Nausubiri uzalendo wa Polepole ndani ya CCM

Rai - - MAKALA - NA LAMU PASCAL ELIZAYO KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI. lamuelizayo@gmail.com +255766033331

HUMPHREY Polepole ni kijana jasiri mwenye mawazo chanya, mwenye kujenga hoja barabara, hongera sana kwa kuaminiwa na viongozi wa chama changu.

Humphrey nikitupia jicho kwenye historia yako hasa mchakato wa Katiba mpya na Uchaguzi Mkuu wa 2015 napata matumaini ya aina yake japo sijui kama utaishi katika historia yako ya kizalendo ukiwa na kofia yetu ya kijana kichwani.

Natamani sana uzalendo wake na ujasiri wake aliouonesha katika mchakato wa Katiba mpya na Uchaguzi Mkuu wa 2015 ulete mabadiliko makubwa ndani ya chama hasa katika maeneo haya

Mosi, wakumbushe wabunge wa CCM waache tabia ya ndiyo mzee, tunasubiri uzalendo wako na ujasiri wako ukomeshe kabisa tabia ya wabunge kujadili na kupitisha miswaada kwa kukifiria chama kuliko Taifa, komesha tabia ya wabunge kutunga sheria kandamizi kwa masilahi yao wakumbushe wabunge watambue Taifa letu ni muhimu zaidi kuliko siasa zetu, ishi katika uzalendo wako waambie kazi ya mbunge siyo kusema ndiyo mzee, naunga mkono hoja, wakumbushe wasiitikie kila kitu wajadili hoja mbalimbali kwa kufikiria wananchi wao kuliko siasa zao wasipitishe bajeti zisizotekelezeka, wakumbushe na kusema nao kusema ukweli siyo usaliti ni uzalendo. Ulisema ukweli juu ya madhaifu na madhambi ya wagombea urais, ubunge na udiwani 2015 mpaka ukatangaza kuwapinga endapo wangepitishwa na chama chetu wagombea, ulisema ukweli kuhusu aina ya muungano kwenye mchakato wa Katiba mpya hakika huwezi kushindwa kukemea tabia ya ndiyo mzee ya wabunge wetu wa CCM.

Pili, kifanye chama chetu kiwe chenye kuisimamia serikali kuliko kusimamiwa na serikali, tunahitaji uzalendo wako ulete mabadiliko makubwa CCM iweze kutoa maagizo kwa serikali kama chama tawala siyo kufuata maagizo ya serikali, tunasubiri uzalendo wako na ujasiri wako upenye kwa viongozi na wanaCCM waweza kuisimamia serikali yetu itekeleze ahadi kwa mwananchi, CCM iwe na sauti ya kukemea viongozi wanaoshindwa kutatua kero za wananchi, CCM iwe na uwezo wa kumwajibisha kiongozi anayeshindwa kufuata ilani ya uchaguzi, CCM isiwe ya kufuata maagizo haiwezekani CCM impe fursa kiongozi halafu ghafla ageuke nakufanya ajuavyo, tunahitaji CCM ikitoa agizo dhidi serikali kumaliza tatizo la maji na iwe hivyo, CCM ikitamkata kiongozi yeyote wa serikali anayetokana na CCM afanye jambo lenye manufaa kwa wananchi na iwe hivyo, haiwezekani CCM itoe ilani halafu viongozi wafanye wajuavyo wao. Polepole tunasubiri uzalendo wako ukiwa na kofia ya kijani, rejesha CCM iliyo mathubuti yenye kusema kwa niaba ya wananchi dhidi ya serikali.

Tatu, tunasubiri uzalendo na ujasiri wako vikomeshe na kumaliza rushwa ndani ya chama chetu katika hili simama na katibu mkuu wetu, shikamana na m/kiti wetu kurejesha CCM iliyo mbali na rushwa nina hakika unajua vizuri, unaelewa vema namna rushwa inavyotemea kwenye chaguzi, unaelewa namna fedha inavyokuwa kipimo cha uongozi, unaelewa namna bahasha za kaki zinavyopishana kwenye uchaguzi, unajua vizuri namna fedha inavyokuwa muhimu kwenye michakato ya uchaguzi. Humphrey shikamana na katibu mkuu wetu anza na uchaguzi wa CCM wa 2017, komesha rushwa kabisa tunasubiri uzalendo wako uwachape bakora wala rushwa ndani ya chama chetu kiwe chama chenye kuchukia rushwa, katika hili nina imani m/kiti wetu atakupa ushirikiano mkubwa.

Nne, Tunasubiri utusaidie kumaliza utata hivi sisi ni wajamaa au mabepari, haiwezekani kwenye Katiba yetu ya chama tuwa wajamaa halafu tunaishi kibepari kwani ni dhambi kurekebisha na kuboresha katiba na kanuni zetu ili tuendane na mabadiliko ya dunia, japo tupo kimya lakini tunajiuliza kimya hivi sisi ni wajamaa au mabepari, kwanini tujiweke huru kuliko kujidanganya wenyewe, kama bado tunapenda ujamaa wa Mwalimu Nyerere basi tuwe wajamaa kweli kweli siyo kwenye makaratasi wajamaa huku maisha yetu ubepari. Humphrey kachokoze mjadala huu tujue ujamaa umekufa au bado upo.

Tano, tunasubiri uzalendo wako uwakumbushe wanaCCM wenzetu waache dhambi ya unafiki nakujipendekeza , wasiogope kufikisha matatizo ya wananch kwa viongozi, wakumbushe viongozi wetu wa CCM wasiishie kunywa chai nakupiga picha pamoja na viongozi wetu , wakumbushe kwenye viongozi wafikishe changamoto za wananchi kwenye vikao wasiende kupongeza na kupiga vigelele kuwafurahisha viongozi, waseme ukweli changamoto za wanaCCM wa chini wanapigania chama kwa moyo pasipo malipo wala masilahi zaidi ya penzi mema ya chama chao. Humphrey tunasubiri ujasiri na ushupavu wako upoteze na kutokomeza kabisa unafiki na kujipendekeza kwa baadhi ya wanachama wenzetu, uliweza kusema ukweli kwenye uchaguzi mkuu, uliweza kusimama na kusema kijasiri mbele ya wazee kwenye mchakato wa katiba mpya nina imani hutoshindwa kuwasema na kuwanyooshea vidole wanafiki wanaopeleka pongeza na sifa kwa viongozi kwenye vikao huku changamoto walizotumwa wapeleke wakitupa shimoni kisa tu waonekane wema, kutokomeza unafiki ndani ya chama Humphrey hakika unafiki unachelewesha majibu ya changamoto zetu wakati mwingine viongozi wetu hawapati taarifa sahihi .

Sita, Humphrey Polepole nenda uwakumbushe viongozi wetu CCM hatupo pekee yetu, kuna vyama vya upinzani wanasubiri madhaifu yetu na uzembe wetu tafadhali kaseme nao waache makosa ya makusudi, waache kuonesha madhaifu yasiyo ya lazima maana ni faida kwa wapinzani wetu, wakumbushe juu ya kauli zao za kuchukiza, wakumbushe juu ya ahadi zao za kusadikika, wakumbushe juu ya uzembe wao wa wazi wazi sema nao kijasiri na kizalendo kama ilivyo jadi yako. CCM hatupo wenyewe kuna wenzetu hawalali wanakesha wakipasha misuli tusibweteke, tuwadharau, tusiishi kwa mazoea , tujione tupo wenyewe , wakumbushe wafanye kazi kwa juhudi, kwa kujituma na kujihami na wapinzani wetu ili tubaki salama. Saba, Humphrey Polepole nenda karudishe CCM wenye kuaminiana na kuheshimina kakomeshe chuki zitokanazo na makundi ya uchaguzi, kawakumbushe vijana kuna maisha baada ya uchaguzi, waambie siyo dhambi kumuunga mkono mgombea umependae kwenye mchakato wa chama, dhambi na usaliti ni Kumpinga mgombea aliyepitishwa na chama, wakileta kiburi na ubishi wakumbushe mapenzi aliyeonesha Dk. Emmanuel Nchimbi kwenye mchakato wa chama kupitisha mgombea baada akaweka mapenzi pembeni akamuunga mkono mgombea wa chama chetu (JPM), waambie vijana siasa siyo chuki waache tabia ya kutukana na kushambuliwa hovyo viongozi wetu kisa tu makundi, ijenge CCM iliyo moja tokomeza tabia ya wanaCCM baadhi kujiona bora kuliko wenzao. Kajenga CCM moja Humphrey uzalendo wako sina mashaka nao.

Nane, kamsaidie m/kiti wetu na katibu mkuu wetu kusimamia mali za chama chetu, tunasubiri uzalendo wako ulete changamoto kufufua viwanja vyetu vya michezo, tunasubiri uzalendo wako umsaidie m/kiti wetu tupate faida ya majengo yetu, tujue matumizi sahihi ya rasilimali zetu, tunasubiri uzalendo na ujasiri wako Humphrey kawanyooshee vidole viongozi wasio waadilifu wanajimilikisha mali za chama chetu, nenda kawashughulikie katika hili m/kiti na katibu mkuu wetu nina hakika hawatakuangusha tazama viwanja vya michezo kila mkoa vimeguka vichaka, tazama majengo yetu mikoani wamefugia kuku, tazama mashamba yetu wamejimilikisha, ona kule majengo yetu wamepangisha na pesa wanakula kama zao.

Tisa, Uoneshe uzalendo wako kwa kukemea bila woga tabia ya wanaCCM baadhi kudhani CCM ni mwamvuli wa kukwepa kodi na kufanya biashara kimagumashi, shikamana na katibu wetu mkuu kuondoa kabisa makada masilahi wanadhani CCM ni sehemu ya kulindwa na kufanya mambo ya hovyo yasiyo na tisa kwa umma, kawapinge wazi wazi wanaodhani CCM ndiyo sehemu yakupatia tenda na kandarasi kiholela bahati nzuri katika hili m/kiti wetu atakuwa na wewe maana hapendi madili nenda kawanyooshee vidole kawaambie CCM siyo chama cha madili.

Kumi, Humphrey Polepole hii ni ngumu kidogo lakini hakuna namna tunasubiri uzalendo na ujasiri wako ukachokoze na kuibua mjadala wa maendeleo ya mchakato wa KATIBA MPYA, nenda kamsihi m/kiti wetu umuhimu wa katiba inayoendana na mabadiliko ya dunia mwambie hata yeye atapata wepesi wa kazi, katiba mpya yenye kusimamia maadili ya utumishi wa umma itamsaidia yeye na wengine wajao, katiba yenye kuzuia mrundikano wa vyeo itamsaidia mpaka yeye, katiba yenye kuwapa Mamlaka wananchi dhidi ya viongozi inamsaidia kuwatetea wanyonge, nenda kuoneshe uzalendo na ujasiri wako wa asili usio na shaka. Humphrey usiogope tafadhari sisi tunasubiri kwa hamu ufufuo wa agenda hii muhimu kwa kila mtanzania mpenda uadilifu, uwajibikaji na uongozi wenye kufikria taifa na watu wake. Mwambie m/kiti bila Katiba inayoendana na matarajio yetu kiongozi ajaye asipokuwa na nia njema anaweza kuvuruga mazuri yote unayoyaweka, anaweza kuvunja misingi imara unayoweka sasa, mwambie Katiba mpya ni majibu ya kudumu ya misingi anayopigania sasa bila hivyo ajaye anaweza kufanya atakavyo na kuachana na haya mazuri yote .

Humphrey Polepole, tunasubiri kwa hamu kushuhudia ubora wako usio na shaka katika kusema ukweli na kuusimamia kizalendo bila kujali matokeo yake , tuna hakika ulichofanya kwenye uchaguzi mkuu haikuwa nguvu ya soda na tuna imani ulichofanya kwenye mchakato wa Katiba mpya ndiyo maisha yako, nenda kijana mwenzangu kaoneshe uzalendo na ujasiri ukiwa na kofia ya kijani, nenda kaseme ukweli, nenda kiongozi ninayaona mafanikio makubwa usoni mwako.

Kila la kheri Humphrey Polepole tupo nyuma yako na Mungu akutangulie, kaijenge CCM yetu kwa uadilifu na uzalendo mtukufu.

Humphrey Polepole

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.