Ujio wa Trump 2016 na hofu ya 2017

Rai - - MAKALA - NA MWANDISHI WETU

Marekani imepata rais wa 45 na mwakani Januari 20, 2017 ataapishwa rasmi kuwa rais wa Marekani. Donald Trump mfanyabiashara bilionea ameshinda urais wa nchi hiyo akipata kura za jumla chache kuliko mgombea wa Democrats, Hillary Clinton.

Ushindi wa Trump umejadiliwa kila kona ya Dunia na jambo hili linaweza kuonesha kuwa nafasi ya Marekani katika siasa za dunia bado ni kubwa ukilinganisha na mataifa mengine makubwa kama China. Marekani anapata faida kubwa ya kutumia lugha ya Kiingereza, lugha inayozungumzwa na wengi duniani huku China akikosa fursa hiyo kufuatia lugha yake kutotanuka.

Uchaguzi uliomuweka Barack Obama madarakani miaka nane iliyopita nao ulikuwa na hamasa kubwa maana wengi walitamani kuona nchi hiyo ikiandika historia mpya ya kuwa na rais wa kwanza mwenye asili ya Afrika. Baba wa Barack Obama anatokea Kenya.

Ushindi wa Trump umeanza kuonesha cheche duniani na inawezekana nafasi ya mahusiano ya Marekani na nchi nyingine duniani yakaanza kupungua. Inawezekana kabisa mahusiano haya kuwa dhaifu kuliko hata yalivyokuwa wakati wa urais wa George Bush, rais wa 43 wa nchi hiyo aliyetokana pia na chama cha Republican ambacho Trump ameshinda urais kupitia tiketi yake.

Tayari taharuki ya kwanza imeshajitokeza. Marekani inailamu Russia kuingia uchaguzi wake na kufanya udukuzi. Madai haya yanathibitishwa na FBI na Rais Obama ameyatolea kauli. Licha ya kutolewa kauli hiyo hayakuweza kubadili matokeo na hivyo Trump ameshapigiwa kura na ‘electoral college’ na hivyo ni rais rasmi nayesubiri kuapishwa.

Wakati hayo yakifanyika Trump kamteua Bosi wa Exxonmobil, Rex Tillerson kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani. Tillerson anatajwa kuwa mfanyabiashara mwenye uhusiano wa karibu na Vladmir Putin Rais wa Russia. Uhusiano wao upo katika biashara na hata kijamii. Jambo la Trump kumteua swahiba wa Urusi inaelezwwa kuwa ni kiashirio cha Trump kuwa nyuma ya Putin na kwamba huenda alijua kuwa udukuzi wa kura ungefanyika kwa maslahi yake. Hata hivyo Tillerson atapitia kipindi kigumu ili kuthibitishwa na Seneti ya nchi hiyo kabla ya kuapishwa kushika wadhifa huo.

Vladimir Putin amenukuliwa hivi karibuni akijidai kwa kusema: “ni sisi peke yetu tuliyefahamu kuwa atashinda hivyo tukaungana naye. Wengine wote wameshangaa kuona alishashinda.” Kauli hii inaashiria kuwepo mazingira ya karibu kabisa katika udukuzi wa kura kwa baadhi ya majimbo na kwamba Putin alikuwa akisimamia jambo hilo moja kwa moja.

Hivi karibuni amekinzana na Israel, taifa linaloelezewa kuwa karibu kabisa na Marekani kuliko mataifa mengine kutokana na kuwa na wafanyabiashara wakubwa walioko Marekani wenye asili ya nchi hiyo. Ukinzani wa Trump na Israel unatokana na suala la ujenzi wa makazi ya walowezi jijini Jerusalem ambapo Marekani imekalia kimya kutoa msimamo wake, jambo ambalo Israel haikulitegemea.

Tena ameonekana kukwaruzana na China kuhusu uwazi na ukweli katika uwekezaji na biashara ya kimataifa. Hali hii inaonesha kuwa katika utawala wa Trump Mchina hatakuwa na nafasi ya majadiliano kwa vile Trump anamtaja bayana kuwa anafanya biashara duniani katika mazingira yasiyo ya uwazi na usawa.

Kama hiyo haitoshi Trump ameshatoa kejeli kuhusu Umoja wa Mataifa akiuita Umoja wa kukutana na kufanya sherehe. Maana halisi ya kauli hii ya bezo ni kuwa Trump anatangazia dunia kuwa atakuwa rais anayetazama kwanza Marekani pasipo kubaini kuwa Marekani inagusa kila kona ya dunia. Lugha nyepesi unaweza kusema Marekani ni dunia na dunia ni Marekani.

Tayari Trump ashaonekana mtu asiyekubalika na hata na majirani wa Marekani kama Mexico. Utamaduni wa Marekani na nchi jirani ni kuwa viongozi wa nchi hizo hufanyoana ziara za kitaifa punde tu wakichaguliwa. Trump atakuwa na wakati mgumu kuzuru Mexico kufuatia sera yake ya kutaka kujenga uzio baina ya nchi hizo ili kuzuia wahamiaji kutioka Mexico kuingia Marekani. Kwa mujibu wa Trump Mexico inaleta wahamiaji wenye sifa za matumizi ya dawa za kulevya wenye tabia zisizofaa nk.

Hata hivyo

mambo ambayo wachambuzi wengine wa siasa a kimataifa wanayatazama ni namna ya kuingiza kipengele cha uendeshaji wa shughuli za kibiashara na hasa makampuni katika uendeshaji wa serikali. Trump hatokani na wanasiasa wa Washington na kimsingi kawashinda katika uchaguzi huu.

Wengi wanatarajia kuona akileta mabadiliko ya namna ya kuendesha serikali ili zitengeneze faida. Tayari ameshatamka kuwa kazi yake kubwa itakuwa kufanya mikataba yenye tija kwa Marekani na kuhakikisha kuwa tija hiyo inatumika kusaidia Marekani. Ameshazungumzia kuhusu suala la kutoza kodi kubwa kwa bidhaa zinazoingia Marekani na kupunguza kodi kwa zile zinazozalishwa ndani ya Marekani.

Kutokana na hali hiyo ni wazi kuwa sera za Trump zinaweza kusaidia kuboresha hali ya maisha na hasa kuongeza kazi ndani ya Marekani na wakati huo huo zikaathiri sana hali ya uchumi kwa nchi ambazo zilitegemea kupata soko la Marekani au kupata uwekezaji humo.

Kwa upande wa Ulaya ni dhahiri kuwa uhusiano wa Trump na Putin utafanya mahusiano na NATO kuyumba. Kuyumba huku kutachangia hata katika uchumi na kunaweza kabisa kufanya mataifa hayo kubakia yakishughulikia masuala yao ya ndani na kujihusisha kidogo na masuala ya nje.

Muathirika mkubwa katika matokeo haya atakuwa Afrika. Afrika inaendelea kukosa misaada iliyokuwa ikiitegemea na Trump anataja hadharani kuwa viongozi wa Afrika wengi wao hawajui wanachokifanya na kwamba bado wanalazimisha kutawala kwa maslahi ya wachache.

Ni wazi pia kuwa dunia itakuwa katika kipindi cha sintofahamu na uwekezaji utapungua. Upo uwezekano ununuzi wa silaha ukawa ni agenda ya nchi nyingi maana kumeanza kuwepo aina ya siasa zilizoasisiwa na Trump katika nchi nyingi kama Australia na Ujerumani ambapo wananchi huko wanaonesha waziwazi vita dhidi ya wahamiaji. Tena, viongozi wanaohubiri chuki na dharau baina ya watu wanaonekana kuanza kukubalika tofauti na ilivyokuwa awali.

kutoka

nchini

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump (kulia) akiwa na Hillary Clinton

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.