Mangula atauziwa tena CCM ndani ya gunia!

Rai - - HABARI/TANGAZO -

MAIS Mstaafu Jakaya Kikwete aliyasema haya kuhusu chama chake alipokuwa akifunga mafunzo maalumu ya siku nne kwa makatibu wa CCM wa mikoa na makatibu na wenyeviti wa wilaya wa chama hicho nchini mjini Dodoma huko nyuma.

Kikwete alisema kuwa kama rushwa haitakomeshwa ndani ya chama hicho, katika Uchaguzu Mkuu utakaofanyika mwaka 2015, CCM itaanguka vibaya; na kama itanusurika, haitapita mwaka 2020.

Alimpa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, jukumu la kile alichokiita “kuwashughulikia bila aibu na huruma viongozi wala rushwa” ndani ya CCM ambao wanadaiwa kuwa mawakala wa kusambaza rushwa bila aibu na hivyo kufisha chama machoni mwa wapigakura.

Lakini iliulizwa wakati huo kama kweli Mangula angeliliweza jukumu hilo lililowashida waliokuwa wamemtangulia, akiwamo Rais wa zamani, Benjamin Mkapa, na Kikwete mwenyewe!

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema nini kuhusu serikali legelege na chama arijojo katika kitabu chake chenye kurasa 69 kinachoitwa “UONGOZI WETU NA HATIMA YA TANZANIA”? Kitabu hiki kilichapishwa na Zimbabwe Publishing House nchini Zimbabwe.

Kwa kunukuu sehemu ya kitabu hicho alisema:

“…Waingereza wana msemo: ‘Nature abhors a vacuum’, ‘hulka huchukia ombwe’. Hata siasa huchukia ombwe. Kama uongozi ni mbovu, upo kama haupo, au upo kwa masilahi ya wenyewe, watatokea watu waujaze uwazi uliopo; hauwezi kuachwa wazi vivi hivi. Lakini uongozi mbovu ni kama mzoga, una tabia ya kukaribisha mafisi na mainzi. Tusidhani kuwa hulka ya siasa yetu ni tofauti na hulka ya siasa ya watu wengine; kwamba sisi tunaweza kuvumilia uongozi mbovu na tusivune matunda ya hulka ya uongozi mbovu…

“... Serikali ni timu, na timu halisi ina dira na rubani. Mkusanyiko wa mawaziri bila mwelekeo, bila mwongozo, bila mshikamano na bila uongozi, kila waziri na lwake, hauwezi ukaitwa serikali. Katika hali kama hiyo, hata bila ubovu mwingine wa nyongeza, mambo muhimu ya nchi hayawezi kujadiliwa wala kushughulikiwa...

“…Pengine kwa nchi yetu hili lisingekuwa jambo la kutisha kama tungekuwa tumeanza kuona chama kizuri cha upinzani ambacho kinaweza kuiongoza nchi hii badala ya CCM. Hakijaonekana bado. Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa vyama vya upinzani, kinaweza kuendelea kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake…

“Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, “potelea mbali:” wakachagua chama chochote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa nchi yetu unataka yasemwe…

“…Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuoingoza nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio ulionifanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa vyama vingi.

“…Nilitumaini kuwa tunaweza kupata chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona chama makini cha upinzani; na wala dalili zozote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM.

“…Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu.”

Haya ni maneno ya Mwalimu Nyerere yaliyo katika kitabu chake kilichotajwa hapo juu, maneno ambayo sasa ni zaidi ya miaka 20 tangu ayatamke. Kwamba ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliomfanya Mwalimu Nyerere kupendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.

Kwamba alitarajia kuwa nchi ingeweza kupata chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi unaofuata.

Bahati mbaya aliposema maneno hayo wakati huo alikuwa bado hajakiona chama makini cha upinzani; na wala dalili zozote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Zaidi ya miaka 20 baada ya maneno haya ya Mwalimu Nyerere, angalau vyama vya upinzani kwa maana ya upinzani sasa vipo, na watu wengi wana imani navyo baada ya kukatishwa tamaa na CCM.

Rais Mstaafu Kikwete ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CCM yeye alikuwa amekata tamaa, rushwa ndani ya chama hicho ilishindikana, na akamtupia mzigo huo mzito makamu wake, mzigo ambao pia ulimshinda mtangulizi wake, Rais wa zamani Mkapa.

Rais Mkapa alimaliza muda wake wa kuliongoza Taifa hili na aliondoka. Kwa hakika alifanya mazuri mengi na anastahili kupumzika. Atakumbukwa kwa mengi, mazuri na mabaya. Kama mazuri yatazidi mabaya, basi mabaya yatafunikwa. Vile vile kama mabaya yatazidi mazuri, hayo mazuri yatafunikwa. Ingawa binadamu tulivyo, baya moja linaweza kufunika mema hata kama ni 1,000.

Kila rais kabla au mara tu baada ya kuingia Ikulu, huwapa matumaini makubwa wananchi katika masuala fulani yanayowakera, na pengine ambayo wanakuwa wamekata tamaa nayo katika maisha yao ya kila siku.

Kwa Tanzania, masuala ambayo yanawakera ni kadhaa, lakini suala ambalo kwa sasa wamekata tamaa nalo ni tatizo la rushwa. Wagombea urais wote kwa nyakati tofauti wamelisemea tatizo hili, akiwamo RaisMstaafu Kikwete na Rais wa sasa Dk. John Magufuli.

Rais Mstaafu Kikwete baada ya kuingia madarakani Desemba 2005 alifanya mabadiliko makubwa ndani ya chama na Serikali.

Eti alimwondoa aliyekuwa Katibu Mkuu wakati huo, Philip Mangula, na kumweka aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba.

Eti Mangula alirudi kwao Iringa kupumzika, kama ni kupumzika kweli. Mwaka 2007 Mangula huyo alijaribu kugombea walau uenyekiti wa mkoa huo, akadondoshwa puuu! Maskini!

Akaona pale hapatoshi, eti akajiendea kijijini kwake Kinenulo, kata ya Imalinyi, wilaya ya Njombe wakati huo. Bwana wee, kilimo hakimtupi mtu eti. Huko aliishia kulima mahindi na mazao mengine shambani kwake.

Akiwa hana hili wala lile, huku nyuma CCM ikaanza kuyumba chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu Makamba. Hadi unafika Uchaguzi Mkuu wa 2010, hali haikuwa nzuri kwani chama kilikuwa kimechafuka kwa kashfa za rushwa na ufisadi.

Mwaka 2011, Rais Kikwete akaangalia kule na huko! Mh, kwa kuepuka fedheha, alimwondoa Makamba katika nafasi hiyo na kumweka Wilson Mukama.

Kuingia kwa Mukama kulikuja sambamba na mkakati ‘kabambe’ wa kujivua gamba, na chama kiliwataka makada wake wajitafakari kisha wawajibike wenyewe.

Kumbe je ilikuwaje? Mukama pamoja na sekretarieti yake walianza kazi kwa moto, tena moto kweli kweli wakiwatia msukomsuko wale makada waliokuwa wakitajwa katika kashfa mbalimbali.

Makada waliotiwa msukosuko nao waligangamala, wakarusha ngumi, wakapangua kwa ustadi mkubwa zile ngumi zilizokuwa zinaelekezwa kwao. Wakabaki washindi.

Ndiyo, chama hakikufua dafu kwani makada hao walidinda; watuhumiwa, wengine pengine walikuwa wa kupikwa au vinginevyo, chama kikawagwaya. Hadi “kujivua gamba” kuliyeyuka kama ilivyoyeyuka “Ari mpya, Kasi Mpya na …?” Eh, wewe malizia bwana!

Mbali na Mukama kupambana kukisafisha chama bila mafanikio, alikuja kutemwa kwenye nafasi hiyo mwaka 2012, akawekwa Abdulrahman Kinana.

Kama hiyo haitoshi, safari hii Rais Kikwete alimkumbuka tena Mangula aliyemweka kando mwaka 2005. Eti alikumbuka uwezo wake kiuongozi na busara zake.

Akamrudisha asaidie kukipeleka chama hadi Uchaguzi Mkuu wa 2015. Mangula naye bila kusita akarudi kutafuna mfupa uliomshinda fisi. Eh, ndiyo uliomshinda fisi!

Alipoingia akakuta harufu za ufisadi hata kwenye chaguzi za ndani ya chama, hivyo akatoa miezi sita kwa wote waliotuhumiwa kuwajibishwa. Hakujua kuwa CCM ya wakati huo haikuwa ile aliyoiongoza enzi za Rais wa zamani, Benjamin Mkapa. Miezi sita ikapita, mwaka ukapita,… hakuna aliyeguswa.

Eti Mangula aliwaonya makada waliokuwa na mihemko ya kuutaka urais 2015 kuwa wasiwe na haraka ya kujitangaza!

Chama kikaunda kamati ya maadili na kuwaonya makada sita waliotuhumiwa kuanza kampeni za urais.

Baada ya kuonywa, kumbe ndiyo kwanza makada hao walianza mbio, walijipitisha huko na kule, na wengine wakawa wanatangaza nia kabisa!

Masikini Mangula alibaki amekodoa macho, bila kusema chochote, bila kuwa na cha kufanya! Mangula alikuwa kwenye mtanziko (dilemma), eti? Alikuwa ameuziwa CCM tena safari hii ikiwa kwenye gunia!

Rais wa sasa Dk. John Magufuli anaonekana ataisafisha CCM. Amekuwa Mwenyekiti wake tangu Julai mwaka huu, juzi ameifumua CCM na kubakiza watu karibu nusu eti wa kufanya kazi badala ya maneno tu! Tusubiri tuone!

Na Mangula bila shaka hatafanywa mtu wa kusafisha CCM bila nyenzo.

MASIKINI Mangula alibaki amekodoa macho, bila kusema chochote, bila kuwa na cha kufanya! Mangula alikuwa kwenye mtanziko (dilemma), eti? Alikuwa ameuziwa CCM tena safari hii ikiwa kwenye gunia!

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.