CONGO DRC: Wapinzani wamvutia pumzi Rais Kabila

Rai - - AFRIKA - KINSHASA, DRC

Mwisho rasmi wa vipindi viwili vya utawala wa Rais Joseph Kabila wa Congo DRC viliisha siku kumi zilizopita (Desemba 19 2016) kufuatana na Katiba ya nchi hiyo.

Siku hiyo ilikuwa inatangazwa sana kwamba itakuwa ni siku ya kuanza kwa vurugu kubwa na ghasia, lakini haikuwa hivyo kwani hali ilibakia kuwa tulivu katika maeneo mengi ya nchi hiyo.

Hii ilitokana na kuwekwa kwa vikosi vingi vya usalama katika barabara za miji mikubwa na sehemu nyingine, hatua ambayo mara nyingi huwaogopoesha wananchi wa nchi hiyo.

Wanaharakati wa masuala ya siasa na haki za binadamu wamedai kwamba mamia ya watu walitiwa mbaroni katika kipindi kuelekea siku ya mwisho ya utawala wa Kabila, na mamia wengine wamezuiliwa baada ya hapo.

Hata hivyo mwezi Septemba, makumi ya watu walipigwa risasi na kuuawa katika mitaa ya Kinshasa wakati wa maandamano makubwa ya kupinga azma ya Kabila ya kujiongezea muda wa kukaa madarakani.

Tukio hilo lilionekana kama ni onyo kutoka kwa utawala kwamba upinzani wowote utakaojitokeza baadaye hautavumiliwa kamwe na utashughulikiwa vilivyo na vyombo vya dola, onyo ambalo lilitekelezwa Desemba 20 2016, siku moja baada ya kwisha kwa muda wa Kabila. Siku hiyo waandamanaji 20 walidaiwa kuuawa walipokwa wakipambana na vikosi vya usalama katika miji mbali mbali nchini.

Matukio haya na mengine ambayo hayakuripotiwa, pamoja na aina nyingine za upinzani katika maeneo yasiyotarajiwa yanatoa ishara ya mambo yanavyoweza kuwa katika wiki au miezi michache ijayo. Badala ya kutarajia maandamano makubwa makubwa katika miji mikubwa ya Congo, inaonekana kama vile nchi inasogelea aina nyingine ya upinzani usiotarajiwa.

Maandamano ya ghafla ya hapa na pale yameibuka katika maeneo yasiyotarajiwa, na mengi ya haya siyo yale ya kawaida ambayo huitishwa na vyama vya upinzani.

Wananchi wa tabaka mbali mbali wameanza kuubeza uhalali wa utawala wa Kabila na mawakala wake. Baadhi ya maandamano ya aina hii yameonekana kuingiliwa kimasilahi na wadau mbali wa kisiasa, hali ambayo inaashiria kuanguka, aghlabu pole pole kwa nguvu ya kisiasa na za kijeshi. Na hili litakuwa ni vigumu kwa utawala kulikabili.

Na wakati huo huo, Maaskofu wa Kikatoliki wamekuwa wakizidisha juhudi zao za kuziba mianya iliyopo kati ya utawala na vikundi vya upinzani.

Baada ya kupumzika kwa siku nne na juhudi nyingine kadha ambazo hazikufanikiwa, mazungumzo haya yanayolenga kufikia muafaka wa kisiasa kuhusu mchakato wa kuwepo kwa utawala wa mpito hadi uchaguzi, zitaendelea tena wiki ijayo.

Hata hivyo juhudi za Maaskofu tayari zimeshaanza kudhoofishwa, kama siyo kuzuiwa kabisa, baada ya kuteuliwa kwa serikali mpya ya Waziri Mkuu Samy Badibanga, iliyotangazwa dakika kabla ya Desemba 19.

Kutangazwa kwa serikali hiyo ya mpito ilionekana kama ni mbinu ya kupotezesha lengo, lakini katika mtazamo mwingine ni kuongeza tu kwa harakati za upinzani nchini.

Kushindwa kwa upinzani kuhamasisha maandamano makubwa Desemba 19 ulionyesha udhaifu wake wa kuzigeuza hasira kubwa walizonazo wananchi kuwa nguvu kubwa dhidi ya utawala, hasa katika miji mikubwa mbali mbali nchini.

Hata hivyo hasira hizi si kwamba zimepotea, bali zipo sana tu na zinaongezeka siku hadi siku, zikisukumwa na hali mbaya ya uchumi. Kushuka kwa thamani ya Franc ya Congo ndani ya muda mfupi kumeathiri sana uwezo wa wananchi wa kawaida kupata mahitaji yao ya lazima. Aidha hali hii pia imeanza kuwaathiri wale wananchi walio katika tabaka la kati.

Hali hii ya uchumi imeathiri sana mapato ya serikali ambayo sasa hivi hayatoshi kulipia mishahara ya watumishi wa umma, pamoja na gharama za vikosi vya ulinzi na usalama.

Hii ina maana ya kwamba serikali sasa hivi haina uwezo kabisa hata wa kugharamia mchakato wa kuendesha zoezi la uchaguzi.

Hali kadhalika hali hii ya ukosefu wa fedha itaathiri utoaji wa huduma muhimu za jamii kama vile ni9shati ya umeme na maji, huduma ambazo zitazidi kuongeza hasira za wananchi kwa utawala wao.

Mapungufu haya yanaonekana zaidi katika miji mikubwa ya nchi hiyo, lakini pia utawala unapaswa kuangalia hali katika maeneo ya vijijini, hasa maeneo ya mashariki.

Huko bado kuna harakati za mashambulizi madogo madogo ya vikundi vyenye silaha dhidi ya vikosi vya serikali silaha. Aidha kuna vikundi vya kikabila ambavyo siku zote vimekuwa vikileta uvunjifu wa amani mbali na suala lile la ukomo wa kipindi cha utawala cha Rais Joseph Kabila.

Katika siku za karibuni makundi mapya yenye silaha yameibuka, huku mengine yakiamua kuungana – kwa mfano baina ya makundi yenye silaha ya Bafulero na Babembe katika maeneo ya Uvira na Fizi, na makundi mengine huko Batembo na Kalehe.

Makundi yote haya ymekuwa yakijiweka sawa na kujiimarisha kwa kueneza himaya zao. Harakati zao zimekuwa zikiulenga utawala wa Kabila, lakini pia husukumwa zaidi na siasa za maeneo husika na maliasili zilizopo.

Wakati uhalali wa utawala unavyozidi kupungua, vikundi hivi vinajizatiti na kujionyesha kwamba ni mbadala wa utawala wa Kabila.

Hivyo kwa ujumla mgogoro unaoendelea nchini na habari za kuwepo kwa uchaguzi utazidisha tu ushindani wa kisiasa.

siku za karibuni makundi mapya yenye silaha yameibuka, huku mengine yakiamua kuungana – kwa mfano baina ya makundi yenye silaha ya Bafulero na Babembe katika maeneo ya Uvira na Fizi, na makundi mengine huko Batembo na Kalehe.

Rais Joseph Kabila

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.