Pori Tengefu Loliondo lishushwe daraja (I)

Rai - - MAKALA -

LENGO la makala haya yenye sehemu mbili ni kuitaarifu Serikali, wadau wa uhifadhi na Watanzania kuhusu hali ya sasa ya Pori Tengefu Loliondo (LGCA).

Ndani ya eneo hilo nyeti kwa mustakabali wa uhifadhi nchini kunafanyika uharibifu wa kutisha kwenye makazi ya asili, mazalia na njia za wanyamapori.

Kutokana na uharibifu mkubwa na uvamizi unaofanywa na binadamu, wanyama wa jamii ya simba, nyati na wengineo wametoweka au huonekana kwa nadra sana.

Wanyama hawa wamejikuta wakilazimika kuhama kwa kukosa chakula, maji pamoja na mazingira yao ya asili kugeuzwa malisho ya mifugo, makazi na mashamba ambayo sasa yanalimwa kwa kutumia matrekta.

Ni kutokana na ukweli huu usio na shaka yoyote, zisipochukuliwa hatua za dharura na Wizara ya Maliasili na Utalii, kuna hatari ya kupoteza kabisa rasilimali ya wanyamapori katika eneo hilo muda mfupi ujao.

Loliondo ilianza kusikika masikioni mwa Watanzania mwanzoni mwa miaka ya 1990, baada ya mwekezaji kampuni ya Otterlo Business Corporation (OBC) kupewa kibali cha kufanya utalii wa uwindaji na ule wa picha.

Mbali ya shughuli za uwindaji, OBC imekuwa ikijihusisha na miradi ya maendeleo na masuala ya uhifadhi kama taratibu na sheria za nchi zinavyoelekeza wawekezaji wote.

Katika miaka ya 1990 wakati shughuli za uwindaji zilipoanza, wanyama wanaopaswa kuwindwa na watalii walikuwapo, lakini hali ilivyo sasa maeneo yaliyokuwa na wanyama hao yamefurika ng’ombe, mbuzi, kondoo na mbwa.

Hivyo kwa ujumla shughuli za uwindaji ambazo zimekuwa zikiipatia Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mabilioni ya shilingi tangu kuwasili kwa mwekezaji huyo, sasa zinaelekea kubaki historia.

Katika kulinda wanyamapori na mazingira ya uhifadhi, Tanzania ilipisha Sheria ya Wanyamapori ya 2009 (Wildlife Management Act, 2009), lakini jambo la kushangaza usimamizi na utekelezaji wa sheria hiyo Loliondo umekwama kabisa.

Kutokana na udhaifu huu mkubwa ambao unajulikana vizuri serikalini, shughuli za kibinadamu zimeacha ziendelee na kuua uhifadhi Loliondo.

Kutokana na ukweli huu, Serikali kushindwa kusimamia sheria imekuwa changamoto kubwa dhidi ya shughuli za uwindaji na uhifadhi kwa ujumla, kwa sababu popote pale duniani, shughuli za kibinadamu ni lazima zisimamiwe na kuratibiwa na sheria.

Mbali ya udhaifu katika kusimamia sheria, katika ngazi ya wilaya hakuna kabisa mpango au mipango ya kusimamia na kulinda uhifadhi, badala yake mifugo imeshika hatamu katika maeneo ya uhifadhi.

Matokeo yake ni shughuli za utalii kukabiliwa na changamoto nyingi, lakini baya zaidi kama ilivyobainishwa awali ni kutoweka kabisa kwa hazina ya wanyamapori.

Mkakati maalumu na wa dharura unapaswa kufanywa sasa sio tu kuokoa Loliondo, lakini kuokoa maeneo muhimu ya uhifadhi yanayotegemeana kama Hifadhi ya Serengeti na Mamlaka ya Bonde la Ngorongoro.

Kwa mujibu wa inayotambuliwa na ya Wanyamapori

kabisa ramani

Idara (Wildlife Division), Pori Tengefu Loliondo lina ukubwa wa kilometa za mraba 6,188. Kwa mujibu wa sheria, eneo lote hilo ni kitalu cha uwindaji.

Hata hivyo, ukubwa huo unajumuisha eneo lote la Loliondo yakiwamo Makao Makuu ya Wilaya, miji midogo kama Waso, Loliondo na vijiji vya Soit Sambu, Ololosokwan, Malambo, Piyaya na vinginevyo.

Pamoja na kilometa hizo 6,188 kujumuisha miji na vijiji, mwekezaji OBC amekuwa akilipa ada ya uwindaji inayolingana na ukubwa wa eneo, jambo ambalo halileti mantiki wala uhalisia.

Pamoja na changamoto zilizopo, ni wakati muafaka kwa Idara ya Wanyamapori kurejea upya na kuainisha eneo halisi linalotumika kwa uhifadhi na uwindaji. Kwa sababu kwa uhalisi si kilometa za mraba 6,188.

Janga la mifugo si tatizo pekee katika eneo hilo, lakini shughuli za kilimo nazo zinakuwa kwa kasi ya ajabu, shughuli ambazo ni tishio kubwa kwa uhifadhi na shughuli za uwindaji.

Kilimo kwa ajili ya mazao ya chakula kinapunguza kwa kasi maeneo ya malisho ya wanyamapori, makazi, mazalia na njia zao (shoroba). Kutokana na uharibifu huo, wanyamapori wanapotea kwa kasi ya ajabu.

Awali, shughuli za kilimo zilikuwa zikifanyika kwenye maeneo ya vijiji, wakati maeneo ya kitalu yaliachwa kwa ajili ya uwindaji, lakini sasa kilimo kimesambaa kila sehemu mpaka kwenye vilindi vya maeneo ya uwindaji.

Mathalan, eneo la Karkamoru ambako ni kilometa 3 kutoka kambi ya mwekezaji inayoitwa LIMA II, kuna mashamba mengi. Jambo lililo dhahiri hapa ni kuwa pindi linapoonekana boma moja au mawili (nyumba za asili za Wamasai), muda mchache baadae utakuta shamba au mashamba.

Kama ufugaji utaendelea kwenda sambamba na kilimo, si wanyamapori pekee watakaopotea, bali hata mifugo itakwisha mbele ya safari, ili kutoa fursa kwa kilimo kama njia mbadala ya kiuchumi.

Mifugo ipo kila kona ya Loliondo, na inaharibu mno mazingira na malisho ya wanyamapori, hata unapowadia msimu wa uwindaji, unakuta hakuwa wanyamapori.

Hii inatokana na vyanzo vya maji, malisho ya wanyama kuzingirwa na mifugo kipindi chote cha mwaka, jambo ambalo pia ni hatari wakati wa uwindaji, kwa sababu wafugaji au mifugo wanaweza kujeruhiwa au kuuawa wakati uwindaji ukifanyika.

Pamoja na kuwa ni tatizo la muda mrefu, hakuna mpango madhubuti wa kuthibiti makundi makubwa ya mifugo kutoka Kenya yanayoingia Loliondo. Mipaka ipo wazi na watu na mifugo huingia na kutoka kadri ya utashi wao.

Mifugo kutoka Kenya inaongezeka kwa wingi katika eneo ambalo tayari limejaa mifugo, tatizo ambalo linachangiwa na ukosefu wa ardhi kwa ajili ya kuchunga katika nchi hiyo, na kuifanya Tanzania kugeuka sehemu huru ya kuingiza kuingiza mifugo.

Serikali inapaswa kujua idadi ya mifugo ya Tanzania ndani ya Loliondo, na ile iliyotoka Kenya kuingia Loliondo, kwa sababu inafahamika vizuri kabisa, ili utaratibu wa haraka ufanyike kuirudisha ilipotoka.

Na kuwe na maofisa wa kutoka katika eneo la mpaka, ili kuzuia kabisa uingizaji wa mifugo, ambao una athari nyingi kuanzia kwenye mazingira, uhifadhi na zaidi afya za wanyama na binadamu.

Mifugo ikiwa ndani ya sehemu ya pori tengefu la Loliondo

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.