WENGER

Mashabiki wazidi kumkaba koo

MZALENDO - - JILIWAZE -

Wamtaka afungashe virago, aondoke Mwenyewe asema mashabiki wana haki

BAADHI ya mashabiki wa soka huwa na msemo kwamba, ukitaka presha katika soka ya England, basi uishabikie Arsenal.

Timu hiyo kwa miaka mingi, imekuwa na kiu ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na mashindano mbalimbali.

Mengi yanazungumzwa kuwa ndiyo chanzo cha kutopata mafanikio.

Kubwa kuliko yote ni kasumba ya kocha wa timu hiyo Arsene Wenger raia wa Ufaransa kutokuwa na kawaida ya kununua wachezaji mahiri.

Mashabiki wa Arsenal wanalalamika kila msimu kwamba Wenger hupendelea kusajili wachezaji ‘choka mbaya’ ambao hawana ubavu wa kuipa timu mafanikio.

Misimu kadhaa Arsenal huanza vyema mechi zake za Ligi Kuu ya England, lakini baadae hushindwa kufikia malengo ya kutwaa ubingwa.

Hali hiyo inawaumiza sana mashabiki wa Arsenal. Kombe wamekuwa wakilishuhudia likinyakuliwa na klabu zingine kama Man United, Man City na Chelsea.

Msimu wa uliopita ndiyo uliwaumiza zaidi mashabiki wa Arsenal, licha ya timu yao kuwemo kwenye mbio za ubingwa, lakini Leicester City iliushangaza ulimwengu ilipoibuka bingwa wa michuano hiyo.

Mara nyingi mashabiki wamekuwa wakipaza sauti kwa kutaka Wenger kuacha ubahili, avunje benki na kusajili wachezaji nyota duniani kama zinavyofanya klabu zingine ambazo baada ya msimu, zinapata mafanikio.

Aidha, wengine wanaamini hatua ya kukaa muda mrefu akiifundisha klabu hiyo, huenda ikawa sababu na sasa mabadilko yanahitajika ili kupiga hatua inayostahili.

Wenger ndiye kocha pekee England aliyedumu kwa muda mrefu baada ya Sir Alex Ferguson kustaafu kufundisha soka.

Hivi karibuni, Wenger aliadhimisha miaka 20 akiwa Arsenal, hivyo mashabiki wanaamini umefika wakati kwake kupisha kocha mwingine aweze kuleta changamoto mpya kwenye klabu hiyo.

Pamoja na malalamiko hayo ya mashabiki, Wenger amefananisha fikra hasi hizo zinazoelekezwa kwake kwa kasi kama virusi.

Amesema mashabiki walipaza sauti zaidi wakati Arsenal ilipocheza dhidi ya Swansea kwenye uwanja wa Emirates, Machi mwaka jana.

Amesema kucheza dhidi ya timu yenye kiwango cha chini, upepo ulibadilika hasa baada ya wapinzani wao kusawazisha

Baada ya kusawazisha, dakika ya 74 Ashley Williams aliwanyima raha mashabiki wa Arsenal ambao walitoka uwanjani wakiwa vichwa chini.

“Naweza kusema kwamba kasoro husambaa kwa kasi, ni kama virusi ambavyo husafiri haraka,” amesema Wenger huku akiikumbuka siku hiyo.

Wenger ambaye alikuwa na tabasamu wakati akizungumza hayo, amesema anafahamu mambo ni magumu kwa sasa.

Wenger anasema: “Arsenal tumepoteza mara moja katika msimu huu ambao ni mchezo wa ufunguzi dhidi ya Liverpool. Tano tumeshinda.”

Mfaransa huyo amesema kufungwa na Swansea, ni sababu dhaifu sana kwa mwenendo wa Arsenal msimu uliopita.

“Tuliharibu nafasi zetu. Tulisemwa sana baada ya mchezo dhidi ya To enham,” anasema Wenger baada ya kutoka sare na wapinzani hao.

Lakini, katika mchezo huo,Wenger alikisifu kikosi chake kucheza kwa kiwango bora kwani kilikuwa nyuma na hatimaye kumaliza dakika 90 kwa sare ya 2-2.

Hata hivyo kwa muda mrefu, Wenger amekuwa na wakati mgumu kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo kwa miongo miwili aliyodumu.

Miaka miwili iliyopita, Wenger aliwahi kuingia katika mzozo wa maneno katika kituo kimoja cha stesheni baada ya mashabiki kumzonga, Arsenal ilipofungwa 3-2.

Kimsingi, mashabiki wenyewe wamegawanyika. Kuna wenye mabango ambayo wanayashika mara kadhaa yakiwa na ujumbe wa kutaka Wenger ang’oke.

Lakini, wapo mashabiki wengine wangependa kumuona kocha huyo akiendelea na kibarua chake.

“Naamini kwa kipindi cha sasa, tuiangalie timu kwa mtazamo chanya,” amesema Wenger.

Akaongeza: “Tuko karibu na timu zilizo kileleni katika msimamo wa ligi kuu. Tunapaswa kuendelea kuweza kufika hatua nyingine. Lazima tutengeneza mazingira rafiki ya kufakikisha tunafanya vyema.

‘Tunahitaji kucheza kwa mafanikio. Mengine tunapaswa kuyapuuza. Hebu tuangalie namna tunavyofanya na jinsi tunavyocheza.

“Tunapaswa kuangalia ambacho ni muhimu. Namna timu inavyocheza na mashabiki wanavyojenga fikra dhidi ya kocha, kuna tofauti kubwa.

“Mashabiki ni sehemu ya mchezo wetu, wana uhakika na haki ya kuhitaji kuwa na furaha. Kazi yangu ni kuangalia nini nafanya kwa mujibu wa kanuni zangu za kazi. Najitahidi kuwafanya mashabiki wafurahi.”

MASHABIKI wakiwa na bango linaloonyesha kuchoshwa na Arsene Wenger. Arsenal jana ilicheza na Swansea

WACHEZAJI wa Arsenal wakijifua juzi

MASHABIKI wa Arsenal, wakiwa na bango lenye kumtaka Arsene Wenger kufungasha virago

WACHEZAJI wa Arsenal wakifanya mazoezi kabla ya mchezo wao dhidi ya Swansea

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.