‘Visasi vinakwamisha upinzani kwenda ikulu’

Rai - - HABARI/TANGAZO - NA MWANDISHI WETU

SIASA za visasi na chuki, zimetajwa kuwa kikwazo kikubwa kwa vyama vya upinzani kufanikisha dhamira ya kukiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kauli hiyo imetolewa juzi na Mwenyekiti wa Chama cha United Peoples Democratic Party (UPDP). Fahmi Dovutwa.

Dovutwa alisema upinzani unayo nafasi kubwa ya kuingia Ikulu, lakini haitakuwa rahisi kama baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wataendelea kuishi na vinyongo, visasi na chuki dhidi ya watu wengine.

Kuhusu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) kuteuliwa na Rais, hatua inayoonekana kutoa nafasi ya upendeleo kwa chama kilichopo madarakani, Dovutwa alisema Tume huru ya uchaguzi haiwezi kusaidia upinzani wenye ubinafsi, vinyongo, chuki na visasi.

“Hata kama wapinzani wakidai tume huru, inaweza isiwe na athari katika mabadiliko ya kiuongozi iwapo viongozi wa vyama hivyo hawatoacha kunuia kulipiza kisasi.

“Kinachosababisha katika nchi nyingi za Kiafrika kushindwa kufikia malengo ya kisiasa ni kauli za viongozi kwamba watalipa visasi, sasa unapomwonesha kiongozi aliyepo madarakani kuwa ukishika dola utalipa kisasi, hawezi kukubali.

“Mfano mwaka 1995 Mrema alikuwa anachukua nchi, ila alisema akichukua nchi mali zote atarudisha kwa wenyewe sasa watu waliozaliwa tangu mwaka 1964 wamezikuta mali unasema utazirudisha kwa wananchi, akaongeza kwamba atafungulia vibaka pale Ukonga na kuwafunga viongozi. Kauli ile ilimuondoa kwenye uhalali wa kushinda,” alisema.

Aliongeza kuwa hata kwenye uchaguzi wa mwaka jana, Chadema ingeweza kushinda urais, lakini Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema mpaka saa nne watakuwa wamemaliza kila kitu.

“Mfano mwingine ni mwaka jana Chadema ilikuwa na nafasi kubwa ya kushinda, lakini alisimama Mbowe na kusema mpaka saa nne watakuwa wamemaliza kila kitu, CCM ni chama ambacho kimepigania uhuru, wana utaalamu mwingi sana wa mambo ya uchaguzi, akaja Marando na kusema asisikilizwe mtu yeye atatangaza matokeo, akaja tena bwana mkubwa na kuongeza kuwa atalinda kura mwenyewe… haya ni baadhi ya mambo ambayo yaliifanya CCM kubaini kuwa huenda yule mkurugenzi NEC ana mawasiliano na Chadema, akaondolewa wiki mbili kabla ya uchaguzi,” alisema.

Aliongeza kuwa kitendo cha kuweka vinyongo na visasi mioyoni mwa baadhi ya wanasiasa wa upinzani, kinawasababishia kuropoka hatua inayoishtua CCM.

“Kinachotuumiza ni sisi viongozi wa vyama vya upinzani ni kuropoka kunakochangiwa na visasi. Mfano Gambia matokeo ya uchaguzi yalishatangazwa, Rais aliyeanguka akakubali, cha ajabu wapinzani wakasema wakiingia madarakani jambo la kwanza ni kumfunga yule Rais… matokeo yake ameenda mahakamani kupinga matokeo, kwa hiyo matamshi yanawatisha wale waliopo madarakani.

“Wenzetu kama Marekani na Ulaya haya yote wameshaachana nayo, Trump alimshushua Obama kuwa alifanya makosa kuvamia Libya na kwingine ila hakusema kuwa atamfunga akiingia madarakani,” alisisitiza Dovutwa.

ACT : Katiba mpya ndio jibu

Hata hivyo hoja ya Dovutwa imepingwa na Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Anna Mghwira ambaye alisema kuwa nafasi ya uenyekiti wa NEC inapaswa kutamkwa kwenye Katiba Mpya.

Alisema ufanisi wa Mwenyekiti wa NEC, na nafasi nyingine zinazogusa masilahi ya vyama vya siasa lazima ufanyiwe mabadiliko na hili litawezekana kwa kubadili Katiba tu.

“Nafasi ya Mwenyekityi wa NEC kuongozwa na Jaji si jambo baya, kwa sababu wao ndio watafsiri wa sheria na wanajua namna ya kuamua na kuendesha mambo kwa mujibu wa sheria, Jaji ana mamlaka makubwa sana kwenye sheria.

“Lakini pia anaoufahamu wa mambo yanavyokwenda kwenye nchi hasa kisiasa. Malalamiko ya wananchi wengi ni kuhusu Tume yenyewe, naamini kama Mwenyekiti aliyechaguliwa angekuwa huru, angefanya mambo mazuri.

“Lakini kwa kuwa ndio ameanza tumpe nafasi tuone, ila mtu yeyote anaonekana kuwa mzalendo, anaweza kuitendea haki nafasi yake hata kama haijaandikwa kwenye Katiba yeye kama Jaji na raia mwema anaweza kuibariki nchi kwa kutenda haki,” alisema. Wanaohama ACT ruksa Kuhusu wanachama wanaokihama chama hicho, Mghwira alisema watu wanaotabiri anguko la chama chake hawajafanya tathmini ya kutosha.

“Uamuzi wa mtu kuhama chama haikikumbi ACT peke yake maana hata juzi baadhi ya wanachama wa Chadema mkoani Mbeya wamehama. Ajabu wanaoondoka ACT ndio wanaoonekana sana. Mtu kuhama chama hiki kwenda kule wala hainisumbui, ni kweli kwamba ndani ya vyama vya siasa kuna makwazo kama ilivyo kazini, kwa wakulima na wafugaji, ila huwezi kuona mkulima ameacha kulima kwa sababu ya migogoro na wafugaji.

“Siasa ni mapenzi, na huchanua, hunyauka na hufa, tusiangalie tu watu watatu ambao wametoka ACT, tuangalie pia walioondoka na Lowassa kwenda Chadema na wale waliotoka Chadema kwenda CCM na ACT.

“Kwa hiyo wanachama wetu niwaambie kila mtu atumie uhuru wake ipasavyo kama unaona una amani CUF nenda au Chadema nenda, kwa sababu ni kama ndoa, waliopo ndani wanataka kutoka na waliopo nje wanataka kuingia. Sio jambo la kujadili,”alisema.

KINGUNGE AONYA

Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru ambaye amejiondoa kwenye siasa za CCM, ameonya kuwa haitakuwa rahisi kwa upinzani kuingia Ikulu bila kuwa na Katiba Mpya.

Alibainisha kuwa bila ya kuwa na tume huru ya uchaguzi na Katiba Mpya, vyama vya upinzani visahau kushinda urais katika chaguzi zijazo.

Aliyasema hayo mbele ya vijana waliokamatwa na Jeshi la Polisi na kushtakiwa kwa makosa yaliyohusu Uchaguzi Mkuu uliopita.

“Yako mambo ambayo itabidi tujitahidi yaamuliwe sasa kabla ya 2020. Mambo hayo makubwa kwanza ni Tume Huru ya Uchaguzi. Suala hilo lazima lizungumzwe sasa, hatuwezi kwenda 2020 na tume ya sasa na Katiba ya mwaka 1977. Tukienda hivyo sahau habari ya upinzani kushinda uchaguzi,” alisema.

Alisema pamoja na kwamba Chadema inapendwa na wananchi wengi na Edward Lowasa aliyegombea urais kwa tiketi chama hicho nae anapendwa, bado ni vigumu kushinda kwa sababu mfumo uliopo sasa hautoi nafasi hiyo.

“Tufanye yoyote, lakini tuhakikishe, ama tunapata Katiba Mpya au vipengele hivi vya sheria vinafanyiwa marekebisho. Kwa maoni yangu, kundi hili lililo madarakani bila shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi, halitataka mabadiliko,” alisema.

UTEUZI WA JAJI KAIJAGE

Uteuzi wa Mwenyekiti mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage uliibua mjadala.

Jaji Kaijage alichukua nafasi ya Jaji mstaafu, Damian Lubuva, ambaye amestaafu.

Kwa muda mrefu, NEC imekuwa ikilalamikiwa na vyama vya upinzani kwa kutokuwa huru kwa sababu ya uongozi wake wote kutokana na uteuzi wa Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, huku sheria zikikataza matokeo ya nafasi ya urais kupingwa mahakamani.

Mbali na mwenyekiti kuteuliwa na Rais, wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo ni wakurugenzi wa wilaya ambao pia huteuliwa na Rais kwa kuwa NEC haina wafanyakazi wake kote nchini. Pamoja na hayo, Jaji Kaijage aliwatoa hofu wapinzani na kuwaahidi utendaji unaozingatia sheria na katiba ya nchi.

“Nitafuata sheria, taratibu na kanuni zinazoongoza Tume ya Uchaguzi. Hakuna namna nyingine ya kumpata mwenyekiti wa tume ya uchaguzi kwa sasa hivi, lazima katiba iongoze na apatikanaje. Nitahakikisha taratibu za uchaguzi kwa mujibu wa kanuni na taratibu za tume hiyo zinafuatwa,” alisema.

Zitto Kabwe na Anna Mghwira.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.