CCM imetoka sebuleni na kurejea chumbani

Rai - - MAKALA - NA MWANDISHI WETU

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefanya mikutano yake ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu wiki iliyopita Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mikutano hiyo ya aina yake kufanyika Ikulu, imeambatana na mabadiliko makubwa ya kimfumo, kiutendaji na kisera katika chama hicho kikongwe Afrika Mashariki.

Haya si mabadiliko ya kwanza, lakini ukiyatafakari utabaini kuwa yalilenga kufifisha yale yaliyofanywa na awamu ya nne iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wa Chama hicho Jakaya Mrisho Kikwete.

Mabadiliko haya mapya chini ya Mwenyekiti mpya Dk. John Pombe Magufuli yamejikita zaidi katika kuunda safu ndogo ya uongozi na mfumo wa utawala wa chama hicho, huku pia yakiakisi kupunguza matumizi ya rasilimali fedha ndani ya chama hicho.

Nini sababu ya mabadiliko haya ya sasa ukizingatia kuwa yaliyopita yamekaa miaka mitano pekee?

Chaguzi za kutafuta ugombea wa nafasi mbalimbali ndani ya chama tangu mwaka 1995 ziligubikwa na matukio makubwa ya ukiukaji wa katiba ya chama hicho huku yakitoa mwanya kwa wenye uwezo wa kifedha kuwa ndio wenye msuli wa kuchaguliwa.

Hii inatokana na chama hicho kupoteza nguvu ya kumiliki serikali moja kwa moja hasa pale yalipofanyika mabadiliko ya Katiba yaliyoruhusu mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

CCM ilianza kujichunguza na kutafuta mbinu mpya za kusaka ushindi katika mazingira mapya. Eneo la matumizi makubwa ya fedha hasa wakati wa chaguzi ukianzia na zile za ndani lilikuwa jambo ambalo lilitoa tafsiri hasi kwa chama hiki.

Ukitazama kwa undani, wengi waliohamia vyama vya upinzani asilimia kubwa walikerwa na mfumo mbovu wa uchaguzi wa ndani ya chama hiki hasa kipengele ambacho sio rasmi kihusucho kutoa rushwa ili upate kupigiwa kura.

Ni jambo la wazi kuwa waliowahi kuwania nafasi za uongozi katika CCM wanafahamu vema adha ya kuombwa rushwa na wakati mwingine wanafahamu adha ya fedha katika kusaka madaraka katika chama hicho.

Mabadiliko yaliyolenga kutoa wawakilishi wa Halmashauri Kuu kutoka ngazi za mkoa na kuwapeleka katika ngazi za wilaya yalilenga kuongeza wigo wa kiushawishi wa chama hicho kwa wananchi. Tena maamuzi ya kuwatumia wanachama wote kupiga kura wakati wa kutafuta kupata wagombea ndani ya chama hicho yalilenga kukipa ahueni chama hicho ili kuepeka mzizi wa rushwa na pia kupata wagombea ambao kweli wanakubalika ili wapitishwapo iwe rahisi wao kushinda katika uchaguzi mkuu.

Taratibu mabadiliko ya kimya kimya yaliondoa mfumo huo ambao pia ulipaswa kutumika katika kupata wagombea urais, kama ilivyo kwa nchi za Marekani. Ikaelezwa kuwa, wenye nguvu ya fedha ndio wanaoweza kuwania nafasi hizo kwa kuwa wanaweza kuzunguka jimbo na hata nchi. Lakini CCM ikasahau adha iliyotokana na mtindo wa kuteka wajumbe wa mkutano wa wilaya na kisha kuwafungia eneo ili wasikutwe na mgombea mwingine hadi siku ya uchaguzi. Jambo hili likarejeshwa na likaachwa kimya kimya kutokana na chama kuona uendeshaji wa chaguzi za wanachama moja kwa moja una gharama kubwa. Lakini faida yake ilikuwa kukifanya chama kuzungumzika kwa wananchi na hivyo kuibua wanachama na mashabiki wapya.

Hivi majuzi Mwenyekiti wa chama hicho kafanya mabadiliko mengine. Mabadiliko ambayo unaweza kuyaita kuwa yanalenga kukirejesha chama hicho ndani ya chumba ilihali kilikuwa kimeshajitoa na kufika sebuleni. Mwenyekiti anatamba kuwa atakata majina ya kila mgombea ambaye ataelezwa kuwa anatoa rushwa. Mwenyekiti hataki kujua kuwa rushwa ina sehemu mbili, mpokeaji na mtoaji. Kama mpokeaji hajajiwekea mazingira ya kutaka kupokea, basi mtoaji atakuwa na wakati mgumu kumshawishi.

Kwa namna wengi wafahamuvyo, rushwa katika CCM inatokana na hali ngumu ya maisha ya watendaji wa chama hicho na hulka ya kudhani kuwa, kila anayegombea anatafuta mali hivyo wao ni lazima wapate mgawo wao kwanza kabla ya kufanikisha ulaji wa mgombea. Kuna kipindi fulani Makatibu wa Mkoa wa Jumuiya mbalimbali walipewa mlungula wa simu. Kila Katibu akaonekana akiwa na simu za aina hiyo zilizotolewa na mgombea mmoja. Hili ni tukio moja tu lakini yapo mengi yanayoambatana na hulka za mashabiki wa CCM ambao huwasema wagombea kuwa hawajawasalimia au kuwatembelea ikiwa ni tafsida ya kuwa hawajawapa chochote. Tena upo mtindo unaoakisi kuwa mwenye fedha kubwa ndiye hushinda, hivyo wagombea hushindana katika kutoa dau.

Mlungula katika chaguzi za CCM ni sawa na jua jangwani. Ni jambo ambalo limezoeleka na kukabiliana nalo kunahitaji mapinduzi makubwa na ikiwezekana kukifuta chama hiki kabisa. Siku za hivi karibuni tabia hii mbaya ya kutu imehamia na vyama vya upinzani. Hali hii huko imetokana na upepo wa urahisi wa kushinda kupitia huko ambako kwa namna kubwa wananchi hujikuta wakiwaaamini wagombea wa huko na kuwaonea huruma hivyo kutowaomba fedha au wakati mwingine kuwachangia kwenye gharama zao za kampeni.

Vladmir Ilych Lenin aliwahi kusema; hakuna serikali yoyote inayoweza kuishi bila kuwa na matumizi. Ni sawa pia kusema kuwa hakuna uchaguzi unaofanyika bila matumizi ya fedha. Lakini hali ngumu ya maisha ya Tanzania yanawafanya wapiga kura kutokuwa na imani na viongozi wanaowachagua kutokana na aina ya maisha wanayoishi wao na familia zao pale wanapopata madaraka. Tena, aina ya viongozi na tabia zao za kuwekana katika nafasi kwa urafiki, ukaribu uswahiba na mengine, yanafanya jamii kubwa kubaki na chuki ambazo haziwekwi hadharani. Kukosekana kwa ajira ni mambo yanayofanya jamii kutazama sana viongozi wa kisiasa na vyama vyao.

Wananchi wanatafuta mbadala na huenda katika kufanya hivyo ndio maana mwenyekiti wa CCM amekuja na mabadiliko yake yanayotaka watendaji wachache katika chama hicho sambamba na viongozi wachache. Mwenyekiti nadhani amefahamu kuwa alio nao wengi ni mzigo, hawana ushawishi na hawawezi kuleta mapya. Huenda ameona kuwa kama hataweza kuiba mbinu za kuendesha vyama kama wafanyavyo washindani wake, basi atakuwa anaongoza taasisi ambayo haifanyi siasa bali ipo katika ajira.

Lakini, kazi ya siasa ni pamoja na ushawishi. Kupunguza idadi ya nafasi kwako hakufanyi kuwa wapinzani wako nao walale au wakuige. Tatizo lililopo ni hali ya kuchokwa, kukosekna uhai mpya na tatizo hilo halijapatiwa tiba. Tiba yake inapaswa kuwa ile inayolenga kuyafikia makundi maalum na ambayo idadi yake inaongezeka ili yaweze kujiunga na chama hicho. Tena inatakiwa kutambua kuwa masuala ya siasa ni ushawishi, hayana bakora hivyo namna utendaji unavyofanyika katika serikali hauwezi kuwa sawa na ule wa kwenye vyama vya siasa.

Je, kwa mabadiliko haya tutegemee nini? Ni dhahiri CCM huko tuendako itayafuta mabadiliko haya. Kwa kuwa itakuwa inafanya kwa mara ya pili yanaweza yasikisaidie vema chama hiki. Misingi ya kero na kuporomoka kwa kutopendwa kwa chama hiki kunaambatana na mambo mengi na kubwa ni kushindwa kwa serikali kukidhi matakwa ya wananchi hasa katika masuala ya huduma za jamii na uimarishaji uchumi. Mabadiliko ambayo hayatazami kuifanya serikali kuwajibika zaidi kamwe hayawezi kuipa uhai CCM.

Tena katika zama hizi ambapo maendeleo ya kiushawishi na ufikishaji wa taarifa sambamba na kuongezeka kwa kundi kubwa linalotambua haki zake, vyama tawala vinatakiwa kuwa vibunifu na hasa pale vinapotakiwa kujiendesha bila kuonesha kuwa vinabebwa na serikali. Mbinu hii husaidia pale inapotokea serikali ikishindwa kutimiza majukumu yake vema.

Lakini pia, CCM inaweza kujikuta inabaki na wanachama na viongozi wake ambao watakuwa wanaugulia moyoni na kutokana na misingi isiyo thabiti iliyowajenga, misingi ya kuoneana haya, kufunikiana mambo, basi mabadiliko haya yanaweza kusawiri sana katika karatasi, yakapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya chama lakini yakashindwa kuwafikia wanachama na wapenzi wa chama hiki hasa wale wasio na nia za teuzi au kupata uongozi.

Rais John Magufuli

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.