ya kwanza iliyokuwa ikundwa na Rais Karume na Nyerere kwa kuwa zinafanana kwa hali mbalimbali.

“Uimara na ushupavu wa Magufuli na Shein unalandana na ule wa Nyerere na Karume. Naamini makubwa yatafikiwa chini ya hawa,”alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.